STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 19, 2013

Salum Sued 'Kussi' arejea dimbani akisubiri kwa hamu duru la pili

Amerudi! Kussi (kushoto) akiwajibika katika moja ya mechi za timu yake ya Mtibwa Sugar kabla ya kuumia

BEKI wa kati wa kutumainiwa wa Mtibwa Sugar, Salum Sued 'Kussi', aliyekosa sehemu kubwa ya duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kuwa majeruhi amepona na sasa anajiandaa na duru lijalo la pili.
Akizungumza na MICHARAZO, Kussi, aliyewahi kuwa nahodha wa Taifa Stars kwa miaka mitano mfululizo, alisema kuwa majeraha yaliyokuwa yakimuandama na kumfanya asiitumikie timu yake duru lililopita yamepona na ameanza kujifua.
Nahodha msaidizi huyo wa Mtibwa, alisema japokuwa mazoezi ya pamoja ya klabu yake hayajaanza rasmi, lakini yeye anaendelea kujifua kwa sasa jijini Dar es Salaam ili kujiweka fiti kwa duru lijalo ambalo amelipania ili kuisaidia klabu yake.
"Baada ya kuwa nje ya dimba kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi nashukuru nimeanza kujifua mwenyewe mtaani kwa sasa kujiweka fiti zaidi kabla ya kuanza mazoezi ya pamoja kujiandaa na duru la pili," alisema Kussi.
Aliongeza ana hamu kubwa ya kurudi tena uwanjani kuipigania timu yake ambayo ilimaliza duru la kwanza ikishika nafasi ya sita kwa kukusanya jumla ya pointi 20 kutokana na mechi 13.
Kussi aliyewahi kuzichezea klabu za Yanga na Azam, alipata majeraha hayo mapema mara baada ya kuanza kwa duru la kwanza na kumfanya kushindwa kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu.
Beki huyo mrefu alisema anaamini duru lijalo litakuwa gumu na hivyo ni lazima ajiweke vyema zaidi kuhakikisha Mtibwa inamaliza katika nafasi nzuri wakati ligi hiyo itakapomalizika Aprili mwakani.

Abdi Kassim 'Babi' achekelea kurejea soka la kulipwa

Babi alipokuwa Azam

Babii (kulia) akiwa na kocha wake binafsi wa mazoezi ( Gym) Amir nchini Malaysia
Abdi Kassim alipokuwa akisaini mkataba wa kuichezea UiTM Fc
KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa klabu za Mtibwa, Yanga na Azam, Abdi Kassim 'Babi' amefurahia kupata nafasi nyingine ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi baada ya kufanikiwa kusajiliwa na klabu ya Ligi Kuu ya Malaysia, UiTM Fc.
Babii anayefahamika pia kama Ballack wa Unguja, amesema kufanikiwa kurejea kwenye soka la kulipwa kwa mara nyingine ni uthibitisho kuwa soka lake bado wamo isipokuwa mizengwe ya kandanda la Tanzania ndiyo inayomfanya asipewe heshima inayostahiki.
Akizungumza na MICHARAZO toka Malaysia, Babi alisema anamshukuru Mungu kwa kutua UiTM timu inayomilikiwa na Chuo cha Teknolojia na kumuomba amuongezee umri mrefu ili atumikie kipaji chake cha soka.
Alisema kabla ya hapo tangu alipotua KMKM akitokea Azam aliokuwa ameachana nao kuna watu walikuwa wakimwekea mizengwe na kutofurahishwa na kusajiliwa kwake katika klabu hiyo, lakini alipigana na hatimaye Mungu amemfungulia neema na kupata timu hiyo ya UiTM.
Babi alisema kwa namna anavyokithamini kipaji chake na kuhakikisha anakilinda kisichuje haraka anaamini ana miaka 10 ya kuendelea kucheza kandanda.
"Naamini nina miaka kama 10 ya kuendelea kucheza kwa sababu najiamini na ninaweza soka, namshukuru sana Mungu , wazazi na wote waliopo nyuma yangu katika mafanikio na jitihada zangu za soka," alisema.
Nyota huyo kabla ya kusajiliwa Azam alikuwa akicheza soka la kulipwa katika klabu ya Dong Long Tam An aliyoichezea kwa muda mfupi lakini akiifungia mabao 7.
Akiwa Azam, Babi anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye uwanja wa Taifa walipoumana na Uganda, aliifungia bao la kwanza kwenye michuano ya Kimataifa dhidi ya Al Nasir Juba waliposhiriki Kombe la Shirikisho.

Spurs majanga, Man Utd wakifuzu Nusu Fainali Capital One

Adebayor akishangilia bao lake la jana

Ashley Young akishangilia bao lake dhdi ya Stoke City
TOTTENHAM licha ya kucheza nyumbani ikiwa na kocha mpya, Tim Sherwood ilijikuta iking'olewa kwenye michuano ya Capital One baada ya kunyukwa mabao 2-1 na West Ham United.
Bao la utangulizi la mshambuliaji toka Togo, Emmanuel Adebayor lilishindwa kuilinda wenyeji kuvuka Nusu Fainali bila ya aliyekuwa kocha wake, AVB aliyefurushwa majuzi baada ya kipigo cha mabao 5-0 toka kwa Liverpool.
Adebayor alifunga bao hilo dakika ya 67, lakini mabao ya dakika za jioni kupitia kwa Jarvis na Maiga yaliyotosha kuivusha West Ham United kwenda kuwakabili Manchester City hatua ya Nusu fainali.
Katika mechi nyingine iliyochezwa pia jana usiku, Manchester United ilimpa nafuu kocha wake, David Moyes baada ya kuinyuka Stoke City ugenini kwa mabao 2-0 na kutinga nusu fainali kuwakabili Sundeland.
Mabao ya Ashley Young dakika ya 61 na Patrice Evra dakika ya 78 yalitosha kuwafanya mashabiki wa Mashetani Wekundu angalau kupumua kwa kuwa na hakika ya kunyakua pengine taji hilo kama wataenda vyema baada ya kuonekana kuchechemea kwenye Ligi Kuu msimu huu bila Sir Alex Ferguson.