STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 18, 2014

ROBO FAINALI YA FA HAIMTISHI KOCHA EVERTON

DROO ya mechi za Robo fainali ya michuano ya Kombe la FA Englabnd imetoka na kuonyesha timu gani itakutana na nani katika hatua hiyo baada ya kufuzu mwishoni mwa wiki.
Arsenal walioing'oa Liverpool wenyewe wataanzia nyumbani dhidi ya Everton iliyoitambia Swansea City kwa kuilaza mabao 3-1.
Hata hivyo kocha wa timu hiyo ya  Everton, Roberto Martinez amesisitiza kuwa hawana cha kuogopa watakaposafiri kwenda Emirates kuivaa Arsenal .
Martinez alisema: "Wakati wa upangaji wa ratiba mara zote unatumai kuangukia nyumbani, lakini hilo halijalishi – kama unahitaji kutwaa kombe siku zote lazima ujiandae kukutana na yeyote. Tutahitaji kuwa katika kiwango chetu bora lakini ni kitu ambacho tunahitaji kukitazama."
Kutinga katika hatua hiyo ni hatua nzuri kwa kocha Arsene Wenger ambaye kwa muda mrefu hajashuhudia klabu yake ikinyakua taji lolote ambapo kesho itakuwa vitani barani Ulaya kuumana na watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kuona kama inaweza kunyakua matji matatu kwa mpigo.
Arsenal ipo katika nafasi nzuri ya ubingwa wa Ligi Kuu ya England ikiongoza kwa sasa mbele ya Chelsea, Manchester City na Liverpool.
Mbali na mechi ya Toffee's na Gunners, pia robo fainali ya FA inaonyesha Brighton & Hove Albion itaumana ama Hull City v Sunderland, Sheffield United v Sheffield Wednesday au Charlton Athletic na  Manchester City dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo Wigan Athletic.

Saleh Tendega: Kipa wa Mgambo JKT aliyewanyamazisha Simba Mkwakwani




LICHA ya sifa nyingi kuelekezwa kwa mshambuliaji Fully Maganga aliyefunga bao pekee lililoizima Simba katika Uwanja wa Mkwakwani, lakini yupo mtu mmoja aliyefanya kazi kubwa kuinyong'onesha Simba jijini Tanga.
Saleh Tendega, katika nafasi yake ya ukipa ndiye aliyeng'ara katika pambano hilo na aliyekuwa 'mwiba' mkali kwa washambuliaji nyota wa Simba kuanzia kinara wa mabao, Amisi Tambwe, Haruna Chanongo, Ali Badru hadi kwa Ramadhani Singano 'Messi'.
Kipa huyo wa Mgambo JKT, katika mechi hiyo alikuwa na kazi moja tu kuhakikisha lango lake hazitikiswi nyavu kama walivyofumaniwa katika mechi ya awali jijini Dar es Salaam mwaka jana walipocharazwa mabao 6-0.
Ingawa katika mechi hiyo ya awali yeye hakukaa langoni, lakini kipigo ilichopewa timu yake bado alikuwa akikikumbuka na hivyo kucheza 'jihad' na kuwakatisha tamaa vijana wa Zdravko Logarusic na hatimaye kulipa kisasi.
Tendega, aliyewahi kuichezea Simba Kids wakati ikinolewa na kocha Mwinyimadi Tambaza, aliyemtoa nafasi ya ushambuliaji hadi katika ukipa, anasema anajisikia faraja kuisaidia timu yake kuizima Simba Mkwakwani.
"Nimejisikia furaha kwa sababu tumeweza kuchukua pointi tatu tulizokuwa tukizipigania ili kutusaidia katika safari yetu ya kuepuka kushuka daraja," anasema.
Nyota huyo anasema pamoja na kuwatungua Simba, lakini anakiri timu hiyo ni nzuri na yenye wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa kisoka na kuitabiria wanaweza kumaliza katika nafasi nzuri kama watakomaa kwa mechi zao zilizosalia.
"Simba ni timu nzuri na yenye watu wa mpira, sema hawakuwa na bahati kwetu na wana nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa, wasikate tamaa kwa kipigo tulichowapa," anasema Tendega anayeishabikia Manchester United.
Tendega akijiandaa kwenda mazoezini
FURAHA
Tendega aliyewahi kuzichezea timu kadhaa ikiwamo Ashanti United, anasema hakuna tukio la furaha kwake kama kufanikiwa kulamba ajira jeshini mbali na mambo mengine aliyovuna katika soka.
"Kupata ajira jeshini kwa sababu ya soka ni jambo la furaha kwangu, na kwa huzuni nalizwa sana na vifo vya wazazi wangu, kila uchao nawaombea kwa Allah awarehemu," anasema.
Kipa huyo anayependa kula ugali kwa samaki, nyama za kuchoma au za kukaanga anasema soka pia limemwezesha kupata elimu yake ya sekondari kabla ya kumpa ajira anayodai inampa faraja na furaha kubwa maishani.
Anasema pamoja na mafanikio makubwa aliyopata katika soka bado hajaridhika na badala yake atazidi kuongeza bidii ili afike mbali zaidi.
Kuhusu soka la Tanzania, Tendega anasema lipo vema isipokuwa anataka juhudi zaidi ziongezwe kuanzia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hadi kwa serikali kujitolea kuwekeza katika soka la vijana alilodai ndiyo mtaji mkuu.
"Lazima kuwapo kwa juhudi na kusaidia kujengwa kwa vituo vya soka kwa vijana na kila klabu kuwa na 'akademi' ya vijana, kama wafanyavyo Ujerumani na hata Uganda ambao leo wametuacha mbali kisoka," anasema Tendega.
Anasema pia kungejengwa shule maalum za kukuzia vipaji vya michezo ikiwamo soka ili kuzalisha nyota wa baadaye watakaolisaidia taifa kutokana na ukweli kwamba imebainika Tanzania ina vipaji, lakini hawana misingi mizuri.
Pia anasema ni vema viongozi wa kandanda nchini wakaondoa ubinafsi na kujali maendeleo ya mchezo huo ili Tanzania ifike mbali katika michuano ya kimataifa badala ya kuwa wasindikizaji kwa miaka mingi na kufarijiana tu.
Kipa huyo anayedai hakuna mshambuliaji yeyote anayemnyima raha dimbani, anaishukuru familia yake inavyomsapoti mpaka sasa, kocha aliyemjengea msingi wake kisoka, Mwinyimadi Tambaza, Joseph Kanakamfumu aliyemnoa akiwa Sekondari ya Makongo na wote waliomfundisha au kumsaidia kufika alipo sasa.
Tendega akiwa katika pozi
ALIPOTOKA
Saleh Ibrahim Tendega, alizaliwa Agosti 24, 1989 jijini Dar es Salaam. Shule ya Mtendeni alipoanza kuonyesha umahiri wake dimbani akiwa darasa la tatu akicheza kama mshambuliaji na timu ya chandimu ikiwa ni Kajima Rangers.
Baadaye alienda kujiunga na Simba Kids chini ya kocha Tambaza aliyemtoa mbele na kumrudisha golini, baadaye alihamia Yetu Afrika ya Vingunguti na kushiriki nao ligi mbalimbali wilayani Ilala kabla Villa Squad kumnyakua.
Villa ilimnyakua kabla ya kwenda Makongo Sekondari alipozidi kuimarika katika soka na baadaye kunyakuliwa na Ashanti United kisha kutua Ruvu Shooting, JKT Ruvu na baadaye Mgambo JKT alionao mpaka sasa.
Juu ya mechi ngumu anayoikumbuka, Tendega anautaja mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu 2007 kati ya timu aliyokuwa akiidakia ya Ashanti United dhidi ya Yanga, ambapo Ashanti waliiduwaza Yanga kwa kuwalaza bao 1-0.
"Naikumbuka siyo kwa ushindi tuliopata, ila kwa vile ilikuwa mechi yangu ya kwanza kubwa, pia kipindi hicho nilikuwa mdogo mno, lakini nilionyesha uwezo wa hali ya juu na kuizuia Yanga iliyokuwa ikitisha enzi hizo," anasema.
Anasema juhudi zake zilizowashangaza mpaka viongozi wake katika mchezo huo, alipochaguliwa kuwa nyota wa mchezo (man of the match) kitu kilichompa faraja na kumuongezea morali ya kujituma zaidi.
Tendega ambaye hajaoa wala kuwa na mtoto, anawaasa wachezaji wenzake kujituma, kuzingatia nidhamu na kumtegemea Mungu kwa kila jambo sambamba na kuwa na kiu ya maendeleo ili wafike mbali na mahali walipo sasa.
Kipa huyo anayependa kutumia muda wake wa ziada kuangalia muvi na kulala kumpumzisha mwili wake, anasema pamoja na Mgambo kuwa katika hatari ya kushuka daraja, lakini wachezaji wamepanga kuipigania ili kucheza Ligi Kuu mssimu ujao.

16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya haponi mtu!

* Man City vs Barca, kesho Arsenal v Bayern Munich
Manchester City watakaoikuwa nyumbani

'Mnyama' Lionel Messi atafanya nini Etihad kuisaidia Barca?

Tegemeo la Arsenal Mesut Ozil kesho ataibeba vipi the Gunners

VITA tupu Ulaya leo na kesho! Ndivyo unavyoweza kusema wakati  hatua ya mtoano ya 16 Bora inapoanza leo na kuendelea kesho kwenye Ligi yua Mabingwa Ulaya.
Vinara wa mabao wa England, Manchester City watakabiliwa na wakati mgumu watakapovaana na miamba ya daraja la juu barani Ulaya, Barcelona kwenye dimba lake la nyumbani la Etihad.
Mechi hiyo ya kukata na shoka inaelezwa kuwa ya kihistoria kutokana na timu zote kushinda kwa kishindo michezo yao ya mwisho Jumamosi, ambako City ilirejea katika kiwango chake cha juu na kuifunga Chelsea 2-0 kwenye Kombe la FA wakati Barcelona yenyewe ikiisambaratisha Rayo Vallecano  kwa mabao 6-0 kwenye La Liga.
Timu zote pia zimeongezewa nguvu baada ya wachezaji wao majeruhi kurejea. Samir Nasri amerudi kikosini katika kipindi cha pili akitokea benchi baada ya kukosa mechi saba na kufunga bao moja katika ushindi wa 2-0 waliopita dhidi ya Chelsea.
Kwa upande wa Barca, Neymar naye aliingia akitokea benchi na kisha kufunga ukurasa wa mabao kwa miamba hiyo ya Nou Camp wakati ikiibuka na ushindi wa 6-0.
Neymar anatarajiwa kuanzia benchi leo jambo ambalo litatoa ahueni kwa City, ambayo itapandisha juu kiwango chao cha soka kama itawatoa mabingwa hao mara nne wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kocha wa City, Manuel Pellegrini yupo makini na anatambua ubora wa Barca kutokana na kipindi chake akiinoa Villarreal, Malaga na Real Madrid huko Hispania, pia kiungo wa City, Yaya Toure kipindi chake cha miaka mitatu alichocheza Nou Camp na kushinda kila kombe kubwa, ikiwa ni pamoja la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2009 anaifahamu ndani nje.
Katika mahojiano na Jarida la Champions, Toure alisema ninatarajia City itashinda mechi yake ya kwanza ya mtoano ili kuonyesha ni kwa kiasi gani klabu imepiga hatua tangu Sheikh Mansour aanze kuwekeza fedha akitaka kuibadilisha kutoka uwezo wa michuano ya ndani kwenda Ligi ya Mabingwa Ulaya.
"Mashabiki wetu wanastahili ushindi dhidi ya klabu kubwa ili kuonyesha ni kwa kiasi gani klabu inaendelea," alisema. "Barcelona ni mfano sahihi, ni klabu kubwa yenye historia ya kipekee ambayo kwa sasa ina wachezaji bora duniani kama Lionel Messi, Iniesta, Xavi, Pique, Busquets.
"Itakuwa mechi kubwa na ni wazi tunatamani kuonyesha City ipo katika njia sahihi."
City haina jina katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwani imetolewa mara mbili katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika awamui mbili ilizoshiriki hivi karibuni.
Lakini msimu huu ndiyo timu inayoongoza kwa kupachika mabao kwenye michuano hiyo baada ya kufumania nyavu mara 28.
"Uzoefu wetu tulioupata kutokana na kipigo msimu uliopita umetufanya kupevuka zaidi mwaka huu," Toure aliongeza.
"Tunao wachezaji, kocha, lakini pia unapaswa kucheza na timu kubwa ili kujaribu kiwango cha uwezo wako."
City iliishangaza Bayern Munich kwa kuichapa mabao 3-2 ugenini katika hatua za makundi na imefunga jumla ya mabao 117 katika mashindano yote msimu huu.
Lionel Messi, ambaye amerejea uwanjani Januari mwaka huu baada ya kuwa majeruhi kwa miezi miwili, alifunga mabao mawili na kumpiku Alfredo di Stefano katika historia ya ufungaji La Liga.
Messi amefumania nyavu mara  228 katika mechi 263 alizocheza ambazo zinamfanya kujiunga nafasi ya tatu sambamba na Raul, wakiwa nyuma ya Telmo Zarra (251) na Hugo Sanchez (234).
Messi hadi sasa ameifungia Barcelona jumla ya mabao 337 katika michuano yote, hivyo kuweka rekodi katika klabu hiyo, lakini amefanikiwa kufunga bao moja tu nchini England wakati wa mechi ya fainali kati ya Barcelona na Manchester United iliyopigwa Uwanja wa Wembley 2011.
Licha ya Messi kuwa katika kiwango cha juu Jumamosi, pia  kiungo Cesc Fabregas na Andres Iniesta walicheza vizuri huku Pedro na Alexis nao wakifunga wakati Barca akichanua dhidi ya Rayo katika Uwanja wa Nou Camp.
"Ushindi utatusaidia kujiamini katika mechi inayofuata, ambayo itakuwa ngumu sana,"  Pedro alisema.
"Tumekuwa katika kiwango bora msimu huu, lakini leo ni kimoja kati ya bora," aliongeza nyota huyo wa Kimataifa wa Hispania.
"Mechi ya Jumanne (leo) dhidi ya City itakuwa ya karibu kuipigania, wote tu timu bora."
Mbali na mechi hiyo, leo pia
Bayer Leverkusen itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Paris St Germain  ambayo itakuwa ikimtegemea mkali wao Zlatan Ibrahimovic huku kesho Arsenal ikiialika Bayern Munich Emirates na AC Milan ikiwa mwenyeji wa Atletico Madrid.