 |
| Kemmy katika pozi |
MSANII wa zamani wa kundi la Kaole Sanaa, Juliet Samson 'Kemmy', amesema kazi yake mpya anayotarajia kuiingiza sokoni ya 'Nguvu ya Imani' ni mwanzo wa kurudi kwenye 'gemu' baada ya mashabiki wake kumkosa kwa muda mrefu.
Alisema amevunja ukimya kwa kupakua filamu hiyo aliyowashirikisha wasanii kadhaa wanaotamba nchini ili kuthibitisha kuwa bado wamo, tofauti na watu wanavyodhani kuwa enzi zake zimeisha.
"Hizi ni salamu na mvua za rasharasha tu, kuna makubwa yanakuja ndani ya 2013 baada ya 'Nguvu ya Imani'," alisema Kemmy.
Kemmy ambaye ni mtunzi, muandaaji na muongozaji kwa sasa, alisema zipo kazi nyingine zilizokaa tayari kuachiwa mara zitakapokamilika, lakini amefungua pazia na filamu hiyo ambayo hivi karibuni itakuwa mtaani.
Filamu hiyo inayohusu simulizi la wanawake wa jamii ya wafugaji na aina ya misukosuko wanayokumbana katika maisha yao ya kila siku ameiigiza yeye (Kemmy), Simon Mwapangata maarufu kama 'Rado', Jackson Kabigili na wengine.

GERARD Pique alikosa furaha kutokana na kufungwa na AC Milan, lakini alikataa kujadili kiwango cha refa licha ya kosa kubwa alilofanya mwamuzi lililoizawadia Milan goli la kuongoza.
Pique alisema: "Refa anaweza kufanya makosa wakati mwingine lakini hakuna visingizio. Si refa, si uwanja, si chochote".
Beki huyo wa kati wa Barcelona alikiri kwamba "ni matokeo mabaya sana. Walipofunga goli la kwanza tukapoteza umakini. Ni lazima tuongeze ubora, tujifunze na kusubiri mechi ya marudiano Camp Nou kwa ajili ya kufuzu. Pengine sisi si wazuri kama kila mtu anavyosema".
Pique hakutaka kutoa visingizio baada ya kiwango kibovu cha timu yake na akasema: "Uwanja wa San Siro ni mgumu kuchezana tunajua kwamba Milan ni klabu kubwa. Sisi ni Barcelona na ni lazima tubadili matokeo haya".
Walioizamisha Barcelona kwenye Uwanja wa San Siro walikuwa ni Waghana watupu. Kevin Prince-Boateng na Sulley Muntari walifunga magoli magoli mawili katika ushindi wa 2-0 juzi usiku. Hiyo ilikuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, kwa wachezaji wawili kutoka nchi hiyo kufunga katika mechi moja.