STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 18, 2012

Fella asita kutoa albamu ‘Kusonona’



ALBAMU mpya ya miondoko ya 'Rusha Roho' ya Meneja wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella iitwayo 'Kusonona Kusonona' haijasambazwa hadi sasa kutokana na kile ambachom mwenyewe amedai kuwa ni kuangalia kwa umakini kama ni muafaka kuitoa sasa ama la.
Akizungumza na MICHARAZO, Fella, alisema albamu hiyo yenye nyimbo sita iliyokuwa isambazwe mwishoni mwa mwaka jana, mpaka sasa haijatoka kwa sabahu hiyo ya kupima 'upepo'.
Fella alisema wakati akijiandaa kuitoa kazi hiyo mtaani, kulikuwa na kazi nyingine lukuki na hivyo kukubali kwamba atulie kwanza ili kuangalia mwenendo wa albamu zilizotangulia na kwamba huenda akaitoa mwisho wa mwezi huu.
"Ile albamu yangu ya 'Kusonona Kusonona' ya miondoko ya taarab, bado sijaiachia hadi sasa kutokana na hali ilivyokuwa sokoni, lakini kwa sasa nipo mbioni kufanya hivyo" alisema Fella.
Aliongeza, licha ya kwamba albamu bado haijaingia sokoni, lakini baadhi ya nyimbo zake zimekuwa zikifanya vema kwenye vituo vya redio na runinga baada ya kusambaza kwa nia ya kuitambulisha albamu hiyo kikiwemo 'Midomo Imewashuka'.
Ndani ya albamu hiyo, Fella amewashirikisha nyota kadhaa wa taarab wakiwemo Khadija Kopa wa TOT, Isha Ramadhani wa Mashauzi Classic na Maua Tego wa kundi la Coast Modern.
Fella alizitaja nyimbo zilizopo ndani ya albamu hiyo kuwa ni 'Simuachi', 'Midomo Imewashuka', 'Mchakamchaka', 'Sijapopoa Dodo', 'Kimodern Modern' na 'Kusonona Kusonona' iliyobeba jina la albamu.

No comments:

Post a Comment