STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 18, 2012

Juma Mgunda ala shavu Coastal, wawili watimuliwa



WAKATI nyota wa zamani wa kimataifa nchini, Juma Mgunda akila 'shavu' kwa kuteuliwa kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Coastal Union ya Tanga, wachezaji wawili wa timu hiyo wamefukuzwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Wachezaji waliotimuliwa Coastal kutokana na kushindwa kuripoti kwenye kambi ya timu hiyo inayojiandaa na mechi za duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara ni Daniel Busungu na Soud Abdallah aliyewahi kuichezea pia Simba msimu kadhaa ya nyuma.
Afisa Habari wa Coastal, Eddo Kumwembe, aliiambia MICHARAZO jana kuwa, Soud na Busungu wamechukuliwa hatua hiyo kutokana na kuonyesha dharau kwa uongozi wao ambao umekuwa ukiwabembeleza kujiunga na kambi ya mazoezi.
Kumwembe alisema kwa mfano Busungu licha ya kutumiwa nauli kwa ajili ya kwenda kambini hadi sasa hajaripoti wala kutoa maelezo jambo linaloonyesha hana nia ya kuichezea timu yao na ndio maana wamemtimua.
"Kwa kuwa tuna nia ya kuona timu yetu inafanya vema tumewatimua wachezaji hao kwa utovu wa nidhamu, kwani wameonyesha hawana nia ya kuichezea Coastal kwa vile fedha za nauli tumewatimua na bado wanatudengulia," alisema Kumwembe.
Aliongeza katika kuhakikisha wanafanya vema kwenye duru lijalo la ligi kuu linaloanza Jumamosi, timu yao imempa ulaji, mshambuliaji nyota wa zamani wa timu hiyo na Taifa Stars, Juma Mgunda kuwa Kaimu Kocha Mkuu.
Kumwembe alisema Mgunda, amechukuliwa kushika nafasi ya Jamhuri Kihwelu 'Julio' ambaye yupo Oman kwa mambo yake binafsi na atakapokuja ataendelea na cheo chake huku Mgunda atakuwa msaidizi wake katika benchi lao la ufundi.
"Timu kwa sasa ipo chini ya Juma Mgunda akisaidiana na Ally Jangalu, ingawa bado Julio tunamtambua kama kocha wetu hadi atakaporudi baada ya kumaliza mambo yake huko Arabuni," alisema Kumwembe.
Kumwembe, alisema kikosi chao kwa ujumla kipo vema tayari kwa mikikimikiki ya duru la pili, ambapo wao wataanza kwa kuvaana na Simba Jumatano ijayo, jijini Dar.

Mwisho

No comments:

Post a Comment