STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 18, 2012

Snake Boy Jr ataka mabondia wapimwe VVU



BONDIA machachari nchini wa ngumi za kulipwa, Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr', ametaka iwe ni lazima kwa mabondia wapimwe VVU kabla ya kupanda ulingoni kwa nia ya kuepusha maambukizi kwa wapiganaji.
Mtoto huyo wa bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla 'Snake Man' alisema kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa katika upimaji afya kwa mabondia kabla ya kupigana hali inayohatarisha usalama wa afya zao ulingoni.
Matumla, alisema ni lazima mabondia wawe wanapimwa afya zao na hasa VVU( Virusi vya Ukimwi), ili kuwaweka salama mabondia wawapo ulingoni ambapo hutokea wakapeana majeraha mauongoni yanayoweza kusababisha maambukizi kati yao.
"Nadhani ipo haja ya kufanyika kwa lazima upimaji wa VVU kama tunataka kuwaweka salama mabondia wetu, mara nyingi tumekuwa tukipanda ulingoni bila kupimwa afya zaidi ya uzito au kupimwa mapigo ya moyo tu, hili ni jambo la hatari," alisema.
Alisema kupitia baba yake amewahi kusikia kwamba kwa mabondia wa nchi za Ulaya wamekuwa makini katika suala la upimaji afya za mabondia kabla ya kupigana kwa lengo la kuwaweka salama na kuwapusha matatizo tofauti na ilivyo nchini.
Bondia huyo 'asiyepigika' tanu aingie kwenye ngumi za kulipwa mwaka juzi, alisema vyama na mabondia wanapaswa kusimamia jambo hilo kwa umakini mkubwa kwa vile inaweza kuleta athari kubwa baadae bila watu kujua tatizo limeanzia wapi.
Aliongeza, hata taarifa kwamba mabondia fulani wamepimwa na kugundulika wapo fiti ni propaganda tu, ukweli huwa hakuna kinachofanyika, japo alikiri suala la upimaji afya ni jambo binafsi la mtu, ila kwa mabondia kama yeye iwe lazima kwa usalama wao.
Kauli ya bondia huyo chipukizi inakaribiana na ile iliyowahi kutolewa na aliyekuwa Bingwa wa Dunia wa WBF, Karama Nyilawila aliyewahi kuvitaka vyama kusimamia suala la upimaji VVU kwa mabondia kabla ya kupanda ulingoni kupigana.

Mwisho

No comments:

Post a Comment