MABONDIA wakongwe wa ngumi za kulipwa nchini, Rashid Matumla 'Snake Man' na Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo' wanatarajiwa kusindikizwa na mabondia 10 tofauti katika pambano lao litakalofanyika mwezi ujao kwenye ukumbi wa PTA, jijini.
Oswald na Matumla watapigana katika pambano lisilo la ubingwa la uzani wa Super Middle, litakalofanyika Februari 25 kwa nia ya kumaliza ubishi baina yao.
Wawili hao walipigana Desemba 25 mwaka uliopita, na kutoka droo ya pointi 99-99 ambapo kila mmoja alinukuliwa kutokubaliana na matokeo hato akisema alistahili kutangazwa mshindi katika mchezo huo uliochezwa katika ukumbi wa Heinken Pub.
Mratibu wa pambano hilo, Issa Malanga, amesema kabla ya mabondia hao wakongwe kupanda ulingoni kutakuwa na michezo kadhaa ya utangulizi ambayo itahusisha mabondia chipukizi na wale wazoefu.
Malanga, alisema baadhi ya mabondia watakaowasindikiza akina Matumla ni Shomari
Mirundi atakayepigana na Mikidadi Abdallah 'Tyson' na Idd Mkenye dhidi ya Shabaan Mtengela 'Zunga Boy'.
Michezo mingine ya utangulizi itawakutanisha, Abdallah Mohamedi dhidi ya Saleh Mkalekwa na Ramadhani Mashudu ataonyeshana kazi na Hassan Kiwale 'Moro Best'.
Malanga alisema anafanya mipango mapambano hayo yapambwe na burudani ya muziki wa kizazi kipya toka kundi la TMK Wanaume Family, ingawa alisema kwa sasa ni mapema mno kwa vile bado hajafanya mazungumzo na wasanii wa kundi hilo.
Matumla na Maneno tayari walishapigana mara nne, mara mbili Matumla akiibuka na ushindi na moja Maneno kutoka kidedea na la mwisho ndilo lililoisha kwa sare inayolalamikiwa na wote wawili.
Mwisho
No comments:
Post a Comment