STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 18, 2012

Mkubwa na Wanae: Kituo cha kuendeleza vipaji







WAKATI kituo cha kuendeleza vipaji vya sanaa kwa vijana cha 'Mkubwa na Wanawe'
kinachomilikiwa na Meneja wa TMK Wanaume Family, Said Fella kilipoanzishwa mwaka jana kilikuwa na msanii mmoja tu, Abdallah Kihambwe 'Dula Yeyo'.
Hata hivyo kikielekea kutimiza muda wa mwaka mmoja mnamo Februari 13, mwaka huu, kituo hicho kina jumla ya wasanii 37, wasichana 10 na waliosalia ni wavulana ambao wote wanaimba na kudansi.
Fella, maarufu kama 'Mkubwa Fella' ambaye ndiye Mkurugenzi wa kituo hicho alisema
alipata wazo la kuanzisha kituo hicho kilichosajiliwa kama kampuni, kutokana na kuvutiwa na mafanikio inayopata kituo kingine cha kuendeleza vipaji cha THT.
Alisema, pia alikianzishwa kwa nia ya kusaidia vijana wadogo kujiepusha kuingia kwenye makundi maovu yatakayoweza kuwapotosha na kufunza stadi za maisha kwa faida yao ya baadae mbali na kuvitumia vipaji vyao vya sanaa kama ajira rasmi.
Fella, alisema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho ambayo anashirikiana kukiendesha na
wakurugenzi wenzake, Hamis Tale 'Babu Tale' na Mheshimiwa Temba, kimeweza kuwatoa wasanii karibu saba ambao wameanza kutamba kwenye fani ya muziki nchini.
"Tunashukuru tangu kuanzishwa kwa kituo hiki, tumefanikiwa kuwatoa wasanii kadhaa ambao wameanza kupata mafanikio katika muziki, licha ya kwamba tunakabiliwa na matatizo makubwa katika kituo chtu kwa vile hakina wafadhili wala wadhamini," alisema.
Aliwataja wasanii wanaokitangaza kituo hicho kwa sasa ni Aslay Isihaka 'Dogo Aslay'
anayetamba na wimbo wa 'Nakusemea' maarufu kama 'Naenda Kusema kwa Mama', Dula Yeyo, Mugogo anayekimbiza na wimbo wa 'Chongochongo' na Hassani Kumbi anayetamba na kibao cha 'Vocha' kilichopo katika mahadhi ya Mduara.
"Wengine ambao tumeanza kuwarekodia kutokana na kuiva kimuziki ni, H. Namba, Bashlee na Asnat wanaotarajia kuibuka na kibao kiitwacho 'Nipe Kidogo', kwa vifupi ni kwamba matunda yameanza kuonekana katika kuwaibua wasanii wapya," alisema.
Fella alisema licha ya kuwafunza namna ya kuimba na kucheza, wasanii waliopo kituo
hapo wanafundishwa stadi za maisha juu ya mapenzi na athari zake, matumizi ya dawa za kulevya na magonjwa mbalimbali kama Ukimwi na mengine na jinsi ya kuepukana nayo.
"Kwa upande wa muziki mwalimu wanayewanoa vijana hao ni Mhe Temba na Dulla Yeyo, wakati Meneja wa kituo ni Yusuf Chambuso na Prodyuza wa kituo ni Suleiman Daud maarufu kama Sulesh au Mr India," alisema Fella.
Juu ya namna ya kukihudumia kituo, Fella alisema wanatumia fedha zao wenyewe wakati wakisubiri kupata ufadhili, ambapo alisema kwa mwezi mzima hutumia si chini ya Sh. Mil moja kwa ajili ya malazi ya chakula.
"Unajua nyumba hii inayowatunzia wasanii ni ya kukodisha, tunalipa pango kwa mwezi
Sh. 250,000, huku huduma ya chakula kwa siku si chini ya Sh 25,000, hiyo ni mbali na
gharama za usafiri na ada kwa wanafunzi tunawaosemesha wenyewe," alisema.
Alisema licha ya wengi wa wasanii wao kutokea majumbani kwao kuja kujifunza fani zao kituo hapo, wapo wasanii 12 wanaoishi katika nyumba hiyo iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam.
Fella alisema matarajio yao hadi kufikia mwisho wa mwa huu wasanii zaidi ya 20 wawe
wameshatoka kisanii, na kuwasaidia vijana zaidi ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo alisema mafanikio hayo yatafikiwa pale atakapopata wafadhili na kuungwa
mkono na serikali katika jitihada zake za kuendeleza sanaa na kuwasaidia vijana kupata ajira kupitia muziki, sambamba na kuwajenga kimaadili.
Fella alisema kituo kwao kitu cha kwanza wanachozingatia ni nidhamu na kuwanyoosha wale wanaoonekana kwenda kinyume, pia wanathamini kipaji cha mtu bila kujali umri wake na bahati nzuri matunda yao yanaonekana kupitia wasanii walioanza kutamba sasa.
Naye Meneja wa kituo hicho, Yusuf Chambuso, alisema kuna vikwazo kadhaa wamewahi kukutana navyo kama baadhi ya wazazi kushindwa kuwaelewa katika wanachokusudia kwa kudhani watoto wao wanafunzwa uhuni, lakini wanapoeleweshwa huwapa sapoti.
Aliongeza wapo baadhi ya vijana wanaoenda kwao huwa hawana uwezo wowote kimuziki, lakini kupitia walimu wao huwasaidia na kuwaweka juu, akimtolea Aslay aliyedai licha ya kugundua kipaji cha muziki, walimsaidia kumweka sawa ndio maana leo anatisha.

Mwisho

No comments:

Post a Comment