KLABU ya soka ya Moro United imesema ipo kwenye mahesabu makali ili kuhakikisha inaibuka na ushindi katika pambano lao la fungua dimba la duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga watakaumana nao Jumamosi ijayo.
Yanga na Moro United zinatarajiwa kushuka dimba la Taifa, Dar es Salaam kuumana katika mechi ya kufungua pazia la duru la pili, ambapo pia siku hiyo kutakuwa na mechi nyingine tatu katika viwanja tofauti nchini.
Katibu Mkuu wa Moro United, Hamza Abdallah, alisema kuwa akili zao zipo kwenye pambano hilo kwa lengo la kupata ushindi katika mchezo huo wa kufungua dimba ili kuanza vema na pia kujiweka katika mazingira mazuri.
Abdallah, alisema wanatambua kuwa pambano hilo litakuwa gumu kutokana na jinsi timu hizo mbili zinapokutana uwanjani mechi yao huwa na upinzani, lakini kubwa kwao ni kuona wanashinda baada ya pambano lao la awali kuisha kwa sare ya 1-1.
"Tunajipanga kuhakikisha tunapata ushindi katika mechi hiyo ya ufunguzi wa duru la pili, tunaamini kikosi tulichonacho ambacho kimeongezewa nguvu na wachezaji wapya na walimu katika benchi la ufundi, kitaisimamisha Yanga Jumamosi," alisema.
Katibu huyo alisema licha ya kwamba imewapoteza wachezaji nyota watatu, Omega Seme na Salum Telela waliorejea Yanga na Gaudence Mwaikimba kuhamia Azam, bado kikosi chao kitafanya vema baada ya kuwanasa wakali wengine kadhaa.
Baadhi ya wachezaji inayojivunia MoroUtd katika kikosi chao cha sasa ni pamoja na Jamal Mnyate toka Azam, Fred Mbuna aliyetoka Yanga, Salum Kanoni na Meshack Abel wote kutoka Simba waliosajiliwa kwenye dirisha dogo lililofungwa hivi karibuni.
Timu hiyo kwa sasa imejichimbia kambini eneo la Tabata, jijini Dar es Salaam tayari kwa ajili ya pambano hilo dhidi ya Yanga.
Mwisho
No comments:
Post a Comment