Juma Kaseja |
Hussein Sharrif 'Casillas' |
KUKWAMA kwa kipa Hussein Sharrif 'Casillas' kujiunga na Fc Lupopo baada ya klabu yake ya Mtibwa kushindwa kuafikiana dau na timu hiyo ya DR Congo kumemfanya 'Tanzania One', Juma Kaseja kushindwa kutua Manungu kuichezea timu hiyo kwa msimu ujao wa Ligi Kuu.
Kaseja aliyetemwa na Simba baada ya kuitumikia miaka karibu 10, alikuwa akitajwa kuwa mbioni kusajili wa Mtibwa, lakini Mkurugenzi wa klabu hiyo, Jamal Bayser aliiambia MICHARAZO muda mchache uliopita kuwa, mpango huo umekufa baada ya Casillas kukwama kutua Lupopo.
Casillas alifuzu majaribio katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya DR Congo na alikuwa katika maandalizi ya kuondoka kwenda kujiunga na timu hiyo wakati klabu hizo mbili zikifanya mazungumzo ya mwisho kuhusu dau la uhamisho wake.
Hata hivyo Bayser alisema kuwa mazungumzo hayo ya Casillas kuhamia Lupopo yamekwama baada ya Wakongo kushindwa kuafiki dau walilokuwa wakilitaka na hivyo kipa huyo atasalia Mtibwa kwa msimu ujao na kwa maana hiyo hawana mpango na kipa mpya.
Bayser alisema walikuwa na dhamira ya kumnyakua Kaseja iwapo mazungumzo baina yao na Lupopo yangeenda vyema kwa Casillas kuondoka, lakini kw ahali ilivyo wamesitisha mipango ya kumsajili Kaseja ambaye alimtaja kama kipa bora ambaye kila timu inatamani iwe naye.
"Mazungumzo yetu na Fc Lupopo juu ya kuwapa Casillas yamekwama na hivyo kipa huyo atasalia Mtibwa na kwa maana hiyo hatuna haja ya kumuongeza kipa yeyote mpya kama ambavyo tulikuwa tumepanga tukimfikiria Kaseja," alisema Bayser.
Bayser aliongeza pia klabu yao haina mpango wowote wa kusajili mchezaji kutoka nje ya nchi na badala yake wataendelea kuwaamini vijana wazawa kama walivyofanya msimu uliopita na kumaliza ligi wakiwa katika nafasi ya tano.
Kwa wiki moja sasa kulikuwa na tetesi kwamba huenda Kaseja aliyetemwa Simba angetua Mtibwa Sugar au Coastal Union, kabla ya Coastal kuweka bayana kuwa haina mpango naye.
No comments:
Post a Comment