STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, July 16, 2013

Hussein Javu atamani soka la kulipwa

Hussein Javu (kulia) akikabana na Aggrey Morris wa Azam katika moja ya mechi za igi Kuu

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Mtibwa Sugar, Hussein Javu amesema anatamani kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchini bila kujali kama ni Afrika au barani Ulaya, ili kutimiza ndoto zake za tangu utotoni.
Javu, aliye katika kikosi cha pili cha taifa 'Young Taifa Stars' alisema ipo mipango anaiweka sawa ili kutimiza ndoto hizo za kucheza soka la kulipwa akiwa tayari kutua kokote hata kama ni nchi jirani za Kenya, DR Congo au Msumbiji.
Alisema kwa sasa anamsikilizia wakala wake kuona mipango hiyo inakwendaje, ingawa alisisitiza kuwa bado ana mkataba wa kuitumikia timu yake ya Mtibwa hadi mwakani.
Mshambuliaji huyo ambaye amekuwa wakitajwa kama miongoni mwa wachezaji wapya wa Yanga, ingawa mwenyewe anakanusha kuwa hajasaini kokote zaidi na kujitambua kama mchezaji wa Mtibwa kulingana na mkataba aliokuwa nao na klabu hiyo aliyojiunga nayo tangu mwaka 2007 katika kikosi cha vijana, alisema kiu ya kucheza soka la kulipwa ni kubwa kiasi cha kutoelezeka.
"Hakuna kitu ninachokitamani na kulilia kama kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, kuna mipango inafanywa lakini siwezi kuiweka wazi kwa sasa kwa vile ni mapema, ila nitafarijika sana kama nitaenda hata Kenya tu," alisema.
Javu anayemhofia dimbani beki wa zamani wa Simba aliyehamia Coastal Union Juma Nyosso, alisema kiu yake ya kucheza nje ya nchi imeongezeka baada ya kuona mafanikio ya wachezaji wenzake wa timu ya taifa, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na watanzania wengine wanaocheza soka hilo barani Afrika katika nchi za DR Congo, Kenya, Msumbiji na Angola.
Pia aliweka bayana kwamba mbali na kiu ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, pia angependa kuichezea timu mojawapo kubwa nchini kati ya Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikimuwinda ili kumsajili.

No comments:

Post a Comment