wanachuo walipoandama baada ya tukio la kuvamiwa na kupigwa risasi kwa wenzao na majambazi waliokamtwa na jeshi l polisi |
WATU wanne wanaodaiwa kuwa majambazi wamenaswa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kuhusika na tukio la ujambazi lililotokea Juni 21, mwaka huu, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika eneo la bweni la Yombo One.
Aidha mtu mwingine anayedaiwa kumlewesha kwa dawa za kulevya kisha kumbaka kabla ya kumpora mfanyabiashara nyumbani kwake naye katiwa mbaroni na jeshi hilo baada ya kuendesha msako dhidi yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Ally Mlege, alisema watuhumiwa wanne waliohusika na tukio la Chuo Kikuu, walikamatwa na jeshi hilo Julai 8, mwaka huu, kwenye kituo cha Daladala Ubungo.
Kamanda Mlege, alisema jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata watu hao wakiwa na silaha aina ya SMG ikiwa na risasi moja, laptop mbili aina ya Toshiba, simu aina ya Samsung, panga moja na nyundo.
Alisema baada ya mahojiano, majambazi hayo yalikiri kuhusika katika tukio la unyang’anyi lililotokea UDSM.
Afande Mlege, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Dolisera Gerald (22), Leonard Mathias (21), Leonard Leopard (32), Gerald Moses (23), ambao licha ya kukiri kuhusika katika tukio hilo pia walikiri kuhusika katika matukio mbalimbali ya kihalifu sehemu tofauti jijini.
Wakati huo huo Kamanda Mlege alisema jeshi hilo limemtia mbaroni mkazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam, Ezekiel Matiti (35), kwa tuhuma za kumlewesha dawa za kulevya mkazi wa Makongo Juu, jijini humo, Aida Kiangi.
Kwa mujibu wa Mlege baada ya mtuhumiwa kumlewesha Aida, alimpeleka nyumbani kwake (Makongo Juu) na kumuingiza ndani na kumbaka na kisha kumuibia runinga, pamoja na vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh. milioni nane.
Aidha aliongeza kuwa, katika tukio lingine, polisi inawashikilia Michael Pascal (35), Donald Joseph (43), Kulwa Adamson (43), na Ally Akiri (41), na watuhumiwa wengine watano, kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la kurushiana risasi na askari polisi eneo la Kunduchi Mtongani.
No comments:
Post a Comment