STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, July 16, 2013

Walimu Shule ya Msingi King'ongo wawalia wazazi, kisa utoro wa wanafunzi



UONGOZI wa Shule ya Msingi King'ongo, iliyopo Kata ya Saranga, wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, umelia na vitendo vya utoro uliokithiri kwa wanafunzi wanaosoma shule hiyo hasa wale wa darasa la saba na kuwaomba wazazi wa wanafunzi hao kuingilia kati kuwasaidia.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Flora Salila alitoa kilio hicho katika mkutano wa pamoja kati yao na wazazi wa wanafunzi wa darasa la saba uliofanyika juzi shuleni hapo.
Mwalimu Salila, alisema uongozi wao umekuwa katika wakati mgumu kutokana na vitendo vya utoro kwa wanafunzi na hasa wa darasa la saba, ambapo kuna wakati hufikia mpaka wanafunzi 58 kati ya 268 wa darasa hilo la saba kutoonekana shuleni.
Mwalimu huyo alisema vitendo hivyo huenda vinachangiwa na wazazi kutojenga utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni na kuwapa wakati mgumu walimu ambao hujaribu kutatua tatizo hilo la utoro bila mafanikio kwa kukosa ushirikiano na wazazi.
"Lazima niwaeleze ukweli kuwa, utoro ni tatizo sugu shuleni kwetu hasa hawa wa darasa la saba kwa mfano karibu wanafunzi 58 miongoni mwa 268 wa darasa hilo hawakuwepo shuleni wakati wa upigaji wa picha za maandalizi ya mitihani, hii siyo jambo zuri, wazazi tusaidieni," alisema.
Aliongeza kwa jumla ya wanafunzi 1762 waliopo shuleni hapo kwa siku watoto kati ya 100-200 huwa hawafiki shuleni na kuhoji wazazi wenye watoto hao wanafanya nini katika kuwasaidia walimu kuwaondoa watoto katika vitendo hivyo vinavyochangia kudumaza taaluma.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa King'ongo,  Demetrius Mapesi alisema ni lazima wazazi washirikiane na walimu kutatua utoro shuleni hapo iwapio wanataka shule yao iendelee kushika nafasi ya pili katika Kata ya Saranga.
Mapesi alisema wazazi wamekuwa wakishindwa kufuatilia nyendo za watoto wao na kuishia kuwatumia lawama walimu pale watoto wao wanapofanya vibaya kwenye mitihani wakati jukumu hilo ni la lazima kwao kabla ya walimu kufuatia hasa wanapokuwa shuleni.
"Wazazi badilikeni, kutofuatilia nyendo za watoto wenu ndiyo chanzo cha kuharibika kwa vijana, dunia ya sasa imeharibika na haiaminiki, ukijifanya upe bize na kazi ujue unazalisha watoto machangudoa, vibaka na hata mashoga, mtakuja kumlaumu nani," alihoji Mapesi.

Mwisho

No comments:

Post a Comment