STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, November 9, 2013

Unyama: Auwawa kwa kukatwa na shoka shingoni


MTU mmoja aliyefahamika  kwa jina la  Ruswetura  Mahongo (40)  mkazi wa Kijiji cha Kambuzi  Halt,  Wilaya  ya Mlele, Mkoa wa Katavi ameuawa  kwa kukatwa na shoka  kichwani na shingoni  na sehemu ya bega la kulia na  watu wawili waliokuwa  wakifanya kazi ya kibarua nyumbani kwake ya kujenga uzio wa zizi la ng’ombe.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi,  Dhahiri Kidavashari,  alisema tukio hilo la mauaji ya kutisha  lilitokea  jana majira ya saa kumi na moja jioni nyumbani kwa marehemu.
Alisema siku moja kabla ya mauaji hayo  alifika mtu mmoja nyumbani kwa marehemu na kuomba kibarua cha kutengeneza zizi la ng’ombe  na ndipo alipokubaliwa na kuanza kazi ambayo hakuimaliza siku hiyo.
Kidavashari alieleza siku iliyofuata kibarua huyo alifika nyumbani kwa marehemu  akiwa na kijana mwingine mbaye alionekana kumsaidia kazi hiyo hata marehemu alielewa hivyo.
Alisema ilipofika majira ya saa kumi na moja jioni marehemu akiwa amelala kwenye jamvi pembeni ya nyumba yake  mke wake mdogo  aitwaye  Tatu  Shiranga  alimuaga marehemu kuwa anakwenda mtoni kuteka maji  na alimuacha marehemu akiwa na  vibarua hao pamoja na mtoto wake mdogo mwenye umri wa miaka saba.
Baada ya mke wake kuondoka  vibarua hao  walimfuata mahali alipokuwa amelala marehemu na kuanza kumkatakata kwa shoka  kichwani, shingoni  na kwenye bega, hali ambayo ilisababisha  mwanae huyo mdogo akimbie mbio na kujificha kichakani huku akiwa akishuhudia  wanavyomshambulia baba yake na alishindwa kuomba msaada kwa majirani kutokana  na wao kuishi mbali na majirani.

Kamanda Kidavashari alieleza mke wa  huyo wa marehemu alirejea kutoka mtoni kuteka maji ndipo alipokaribia kufika kwake mtoto wake alimkimbilia na kumweleza kuwa wale  watu wawili  waliokuwa wakifanya kazi ya kibarua  wamemkata baba yake kwa shoka  na kisha wamekimbilia porini.
Alisema mke wa marehemu alilazimika kwenda kuangalia pale  ambapo alikuwa amemuacha mumewe  amelala  na ndipo alipomkuta  akiwa amegalagala chini huku mwili wake ukiwa na majeraha makubwa na damu zikiwa zimetapakaa huku akiwa amefariki dunia.
Alifafanua kuwa uchunguzi  uliofanywa na Jeshi la Polisi  baada ya kumhoji  mke mdogo wa marehemu na ndugu zake kifo hicho kimesababishwa na sababu mbambali zilizotokana na tabia ya ukorofi  na ubabe wa marehemu  kwa majirani na ndugu zake.
Marehemu wakati akiishi katika Kijiji cha Mtowisa  Mkoa wa Rukwa hapo mwaka 2012 aliwahi  kuvamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa kwa mapanga  na kuponea chupuchupu  na nyumba yake kuchomwa moto  na ndipo baada ya hapo marehemu aliamua huhamia katika kijiji hicho  mkoani Katavi.
Kamanda Kidavashari alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa na jitihada za kuwasaka watu waliohusika katika mauaji ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria zinaendelea.
Chanzo:Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment