STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, November 9, 2013

KIUNGO WA YANGA HAROUNA NIYONZIMA NDIYE MWANASOKA BORA WA MWANASPOTI 2013

Haruna akiwajibika uwanjani

Haruna na tuzo zake tatu

KIUNGO wa Yanga SC, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima raia wa Rwanda, ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa gazeti la Mwanaspoti, akiwashinda Amri Kiemba, Shomary Kapombe wa Simba SC na Themi Felix wa Kagera Sugar. 


Katika hafla iliyofana kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wachezaji wengi, mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa (TEKNOHAMA) Januari Makamba, mchezaji Niyonzima aliondoka na tuzo tatu, nyingine ya mchezaji wa kigeni na 11 Bora wa Mwanaspti.

Haruna akipokea tuzo yake ya Mwanasoka Bora wa Kigeni kutoka kwa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA)

Katika tuzo ya mchezaji bora wa kigeni, Niyonzima aliwashinda mchezaji mwenzake wa Yanga, mshambuliaji wa Kiganda, Hamisi Friday Kiiza na mshambuliaji wa Azam kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche. Mchezaji wa Azam FC, Joseph Kimwaga aliwashinda Juma Luizio wa Mtibwa Sugar na Ramadhani Singano ‘Messi’ katika kinyang’anyiro cha tuzo ya Mchezaji Chipukizi.


Mwanahamisi Omar wa Mburahati Queens aliwashinda Shelida Boniface na Fatuma Mussa katika ya Mchezaji Bora wa kike, wakati Mbwana Samatta aliwashinda Henry Joseph aliyekuwa anacheza Kongsvinger ya Norway kabla ya kurejea Simba SC msimu huu na mshambuliaji mwenzake wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu katika tuzo ya mwanasoka anayecheza nje.
Haruna akipokea hundi ya Sh. Milioni 5 kutoka kwa Naibu Waziri wa TEKNOHAMA, Januari Makamba. Wengine kulia ni Zuhura Muro, Mwenyekiti wa Bodi wa MCL na Tido Mhando kushoto, Ofisa Mtendaji Mkuu wa MCL.


Oden Mbaga aliwashinda Martin Sanya na Ibrahim Kidiwa katika tuzo ya Refa bora, wakati Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ aliwashinda Muingereza Stewart Hall wa Azam na Mholanzi Ernie Brandts wa Yanga katika tuzo ya kocha bora.


Thomas Ulimwengu alishinda tuzo ya bao bora alilofunga katika mechi dhidi ya Ivory Coast kuwania tiketi ya Kombe la Dunia, wakati Kipre Tchetche ameshinda tuzo ya Mfungaji bora. 

Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, David Mwantika, Amri Kiemba, Thomas Ulimwengu, Haruna Niyonzima, Themi Felix, Mbwana Samatta na Kipre Tchetche wameteuliwa katika ’11 Bora’ wa Mwanaspoti.
 
Zilizotolewa pia tuzo za heshima kwa wachezaji wa zamani nchini akina Nicholas Akwitende, John Lyimo, Mbwana Abushiri, Omar Zimbwe, Jellah Mtagwa na mtangazaji wa zamani maarufu, Mshindo Mkeyenge. Mkeyenge aliyeanza kutangza tangu miaka ya 1960 Radio Tanzania (RTD) aliwahuzunisha wengi baada ya kuwasili jukwaani akiwa amebebwa kutokana na kukatwa mguu kwa sababu ya maradhi ya kupooza. 

Hadhara Charles alipewa tuzo ya kipaji maalum, wakati Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga alipewa tuzo ya Utawala Bora katika soka. 

Washindi walipewa na zawadi za fedha, Niyonzima Sh. Milioni 5, wengine Sh. Milioni 1 na wengine 500,000. Kwa ujumla tuzo hizo zilizosindikizwa na burudani ya wanamuziki Juma Nature, Joh Makini na King Kiki zilifana.


BIN ZUBEIRY 

No comments:

Post a Comment