STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 24, 2014

'Yanga funga hao Al Ahly tupumue mitaani'

http://2.bp.blogspot.com/-2AgowyAqcZA/UMWSUxAbTGI/AAAAAAAABK8/fmQ5f4m08P4/s1600/mko+2.jpg
Mkono wa Mkonole
MCHEKESHAJI Fadhil Omar 'Mkono wa Mkonole' ameiangukia timu anayoishabiki ya Yanga, kuhakikisha inafanya kweli mbele ya Waarabu ili kuweza kuzima kebehi wanazopewa na watani zao mitaani.
Mkono aliyepo mjini Morogoro kwa sasa akirekodi filamu mpya alisema yeye ni mnazi mkubwa wa Yanga na amekuwa akiifuatilia katika mechi zake za ndani na za kimataifa, lakini hana furaha kwa kebehi toka kwa watu wa Simba.
"Watani wetu wanatucheka eti, sisi kwa Waarabu ni kama 'Mbwa kwa Chatu', nilikuwa nawaomba wachezaji wa Yanga wasituangushe mbele ya Al Ahly, waifunge kukata mzizi wa fitina na kuwaziba midomo watani wetu," alisema.
Mkono alisema anaamini Yanga wakijipanga vyema kwa mechi ya awali ya ugenini kabla ya kuja kumalizana nao jijini Dar es Salaam wanaweza kurejea rekodi ya Simba ya mwaka 2003 waliivua ubingwa Zamalek.
"Yanga ikikaza msuli na kujipanga vyema wanaweza kurejea yaliyofanywa na Simba mwaka 2003, tunajisikia wanyonge kwa kejeli za watu wa Simba wakidai eti safari yetu kimataifa imefikia tamati kwa Al Ahly," alisema.
Yanga iliyokuwa Comoro inatarajiwa kuvaana na Al Ahly mwishoni mwa wiki hii baada ya kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuing'oa Komorozine kwa jumla ya mabao 12-2.
Msanii huyo alisema haoni sababu ya Yanga kushindwa kuifanyizia Al Ahly ambao pia ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo kwa madai Jangwani wana kikosi imara na kocha mzoefu, Johannes van Der Pluijm.
Pambano hilo linatarajiwa kuchezwa siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa, na Yanga inahitajika kushinda idadi kubwa ya mabao ili kurahisisha pambano lao la marudiano wiki ijayo mjini Cairo.
Al Ahly ndiyo mabingwa watetezi na pia wanashikilia taji la Super Cup iliyotwaa Alhamis iliyopita baada ya kuilaza CS Sfaxien ya Tunisia kwa mabao 3-2 huku wakishuhudiwa na kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa 'Master' aliyetumwa kwenda kufanya ushushushu.

No comments:

Post a Comment