STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 8, 2014

Chelsea kikaangoni leo, Ronaldo fit kuwakabili Dortmund

Ronaldo aliyerejea tena dimbani
Chelsea watakaokuwa na kibarua kigumu mjini London mbele ya PSG
WINGA nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo yupo fiti tayari kuwakabili Wajeruman, Borussia Dortmund katika pambano la leo la marudiano la Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, licha ya kudaiwa kulalamika kusumbuliwa na goti baada ya kuumia wakati Real Madrid ikishinda 3-0 kwenye mechi ya awali.
Wakati Real wakichekelea, Chelsea watakuwa na kazi ngumu ya kubadili matokeo ya kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya PSG, licha ya kiungo wake kutamba kuwa hilo litawezekana leo Stanford Bridge.
Kocha wa Real, Carlo Ancelotti alimpumzisha Ronaldo katika mechi ya La Liga Jumamosi ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 4-0 uliowasaidia kupunguza wigo wa pointi dhidi ya vinara Atletico Madrid na mabingwa watetezi Barcelona wanaoshika nafasi ya pili.
Nahodha huyo wa Ureno, ambaye wiki iliyopita aliweka rekodi kwa kufikisha mabao 14 msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, alikuwa alilalamika kutojisikia vizuri katika goti la mguu wa kushoto lakini Ancelotti alisema atakuwapo uwanjani katika mechi ya marudiano leo nchini Ujerumani baada ya kupata matibabu na mapumziko.
Ronaldo alifikisha mechi 100 za Ligi ya Mabingwa Ulaya katika mchezo wa awali Bernabeu na mabao yake 14 yalimfanya kuifikia rekodi ya Lionel Messi aliyoiweka katika msimu mmoja wa 2011/12.
Kwa ujumla Ronaldo amefunga mabao 64 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, matatu nyuma ya nyota wa Barcelona, Messi, na anayo 54 katika mechi 44 zilizopita za Real na Ureno ikiwa ni pamoja na 'hat-trick' tano.
Real ina hofu ya kumkosa mchezaji ghali zaidi duniani Gareth Bale baada ya Jumamosi kupata majeraha katika goti lake la kulia wakati wakicheza huko San Sebastian.
Winga huyo wa Kimataifa wa Wales, ambaye alifumania nyavu na kuifanya Real kuwa mbele kwa mabao 2-0, alihitaji kushonwa nyuzi mbili, taarifa za ndani zilieleza.
Hata hivyo, Ancelotti hakuongea lolotekatika mkutano na waandishi wa habari kuhusu majeraha ya winga huyo.
"Ushindi huu umetuimarisha na pia tumeepuka kuwa na mejeruhi na tulikuwa imara," Muitalia huyo alisema. "Tumecheza vizuri sana, kwa akili. Tulianza kwa kasi na tulikuwa imara sana katika kipindi cha pili.
"Kila mmoja alikuwa katika nafasi nzuri kimchezo ninafurahi kwa kuwa haikuwa rahisi. Ninajisikia furaha kuiongoza timu hii. Ninao wachezaji ambao wanapenda kupigana, tutaendelea kupigana hadi mechi ya mwisho."
Msimu uliopita katika michuano hiyo Dortmund ilipeperusha ndoto za Real baada ya kuitoa kwenye hatua ya nusu fainali.
Dortmund, pia ilijiweka katika nafasi ya kufanya vizuri katika mechi ya leo baada ya Jumamosi kutoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya VfL Wolfsburg kwenye mechi ya Bunsdesliga, hivyo kushika nafasi ya pili katika kinyang'anyiro hicho ambacho Bayern Munich imeshaibuka mabingwa.
"Ushindi huu ni mzuri kwetu," alisema Kocha wa Dortmund, Juergen Klopp. "Kama tungepoteza tungekuwa tumenyosha mikono juu kutokana na presha ya mchezo. Ilikuwa ni muhimu kushinda na kuelekea mechi ya Jumanne tukiwa tunajisikia vizuri.
"Hatuwezi kuachia chochote bure. Jumanne (leo) tunahitaji kuwa na nusu ya pili nzuri na baada ya hapo tutaona nini kinatokea."
Klopp atakuwa na kinara wake wa kucheka na nyavu Robert Lewandowski baada ya mechi iliyopita kuwa nje akitumikia adhabu.
Lewandowski alifumania nyavu dhidi ya Wolfsburg Jumamosi, hivyo uwezo wake wa kucheka na nyavu utakuwa muhimu leo kama Wajerumani hao wanataka kusonga mbele.
Kocha Jose Mourinho amekuwa akilalamika kuwa kikosi chake hakina mshambuliaji, lakini vyovyote itakavyokuwa, Chelsea bado inayo nguvu ya kuwafunga mabingwa wa Ufaransa Paris St Germain na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo.
PSG, bila nyota wake Zlatan Ibrahimovic ambaye ni majeruhi, haitahitaji kufunga bao Uwanja wa Stamford Bridge leo ili kuitoa Chelsea, kwani tayari ina faida ya mabao 3-1 kwenye mechi ya awali jijini Paris.
Ni wazi hautakuwa rahisi, hasa ikifahamika kuwa ushindi wa 2-0 unatosha kwa Chelsea kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.
Hata kama washambuliaji wake watashindwa kufumvutia Mourinho, Chelsea ina viungo wanaojua kuteleza na kuibeba miamba hiyo ya Magharibi mwa London.
Hata hivyo, Chelsea katika Uwanja wa Stamford Bridge ni habari tofauti kwa timu ambayo imepoteza mechi tatu za nje katika michuano yote msimu huu.
Jumamosi iliitandika Stoke City 3-0 katika Ligi Kuu England huku mabao yote yakifungwa na viungo: Mohamed Salah, Willian na Frank Lampard, ambaye mpaka sasa ameshafumania nyavu mara 250 tangu akiwa West Ham United, Swansea City na sasa Chelsea. Pia ana mabao mengine 29 kwa timu ya Taifa ya England.
Mechi hiyo pia ilikuwa ya 77 bila kufungwa kwa Mourinho katika vipindi vyake viwili kwenye klabu hiyo, jambo ambalo atahitaji kuonyesha ubora wake tena Ulaya.
"Tunajua haitakuwa rahisi nyumbani, lakini tutabadili matokeo," kiungo Eden Hazard, ambaye alifunga kwa penalti katika mechi ya awali alisema.
"Tulithibitisha tunaweza kufanya hivyo kabla, na tunaweza kufanya hivyo tena wiki hii (leo)."

No comments:

Post a Comment