NYOTA wa muziki wa Injili nchini, Jennifer Mgendi, amefyatua nyimbo kadhaa mpya ikiwa ni maandalizi ya kutoa albamu yake nyingine itakayotoka sambamba na filamu iitwayo 'Shelina'.
Akizungumza na MICHARAZO, Mgendi alisema nyimbo hizo zilizorekodiwa katika studio tofauti za jijini Dar es Salaam pia zitatumika kama 'soundtracks' katika filamu yake mpya aliyoanza kuiandaa iitwayo 'Shelina' na kazi hizo zote zitaachiwa rasmi sokoni kwa pamoja Juni mwaka huu.
Mgendi anayetamba kwa sasa na albamu ya 'Hongera Yesu', alizitaja nyimbo hizo mpya kuwa ni 'Kaa Chonjo', 'Kimbilia Msalabani', 'Jambo Jipya', 'Watasubiri Sana', 'Nitakungoja', 'Akiba Haiozi' na 'Ita Damu' zilizorekodiwa katika studio za Fishcrab kwa Lamar, Highland Records, Fabrice Records na Tika Studios inayomilikiwa na Kameta.
'Nimeanza kurekodi nyimbo kwa ajili ya albamu yangu mpya ijayo itakayoitwa 'Kaa Chonjo', safari hii zimerekodiwa katika studio kadhaa maarufu na baadhi ya nyimbo hizo natarajia kuziachia wakati wowote kuanzia sasa na zitakuwa pia kwenye filamu yangu ninayoiandaa ya Shelina' ambayo itawaashirikisha nyota kadhaa wa filamu na muziki wa Injili na kuachia sambamba na albamu hiyo," alisema Mgendi.
No comments:
Post a Comment