STRIKA
USILIKOSE
Friday, July 4, 2014
Abdi Banda asilimia 100 Simba
IMETHIBITIKA kuwa, beki wa kushoto wa Coastal Union Abdi Banda atakipiga Msimbazi na siyo Jangwani tena kama ilivyokuwa ikiripotiwa baada ya Simba kuonyesha dhamira zote za kumnyakua kinda hilo.
Banda anayeichezea pia timu ya taifa ya vijana U20 aliyeng'ara katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopita, alikuwa akitajwa kuviziwa na vigogo wa Simba na Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.
Hata hivyo Meneja wa mchezaji huyo, Abdul Bosnia aliliambia MICHARAZO mapema kuwa walikuwa wakisubiri kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Simba ili viiongozi wapya wamalizane naye kuhusu mchezaji huyo aliyekuwa akiwindwa pia na klabu za Ligi Kuu ya Kenya.
Bosnia alisema aliufahamisha uongozi wa Simba kwamba Banda bado ana mkataba na Coastal Union hivyo wakazungumze na viongozi wenzao wakishamalizana waje mezani kumaliza mambo.
"Simba ndiyo inayoonyesha dalili za kumtaka Banda na niliwajulisha kwamba mchezaji bado ana mkataba na Coastal na kuwataka wakazungumze na wenzao wakimalizana waje kwangu," alisema.
Alisema hata hivyo viongozi hao walimfahamisha kuwa watafanya jambo hilo, ila wanamalizia kwanza uchaguzi wao uliofanyika Juni 29, ndipo waje kuzungumza naye.
"Walinifahamisha kuwa walikuwa wakisubiri wamalize kwanza uchaguzi wao kisha waje kuzungumza nasi na hizi ni dalili za wazi za kumtaka Banda kuliko ilivyo kwa Yanga ambao wamekaa kimya mpaka sasa," alisema.
Bosnia alisema yeye kama meneja wa Banda hana tatizo lolote juu ya mchezaji huyo kutua klabu gani, muhimu zinazomtaka zimalizane kwanza na Coastal kwani ndiyo inayommiliki kwa sasa.
Simba inamtaka Banda ili kumpunguzia majukumu Issa Rashid 'Baba Ubaya', wakati Yanga ilitajwa kumtaka beki huyo ili kumpa nafuu Oscar Joshua kufuatia taarifa za kutaka kumtema David Luhende.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment