STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 4, 2014

RAMADHANI KAREEM, JUMAA MUBARAK


 
LEO ni Ijumaa ya kwanza ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Mwezi ambao waumini wa Kiislam wameamriwa kufungwa swaumu ikiwa ni utekezaji wa Nguzo ya Nne kati ya Tano za Dini ya Kiislam.
Waumini wanaomuogopa Allah Subhanna Wataala pamoja na kuuhofia Moto Siku ya Hesabu wanaendelea na swaumu wakiingia siku ya 7 na wengine 6 Allah Aalam!
Kama miongoni mwa waumini, nilikuwa nakukiumbushia waliopo kwenye mfungo kuitekeleza ibada hiyo kama nasaha yangu kwao ili kufanikisha lengo la swaumu kama Mwenyezi Mungu anavyosema kwenye Suratul Bakarah (2-183-5) kuwa 'Enyi Mlioamini mmefadhilishiwa funga na Ramadhani kama waliofaridhishiwa waliokuwapo kabla yenu ili kuwa Wacha Mungu'.
Muhimu mfungaji licha ya kujikurubisha kwa kutenda mambo mema ambayo hata katika miezi ingine imehimizwa, kuwahurumiwa wasio na uwezo na kujikithirisha kusoma Kur'an na kufanya Ibadat mbalimbali, lakini pia ni vyema kuchunga swaumu zao.
WAUMINI wa Kiislam wapo kwenye Mfungo wa Mwezi Ni wajibu wa mwenye kufunga kumhimidi Mwenyezi Mungu kwa sifa zake alizojihimidi Mwenyewe, kwa kuwa kamuafikisha kufanya hiyo Siyyam na kuihiifadhi Swaum yake ili asiitie uchafu na kuiumbua weupe wake kwa maasi, na aepuke yale ambayo Mtume,  swalla-Llahu alayhi waa aaliyhi wasallaam, aliyesema katika Hadithi, ‘Matano humfungulisha mwenye kufunga: uwongo, na usengenyaji, na mtindo wa kubeba maneno na kuyapeleka baina ya watu ili kuwafitinisha, na yamini ya uwongo na mtazamo wenye matamanio.’ 
Mambo matano hayo yampasa muumini ajikinge nayo, na ayaepuke na aiihifadhi Swaum yake isikumbwe nayo.

La kwanza: Uwongo. Asiwe mwenye kutumia uwongo kwenye maneno yake na katika habari zake na katika kukataa kwake na katika jawabu yake, hasa hasa uwongo juu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

La pili: Usengenyaji – ghiiba – ni kule kuwataja ndugu zako Waisilamu kwa yale wasio yapenda hata ukiwa mkweli. Anapenda mmoja wenu, kula nyamamfu ya nduguye? Na ghiiba – kusengenya ni kati ya madhambi makubwa – kabaa-ir – lakini kwenye mwezi wa Ramadhani, hilo huwa shadidi zaidi kwa vile linabatilisha thawabu za swaumu. 


La tatu: Tena kuna namiima. Na nammaam ni yule mwenye kuchochea fitina baina ya ndugu, na hilo vile vile ni miongoni mwa maasi makubwa kabisa kupita yote. Na kwenye funga ni shadidi zaidi.


La nne: Tena kuna yamini ya uwongo, hiyo hubatilisha thawabu za mwenye kufunga kwa sababu kaonyesha dharau kwa cheo cha Mola na kamtaja pahali pasipo pa haki.


La tano: Tena mtazamo wa matamanio. Yaani ni mtazamo kwa mtu asiyekuwa mahram kwa jicho la kumtaka. Wingi ulioje wa mtazamo huu na wingi ulioje wa mtazamo huu katika zama zetu hizi. Nakuunyamazia hayo si jambo lenye kuhimidiwa  (kutajwa kwa wema).

Kila pahala unapogeukia utawakuta mabinti wenye kukosa hayaa. Na imekuwa wanawake wengi wamelivua jilbab la hayaa na amekuwa kijana ambaye hajanawirika (kwa nuru ya ilmu yenye kumpambanulia kwamba mtazamo ule ni sumu ya imani yake) lengo la mtazamo huu. Katika miezi isiyokuwa ya Ramadhani mtazamo huo huwa mshale kati ya mishale ya ibilisi. Na katika mwezi wa Ramadhani, zaidi ya hayo yalotangulia, mtazamo huo hubadilisha ujira wa Swaumu.

Jitahidini enyi ndugu zangu, msiwe wenye kukodoa macho kwa asiokuwa mahram, ambaye haikujuzieni nyinyi kuwaangalia. Na jikingeni na hayo kama mnavyoweza. Unaloachiwa katika hayo ni kile kinachosadifu mtazamo wako wa mwanzo. Ukiwa wakati unakwenda na hapo kuna mabibi na jicho lako limetua juu yao, basi mtazamo huo wa mwanzo hauna ubaya. Lakini tena usikodoe jicho baada ya hapo. Kwa sababu ule mtazamo wenye hatari, ambao unautegemea kuenea yale mazuri ya yule bibi, ndiyo wenye kubatilisha Swaumu.
Jumaa Mubarak, Ramadhani Kareeem! Allah atuwezeshe kuwa ni wenye kuzingatia Inshallah!

No comments:

Post a Comment