STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 4, 2014

Ujerumani, Ufaransa hapatoshi leo Brazil

* Wenyeji Brazil na Colombia kumaliza udhia

* Neymar shakani, akiwaonya majirani zao

Wenyeji Brazil

Wakali wa Colombia
UTAMU wa Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Brazil unatarajiwa kuanza kunoga leo wakati michezo ya Robo Fainali itakapochezwa kwa timu wenyeji Brazil kuvaana na majirani zao Colombia, huku mabingwa wa zamani Ujerumani na Ufaransa wakikumbushia nusu fainali ya mwaka 1982 nchini Hispania.
Ujerumani walionyakua taji hilo la Dunia mara tatu itawavaa mabingwa hao wa mwaka 1998 katika mechi ya kwanza ya hatua hiyo kwenye uwanja wa Maracana, kuanzia saa 1 usiku kwa saa za Afrika Mashariki huku kila timu ikitambia nyota wake na kuwa na kiu ya kusonga mbele katika nusu fainali.
Ni mechi ambayo haraka inaleta kumbukumbu ya mwaka za mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia baina ya timu hizo mwaka 1982, pale Ujerumani iliposhinda kwa "matuta" baada ya sare ya 3-3  inayokumbukwa kwa rafu mbaya ya Harold Schumacher dhidi ya mshambuliaji wa Ufaransa, Patrick Battiston.
Ujerumani watakuwa wakicheza robo fainali yao ya tisa mfululizo ya Kombe la Dunia, lakini kikosi cha Joachim Low kimeshindwa kuonyesha ubora nchini Brazil tangu kiliposhinda 4-0 dhidi ya Ureno katika mechi ya ufunguzi.
Katika mechi yao iliyopita, walishinda kwa shida 2-1 dhidi ya Algeria katika muda wa nyongeza na kuzua mijadala mizito nyumbani kwao kuhusu kiwango cha timu hiyo, mbinu na staili ya uchezaji.
Moja ya mijadala ni kwa kocha Low anapojadili kikosi chake kwamba amchezeshe Philipp Lahm kama kingo ama beki wa kulia. Mijadala mingine ni kiwango cha chini cha wachezaji kama Mesut Ozil na Mario Gotze.
Wajerumani watapata nguvu kwa kurejea kikosini kwa beki Mats Hummels baada ya kuikosa mechi dhidi ya Algeria kutokana na kuwa mgonjwa kambini, lakini Shkodran Mustafi ameaga mashindano hayo kutokana na maumivu ya misuli ya nyuma ya paja.
Katika ushambuliaji, Andre Schurrle anatarajiwa kuanza baada ya kufunga goli akitokea benchini dhidi ya Algeria, wakati Thomas Muller ataongoza mashambulizi, jambo linalomaanisha kwamba Miroslav Klose atalazimika kuanzia benchi kama atahitaji kuvunja rekodi ya dunia ya kufunga magoli mengi zaidi.
Wakati Ujerumani wanaonekana kuwa na uchovu baada ya ratiba ngumu kaskazini, Ufaransa wanakuja kwenye mechi wakiwa na nguvu zaidibaada ya kuifunga Nigeria 2-0 katika raundi iliyopita.
Ufaransa hawakuwa katika kiwango cha kutisha katika hatua ya 16-Bora lakini wamecheza soka zuri mara moja moja katika michuano hiyo, huku kocha Didier Deschamps akiwatumia washambuliaji wake kiwerevu.
Uwanja ni wake Paul Pogba kuonyesha kwanini anatajwa kama mmoja wa viungo bora zaidi duniani akiwa na umri wa miaka 21 tu. Nyota huyo wa Juventus amekuwa na kiwango kinachopanda na kushuka katika fainali zake hizi za kwanza za Kombe la Dunia lakini tayari ameonyesha ishara za uwezo wake wa kuwa mchezaji mshindi kwa kufunga goli la kwanza dhidi ya Nigeria.
Bila shaka mechi hiyoya mapema itakuwa ni 'tamu' kuliko inavyotarajiwa kutokana na kuwepo kwa mchuano wa kimya kimya wa ufungaji baina ya Karim Benzema wa Ufaransa dhidi ya Thomas Muiller ambao wanatofautiana kwa bao moja, Muiller akiwa na manne sawa na Neymar na Messi, huku Benzema akiwa na matatu akilingana na Arjen Robben, Robin van Persie wa Uholanzi, Enner Valencia wa Ecuador na Xherdan Shaqiri wa Uswisi.
Katika mechi itakayopigwa baadaye saa tano usiku, wenyeji Brazil ambayo awali kulikuwa na hofu ya kukosa huduma za nyota wao Neymar aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu ya misuli, itashuka dimbani kuwakabili Colombia waliopo kwenye kiwango cha hali juu katika fainali hizo.
Colombia iliyoshinda mechi zake zote za makundi kwa asilimia 100 na kuing'oa Uruguay kwa mabao 2-0 katika muda wa kawaida, itawakabili wenyeji wakiwa wanafahamu wapo nyumbani na wakipewa sapoti na maelfu ya mashabiki vichaa wa soka wa taifa hilo lenye watu wanaokadiriwa Miliioni 200.
Wakimtegemea nyota wao mpya anayeongoza kwenye safu ya Ufungaji Bora wa Fainali hizo za Brazil, James Rodriguez, Colombia bila shaka itakuwa na kiu kubwa ya kutinga hatua hiyo ya Nusu fainali ili kuzidi kuboresha reklodi yao baada ya kipindi cha muda mrefu. Kwani haikuwahi kutinga hatua ya Riobo Fainali waliyopo sasa wala kunusa Nusu Fainali tangu ianze kushiriki michuano hiyo.
Hatua kubwa kwake ni kutinga 16 Bora katika fainali za mwaka 1990 zilipofanyika nchini Italia, na mara zote ilikuwa ikikwamia katika hatua ya makundi na kwa kasi waliyoonyesha msimu huu ni wazi Brazil inapaswa kujichunga la sivyo watashuhudia wakibaki kuwashangilia wageni na wao kuwa watazamaji.
Rodriguez aliyefunga mabao matano na kufunika kabisa pengo lililokuwa likitarajiwa kuiathiri nchini baada ya Radamel Falcao kuumia na kuondolewa kikosini, anatazamwa kama tumaini ya Colombia kuweka historia kubwa zaidi kwa nchi hiyo ambayo pia ina wakali kadha wanaotamba duniani kama Jackson Martinez, Adrian Ramos na kipa mkongwe aliyeweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji mzee kucheza Fainali za Kombe la Dunia akimpiku Mcameroon, Roger Milla. Faryd Mondragon mwenye miaka 43.
Hata hivyo Brazil siyo rahisi kwao kukubali kufanywa daraja na majirani zao hao katika mchezo huo na nyota wake Neymar amenukuliwa kujiandaa kumfunika Rodriguez na Colombia kwa ujumla.
Neymar alisema Brazil imedhamiria kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia kwa ushindi dhidi ya Colombia mjini Fortaleza, licha ya kumsifu  James kwa kiwango chake katika michuano hiyo akimtaja kama 'Mchezaji Mkubwa', ila akisistiza kuwa yeye na wachezaji wenzake watahitimisha safari nzuri ya wapinzani wao hao katika michuano hiyo leo.
"Colombia ni timu nzuri, wamekuwa wakishinda sana, wameonyesha wana nguvu wakati wa mechi zao. James ni bonge lamchezaji: yeye ni nyota, ingawa ni mdogo sana, miaka 22 kama mimi. Amekuwa akionyesha namna alivyo mchezaji mkubwa na tunapaswa kumpongeza kwa kila anachokifanya.
"Lakini natumai safari yake katika Kombe la Dunia hili imefikia tamati sasa na Brazil iendelee – kwa heshima yote, hakika."
Mbali na Neymar, Brazil pia inatambia nyota kama Fred, Davud Luis, Oscar, na kipa aliyegeuzwa 'Mungu' kwa sasa akiabudiwa kwa kuivusha timu yao hatua hiyi kwa kudaka penati mbili za Chile, Julio Cesar.
Je ni Ujerumani au Ufaransa zitakazotangulia Nusu fainali ma vipi wenyeji Brazil watatibua rekodi ya Colombia ya kushinda mechi kwa asilimia 100? Tusubiri kuona hiyo usiku.

No comments:

Post a Comment