STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 4, 2014

Wambura wenzake wapigwa 'stop' Simba

UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umetangaza rasmi kumsimamisha uanachama aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi uliofanyika Jumapili, Michael Wambura, pamoja na wengine 70 kutokana na kwenda kufungua kesi kwenye mahakama za kawaida za nchi, imeelezwa jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyoko mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini jana, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema kuwa maamuzi ya kumsimamisha Wambura na wenzake yametolewa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao walikutana kwa mara ya kwanza juzi.
Aveva alisema kuwa kamati hiyo imechukua maamuzi ya kuwasimamisha kwa kufuata ibara ya 11 (1) (b) ya katiba ya Simba na kuongeza kuwa hatma yao itajulikana katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu unaotarajiwa kufanyika Agosti 3.
Rais huyo alisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuilinda katiba ya Simba na uanachama wa klabu hiyo katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
"Suala la Wambura lilijadiliwa lakini hatukufikia mwafaka na kuamua lipelekwe katika mkutano mkuu ili wanachama waamue, tumewasimamisha wale 69 na katika kesi ya mwaka 2010 aliyofungua Wambura alishirikiana na Juma Mtemi, naye tumemsimamisha," alieleza Aveva.
Alisema kuwa katika mkutano mkuu unaokuja wanachama watajadili pia ripoti ya fedha na mabadiliko ya katiba ambayo yameonekana kuwa na mapungufu.
Kiongozi huyo pia aliwashukuru wanachama wote wa Simba waliompigia na wasiompigia kura kwa sababu kila mmoja ametekeleza haki yake ya kidemokrasia.
Alisema uchaguzi umekwisha sasa wanachama wote ni kitu kimoja waungane kuijenga klabu yao.
"Sasa tuungane kutekeleza ahadi zetu ambazo ni pointi tatu uwanjani, umoja na maendeleo, tusahau tofauti zetu, Simba ni muhimu kuliko sisi sote," alisema kiongozi huyo.

WACHEZAJI KULIPWA LEO
Aveva alisema kuwa uongozi wake unatarajia leo kuwalipa mishahara wachezaji wake ili kuwaweka tayari kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kitaanza mazoezi yake Jumatano Julai 9 huku pia wakianza maandalizi ya tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 8 mwaka huu.
Alisema kwamba kocha mkuu wa timu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic, atarejea nchini Jumatatu na taratibu za kumtumia tiketi ya ndege zimeshaanza.

WAJUME WAPYA, KAMATI MPYA
Aveva aliwataja wajumbe watatu wapya wa kuteuliwa watakaoingia katika Kamati ya Utendaji kuwa ni Mohammed Nassor, Musley Al Ruwey na Salim Abdallah huku wengine wawili waliobaki kwa mujibu wa matakwa ya katiba atawatangaza baadaye.
Uongozi huo mpya pia jana ulitangaza kamati tatu zitakazosimamia shughuli mbalimbali za kila siku lakini akisema Kamati ya Usajili itakuwa ni ya muda na itaongozwa na Hanspoppe Zacharia, Kassim Dewji, Saidi Tulliy, Musley Al Ruweh, Crescentius Magori na Rodney Chiduo.
Aliwataja wajumbe wanaounda kamati ya mashindano itakayokuwa chini ya mwenyekiti, Mohammed Nassor, kuwa ni Iddi Kajuna, Jerry Yambi, Hussein Simba na Mohammed Omary.
Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana ni Tulliy, Ally Suru, ambao wote ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Patrick Rweyemamu, Mulamu Nghambi, Madaraka Suleiman na Amina Poyo.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment