STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, October 31, 2014

Dk Ndumbaro amtangazia 'vita' Malinzi

http://api.ning.com/files/E2q56SVxnZdQOwcR6HaKivVPSGgbEBhknIlVqnDS5NGE1d3uRzai0weL*GGoN62tttqwLdV3ITGWsWmHb7LWq2escwr5Sbk8/3.jpg
DK Damas Ndumbaro
MWANASHERIA Dk. Damas Ndumbaro, amefichua kuwa amekata rufaa kupinga adhabu ya miaka 7 aliyopewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku akisisitiza kuwa ataendelea kufanya kazi zake za kuwawakilisha wadau wa soka watakaohitaji huduma yake ya uwakili.
Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, Ndumbaro alisema kuwa TFF na Kamati zake hazina mamlaka ya kumfungia kufanya kazi za uwakili, isipokuwa Jaji Mkuu wa Tanzania na serikali.
Ndumbaro alisema kuwa anashangaa kuona amehukumiwa na Kamati ya Nidhamu kwa kosa la maadili na kuongeza kwamba kamati hiyo haikupaswa kusikiliza tuhuma zilizokuwa zinamkabili.
Alisema kuwa adhabu hiyo aliyopewa ni dalili za wazi za 'chuki' dhidi yake kwa sababu yeye alichokizungumza ilikuwa ni maamuzi ya klabu 12 za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambazo zilikubaliana na kumteua yeye kupitia Kampuni yake ya Uwakili ya Maleta & Ndumbaro ya jijini.
"Sikuzungumza kwa niaba yangu, nilikuwa na ridhaa ya klabu 12, isipokuwa Stand United na Coastal Union, Kamati hii inatumiwa na Jamal Malinzi, ndio kamati iliyoipa ushindi Stand United kupanda Ligi Kuu," alisema Ndumbaro.
Wakili huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba alisema kuwa alianza kuonekana ni adui mara baada ya kukataa kushiriki katika ufujaji wa fedha ambapo kwa vipindi vitatu tofauti alikataa kusaini hundi za fedha ambazo TFF iliomba kutoka kwenye Bodi ya Ligi Kuu (TPL).
Alisema kwamba kwa sasa shirikisho hilo linakabiliwa na ukata baada ya kutumia kiasi cha Dola za Marekani 696,823 bila ya kupata kibali cha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambao wamezitoa kwa ajili ya udhamini wake wa timu ya Taifa (Taifa Stars).
Mbali na matumizi hayo, pia Jamal Malinzi anadaiwa kujilipa binafsi Dola za Marekani 159,140 ndio maana sasa wanaamua kufidia fedha hizo katika gharama nyingine ikiwamo makato ya Sh.1,000 kwa kila tiketi," alisema Ndumbaro.
Aliongeza kuwa anashangaa kuona TFF inaendelea kukata Sh. 1,000 katika kila tiketi za mashabiki wanaoingia uwanjani kushuhudia mechi za Ligi Kuu Bara na kutaja kiasi kilichokatwa hadi kufikia jana ni Sh. milioni 193.2 zilizotokana na mashabiki 193,257 walioingia viwanjani kushuhudia michezo ya ligi iliyoanza Septemba 20 mwaka huu.
Alisema pia anashangaa kuona rufaa yake aliyokata tangu Oktoba 21 mwaka huu haijapangiwa siku ya kusikilizwa lakini kikao cha Kamati ya Nidhamu kilichokutana kumjadili kilichukua siku mbili.
Aliongeza kuwa leo Oktoba 31 mwaka huu siku ya 10 na hakuna dalili za kusikilizwa, tutaendelea kuhesabu,  mambo mengi yako katika rufaa.
Alisema kwamba yeye hajawahi kutoa siri za shirikisho na kueleza kuwa kanuni za ligi na mikataba inayoingiwa si siri.
Taarifa rasmi ya Dk Ndamburo iko hivi:
31 Oktoba 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KAMPUNI ya Mawakili ya MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, ambayo inawakilisha vilabu 13 vya LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA, inapenda kutoa tamko kwa umma kama ifuatavyo:
1. Kampuni ya MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, iliteuliwa na vilabu 13 vya LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA, kwa maandishi, ili kuwawakilisha na kuwatetea katika kudai haki zao ambazo tayari SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA (TFF) liliamua kukata fedha za udhamini na viingilio vya mechi pasipo kuwashirikisha. Dk. Damas Daniel Ndumbaro, wakili mwandamizi, ndiye aliyekabidhiwa file hilo kwa mujibu wa utaratibu wa ofisi yetu.
2. Kwamba, tarehe MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, kupitia wakili wake mwandamizi, Dk. Damas Daniel Ndumbaro, iliandika barua ya madai (Demand Notice) TFF na kuongea na waandishi wa habari.
3. Kwamba tarehe Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mh. Juma Nkamia (MB) aliitisha mkutano kati ya TFF (ambayo iliwakilishwa na Wilfred Kidau-Mjumbe Kamati ya Utendaji, na Selestine Mwesiga, Katibu Mkuu), Bodi ya Ligi, Vilabu vya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania na Dk. Damas Daniel Ndumbaro (kama wakili wa vilabu). Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mh. Juma Nkamia alitoa fursa kwa TFF, Bodi ya Ligi, na Wakili wa vilabu kutoa maelezo yao na hatimaye  Mh. Juma Nkamia alitoa maelekezo kama ifuatavyo:
i.  Jamal Malinzi sio Rais wa Nchi, na aliwaagiza wawakilishi wa TFF wafikishe ujumbe huo kwa Bw. Jamal Malinzi.
ii.  Makato ya Tshs. 1000/= kwa kila tiketi ni wizi wa mchana.
iii. TFF isitishe makato ya 5% na Tshs. 1000 kwa kila tiketi mpaka watakapoongea na kukubaliana na vilabu
4. Baadaya hapo, MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, ilikutana na vilabu ambayo vilikuwepo siku hiyo na kukubaliana kuwa sasa tusibiri majadiliano na TFF na kwamba MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, ikiongozwa na Dk. Ndumbaro iandae mapendekezo ili yajadiliwe na mkutano mkuu wa vilabu.
5. Kwamba tarehe 11 Oktoba 2014 TFF ilifanya mkutano wa Kamati ya Utendaji na kutoa tamko kuwa kumekuwa na taarifa za upotoshaji kuhusu kanuni za ligi kuu na kwamba Sekretariati ya TFF imefungua mashtaka dhidi ya Dk. Ndumbaro ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Ligi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba.
6. Kwamba Kamati ya Utendaji ya TFF iliendelea kusema kuwa Kutokana na madai ya klabu kuhusu vipengele kadhaa vya Kanuni za Ligi Kuu 2014/15, Kamati ya Utendaji imepanga kukutana na viongozi wa klabu za Ligi Kuu siku ya Jumamosi, Oktoba 18 mwaka huu ili kuwasikiliza na kushauriana kuhusu changamoto za kikanuni na uendeshaji wa mashindano kwa ujumla na kwamba.
7. TFF imefanya kosa kumshitaki Dk. Ndumbaro kwa kofia ya Mjumbe wa Bodi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Simba kwasababu barua toka MALETA & NDUMBARO ADVOCATES, barua za vilabu 13 na taarifa kwa vyombo vya habari ilikuwa bayana kuwa Dk. Ndumbaro anawakilisha vilabu vya ligi kuu kama wakili toka kampuni ya MALETA & NDUMBARO ADVOCATES na wala sio mwakilishi wa Bodi au Mwenyekiti wa uchaguzi wa Simba kwasababu hakukuwa na uchaguzi wa Simba.
8. Kwamba TFF inakiri kuwa klabu za Ligi kuu zinapaswa kukutana na TFF kujadili kasoro za Kanuni za Ligi kuu. Hapa TFF inakiri kuwa haikukutana na vilabu katika mchakato wa kutunga kanuni hizi na kwamba kanuni hizo zinakasoro. Ifahamike kwamba hayo ndio madai ambayo vilabu kupitia MALETA & NDUMBARO ADVOCATES iliyapeleka TFF kwa maandishi.
9. Tarehe 7 Oktoba 2014 TFF iliepeleka Mshtaka katika Kamati ya Nidhamu dhidi ya Dk. Ndumbaro. Kamati ya Nidhamu ilipanga kusikiliza Mashtaka hayo tare 09 / 10 / 2014 saa 08: oo mchana, yaani siku mbili tu baadaya ya kuwasilishwa katika kamati ya nidhamu. Mashitaka hayo yalijaa ubabaishaji na chuki binafsi dhidi ya wakili wa vilabu 13 vya Ligi Kuu.
10. Kwamba TFF ililazimisha kusikiliza mashtaka hayo kwa haraka na dharura ya ajabu pasipo kuwepo Dk. Ndumbaro ambaye alitoa taarifa ya maandishi kuwa atakuwa safarini Nchini Marekani kikazi, kwa barua ya tarehe  8th October 2014.
11. Kwamba Kamati ya Nidhamu ya TFF ilitoa maamuzi ya kumfungia Dk. Ndumbaro asijihusishe na Soka kwa kipindi cha miaka saba pasipo kutoa sababu za msingi za kufanya hivyo wala kutoa nakala ya hukumu hiyo.
12. Kwamba MALETA & NDUMBARO ADVOCATES kwa niaba ya vilabu vya Ligi kuu inapinga adhabu hiyo ya uonevu kwa misingi ifuatayo:
i.  Kamati ya nidhamu ya TFF haina mamlaka ya kisheria ya kushughulikia suala hili. (ARTICLE 2, 3,76 and 77 of TFF Disciplinary  Code)
ii. Kamati ya nidhamu ya TFF ilikosea kuamua suala hili bila kutoa haki ya msingi ya kuisikiliza MALETA & NDUMBARO ADVOCATES na Dk. Damas Daniel Ndumbaro
iii. Hakuna Chombo chochote cha TFF chenye mamlaka ya kumzuia au kumfungia Wakili wa kujitegemea kuwawakilisha wateja wake.
13. MALETA & NDUMBARO ADVOCATES inaandaa kesi ya madai dhidi ya TFF kwa kuizuia isifanye biashara yake halali.
14. MALETA & NDUMBARO ADVOCATES inapenda kuwajulisha wadau wote kuwa kupinga maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya TFF sio kosa. Ikumbukwe kuwa JAMAL MALINZI aliwahi kupinga maamuzi ya FIFA, CAF na TFF kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, kwa njia ya Circular Resolution, ili kuunda Kamati za Rufaa ya Uchaguzi, Kamati ya Maadili na Club Lincensing. Lakini leo Jamal Malinzi hataki kupingwa huyu ni dikteta.
15. Kwamba MALETA & NDUMBARO ADVOCATES inaandaa mashtaka dhidi ya Uongozi wa TFF, katika mambo yafuatayo:
i.  Ubadhirifu wa US$ 200,000 fedha za TBL udhamini wa Taifa Stars
ii. Kupinga Maamuzi ya FIFA kurejea Karume ( Haya yalikuwa mapendekezo haikuwa amri)
iii.Kufanya matumizi na manunuzi bila kibali cha kamati ya fedha ambayo ndiyo kamati ya manunuzi ya TFF kwa mujibu wa kanuni za manunuzi za TFF, manunuzi yaliyofanyika yanahusiana na Vifaa vya michezo wakati wa maboresho ya Taifa stars, Tiketi za ndege za Taifa Stars, timu ya wanawake na za vijana katika michezo yake na hotel za kambi ya timu ya Taifa ambapo hakukuwa na tenda zilizotangazwa wala ushindanishwaji wa aina yoyote jambo linaloashiria matumizi mabaya ya madaraka na fedha na kwa kuwa Rais ndiye msimamizi wa shughuli za sekretariet kikatiba jambo hili linakuwa pamoja na mengine ni suala la kimaadili kwa sheria za mpira.
16.  Kwamba  MALETA& NDUMBARO ADVOCATES inaandaa mashtaka dhidi ya Jamal Malinzi kwa Kupinga Maamuzi ya FIFA, CAF na TFF ili kufanya marekebisho ya Katiba mwaka 2013.
17. Tarehe  21 Oktoba 2014, Dk. Damas Daniel Ndumbaro alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya TFF lakini mpaka sasa Kamati ya Rufaa ya Nidhamu TFF haijasema lina inakaa. Tunatarajia kuwa haraka na dharura iliyotumika katika kuamua shauri katika kamati ya nidhamu itatumika pia kuamua shauri katika rufaa. Leo ni siku ya 10 toka rufaa ikatwe lakini bado kimya wakati ilichukua siku 2 tu kusikiliza kesi ya msingi.
KWAHIYO Dk. Damas Daniel Ndumbaro wa MALETA & NDUMBARO ADVOCATES kwa naiba ya wateja wetu tunasema kuwa:
a. Tutaendelea na kuwawakilisha wateja wetu kwa uadilifu wa hali ya juu.
b. Kwamba madai yote tuliyoyasema katika barua ya awali dhidi ya TFF ikiwemo madai yanayohusiana na Mkutano Mkuu yapo pale pale.
c.  Tumekata Rufaa dhidi ya maamuzi ya kamati ya nidhamu ya TFF kuanzia tarehe 21 Okotba 2014
d. Tunaandaa mashtaka dhidi ya Uongozi wa TFF kwa ubadhirifu wa fedha za umma
e. Tunaandaa mashtaka dhidi ya TFF kwa kosa la kupinga agizo la FIFA kurejea Karume
f.  Tunaandaa Mashtaka dhidi ya Jamal Malinzi kwa kosa la kupinga Maamuzi ya TFF, CAF na FIFA katika mabadiliko ya Katiba ya TFF mwaka
2013.
Wako
Dk. Damas Daniel Ndumbaro (PhD)
For: Maleta & Ndumbaro Advocates
www.maletandumbaroadvocates.com
 

Nakala: i. Vilabu 13 vya Ligi Kuu
             ii. Mh. Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
                                      .............
                                  31 Oct 2014

No comments:

Post a Comment