STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, October 31, 2014

Viongozi 'mchwa' Vyama vya Ushirika waonywa

Mrajisi w Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabazibwa akizungumza

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi akizungumza na wanachama wa MHCS
Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabazibwa akizungumza mbele ya wanachama wa MHCS
VIONGOZI wa vyama vya Ushirika nchini wamechimbwa mkwara na kutahadharishwa juu ya tabia zao za wizi na ubadhilifu wa fedha za vyama vyao kwa kuelezwa kuwa watakapobainika kuhusika na vitendo hivyo watafungwa na kulipia fidia kwa hasara zote walizosababisha.
Mkwara huo umetolewa na Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabanzibwa wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa Chama Cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge (MHCS Ltd) katika sherehe za uzinduzi wa ofisi ya chama hicho kijiji cha Kibiki-Chalinze zilizofanyika juzi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambayo alikuwa mgeni rasmi.
Dk Rutabazibwa alisema kutokana na mabadiliko ya Sheria namba 6 ya Vyama vya Ushirika, wanaobainika kufanya wizi na ubadhilifu wa mali za vyama hivyo hawafukuzwi kazi tu au kuhamishwa na kuachwa walivyo badala yake wanafikishwa mahakamani na adhabu ya chini ni miaka miwili pamoja na kulipa fidia ya hasara wanazosababisha.
Mrajisi huyo alisema siku za nyuma kabla ya mabadiliko hayo ya mwaka jana, viongozi na watendaji wa vyama hivyo walikuwa wakifanya wizi wa kufuru na ubadhilifu kwa sababu hakukuwa na sheria kali ya kuwabana.
Dk Rutabazibwa aliusifu uongozi wa MHCS kwa kubuni mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wanachama wake na kuwataka wauendeleze na kufikia lengo la kupanua wigo wa chama hicho nchi nzima kama ilivyokuwa lengo la waasisi wa chama hicho akiwamo Hayati Baba wa Taifa, Mwl Nyerere.
"Nimesikia mkisema kuwa mmepanga kuanzisha mradi kama huo katika mikoa saba tofauti, mimi nawataka mjitanue nchi nzima kama ilivyokuwa lengo la Mwalimu Nyerere alipoasisi Mwenge wa Uhuru ili umulike nchi nzima," alisema.
Aliongeza kitu cha muhimu MHCS ijenge kweli nyumba za bei nafuu ili wanachama na wakazi wa Chalinze waweze kuzimudu na katu asifuate mfano wa asasi nyingine zinazotangaza kujenga nyuma za bei nafuu lakini iliyo ya chini kabisa ikiwa inauzwa Sh Mil 40-50.
"Mkifuata mkumbo huo wa kuuza nyuma kwa bei ambazo hazilengi watu wa chini hamtakuwa mmefikia lengo la kuwasaidia wanachama wenu na watu wengine, hivyo nauomba uongozi wa Ushirika wa Mwenge kujenga nyumba za bei ya chini kweli," alisema.
Kabla ya Mgeni rasmi huyo kuyasema hayo uongozi wa MHCS kupitia risala yao iliyosomwa na Mjumbe wa Bodi hiyo, Hellen Khamsini ulisema eneo jipya lililopatikana Kibiki-Chalinze lenye ukubwa wa Ekari 227 litajengwa nyumba za kisasa na bora zaidi na zile za Mwenge ili kuwarahisishia wanachama wao kuishi katika maeneo bora.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Ahmed Kipozi aliwakaribisha wawekezaji hao wapya katika wilaya yake, lakini akiwataka kutowatenga wenyeji katika mradi huo wa nyumba ili kusaidia kujenga umoja na mshikamano.
DC Kipozi alisema amefurahia MHCS wamejitokeza kuanzisha mradi huo wakati mradi mkubwa wa mji wa Bagamoyo unaofahamika kama Satelite City ukiwa njiani ambao utabadilisha mandhari ya mji huo na kuinua maisha bora ya wakazi wake na wananchi wengine.
Katika sherehe hizo, Dk Rutabazibwa alifungua rasmi ofisi ya MHCS, na kugawa vyeti vya hisa kwa baadhi ya wanachama pamoja na kugawa viwanja kwa wanachama wa ushirika huo ulioasisiwa mwaka 1971 ukiwa na wanachama 25 na sasa ukiwa na wanachama 385.

No comments:

Post a Comment