STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, October 31, 2014

Simanzi! Ben Kiko afariki, Rais JK amlilia


Katibu wa Rais maswala ya Habari, Issa Michuzi kulia akiwa na mtangazaji wa siku nyingi, Beni Kiko wakifurahia jambo wakati wa uhai wake katika tuzo za mwandishi bora 

Ben Kiko enzi za uhai wake
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenela Mukangara kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mtangazaji na Mwandishi Mkongwe na Mahiri hapa nchini wa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo kwa sasa ni TBC Taifa, Ben Hamis Kikoromo maarufu kama Ben Kiko.
Ben Kiko amefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 31 Oktoba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akiendelea na matibabu ya figo baada ya kuhamishiwa hapo akitokea Hospitali ya Jeshi ya Milambo Mkoani Tabora.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mwanahabari na Mtangazaji huyu Mahiri ambaye ametoa mchango mkubwa wa kihabari kwa Taifa letu”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba wa Ben Hamis Kikoromo.
“Namkumbuka Marehemu Ben Kiko, enzi za uhai wake, kama Mtangazaji aliyekuwa na mvuto mkubwa kwa wasikilizaji wake kutokana na namna yake ya kipekee ya kuripoti matukio hususan katika kipindi kilichojizolea umaarufu mkubwa wakati huo cha MAJIRA kilichokuwa kikirushwa hewani na  Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD)”.
 Wakati wa vita dhidi ya Nduli Idi Amin wa Uganda mwaka 1978, Ben Hamis Kikoromo alifanya kazi kubwa kwa Taifa kwani aliweza kuripoti matukio mbalimbali kutoka katika uwanja wenyewe wa vita, na hivyo kuliwezesha Taifa na wananchi kwa ujumla kuhabarika vilivyo na matukio yaliyokuwa yakiendelea.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, pokea salamu zangu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza mmoja wa Waandishi na Watangazaji Mahiri katika Tasnia ya Habari hapa nchini. 
Vilevile kupitia kwako, naomba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi ziifikie Familia ya Marehemu Ben Hamis Kikoromo kwa kupoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia.  Nawaomba Wanafamilia wote, ndugu na Jamaa wa Marehemu wawe wavumilivu na wenye subira wanapoomboleza kifo cha mpendwa wao huku wakitambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete.
  Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika muda wote wa maombolezo, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Ben Hamis Kikoromo, Amina.
Aidha Rais Kikwete ametuma Salamu za Rambirambi kwa Wanahabari kote nchini ambao kwa hakika msiba wa Ben Kiko utakuwa umewagusa kwa karibu. 
Hata hivyo amesema kuondoka kwa Ben Kiko kusiwe chanzo cha wao kukata tamaa, bali kifo chake hakina budi kuwa chachu katika kujituma zaidi, na wawe tayari kuiga yote mazuri aliyoyafanya Marehemu enzi za uhai wake hapa duniani hususan katika Taaluma ya Uandishi wa Habari.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
31 Oktoba, 2014.

No comments:

Post a Comment