STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 22, 2013

Pique asononeshwa kipigo Barca



GERARD Pique alikosa furaha kutokana na kufungwa na AC Milan, lakini alikataa kujadili kiwango cha refa licha ya kosa kubwa alilofanya mwamuzi lililoizawadia Milan goli la kuongoza.
Pique alisema: "Refa anaweza kufanya makosa wakati mwingine lakini hakuna visingizio. Si refa, si uwanja, si chochote".
Beki huyo wa kati wa Barcelona alikiri kwamba "ni matokeo mabaya sana. Walipofunga goli la kwanza tukapoteza umakini. Ni lazima tuongeze ubora, tujifunze na kusubiri mechi ya marudiano Camp Nou kwa ajili ya kufuzu. Pengine sisi si wazuri kama kila mtu anavyosema".
Pique hakutaka kutoa visingizio baada ya kiwango kibovu cha timu yake na akasema: "Uwanja wa San Siro ni mgumu kuchezana tunajua kwamba Milan ni klabu kubwa. Sisi ni Barcelona na ni lazima tubadili matokeo haya".
Walioizamisha Barcelona kwenye Uwanja wa San Siro walikuwa ni Waghana watupu. Kevin Prince-Boateng na Sulley Muntari walifunga magoli magoli mawili katika ushindi wa 2-0 juzi usiku. Hiyo ilikuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, kwa wachezaji wawili kutoka nchi hiyo kufunga katika mechi moja.

KUMEKUCHA MICHUANO YA NSSF





KAMATI ya usajili na uhakiki ya michuano ya Kombe la NSSF kwa vyombo vya habari jana ilianza kazi ya kuhakiki wachezaji watakaoshiriki michuano ya mwaka huu.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Paul Urio, amesema jana jijini kuwa, kamati yao itapita kwenye vyombo vya habari 17 ambavyo timu zao zimethibitisha kushiriki michuano hiyo ili kujiridhisha juu ya uhalali wa wachezaji wao.
Alisema michuano hiyo itaanza Machi 9 katika viwanja vya TCC Sigara vilivyopo Chang'ombe jijini Dar es Salaam.
Urio alisema uhakiki huo utahusisha timu za soka kwa wanaume na netiboli kwa wanawake.
"Tunataka kujiridhisha kama wachezaji kwa kila timu waliosajiliwa ni wanahabari kweli au la," alisema Urio.
Urio aliwataja vingozi wengine wa kamati yao kuwa ni Ridhwani Ramadhani kutoka gazeti la Changamoto  ambaye pia ni katibu wao, Majuto Omary (Mwananchi), Modesti Msangi (Tumaini Media), Julius Kihampa (Jambo Leo) na Mohamed Mharizo (Mtanzania).
Hadi sasa, timu zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo ni Tumaini, IPP, Sahara, Changamoto, Jambo Leo, Free Media na BTL.
Urio alizitaja timu nyingine kuwa ni Radio Kheri, Mlimani, TSN, TBC, New Habari, Uhuru Publishers, Habari Zanzibar, Mwananchi, Global Publishers na waandaaji NSSF





Mechi ya Simba, Prisons yaingiza mil.40/-

Kikosi cha Simba

MECHI ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya mabingwa watetezi Simba dhidi ya wenyeji Prisons iliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa imeingiza Sh. milioni 40.8.
Akizungumza jana, mkuu wa kituo katika kanda hiyo, Blassy Kiondo, alisema jumla ya mashabiki 8,165 walilipa kiingilio cha Sh. 5,000 kila mmoja kushuhudia mchezo huo.
Kiondo alisema kuwa kila klabu imepata jumla ya Sh. milioni 8.7 na kiasi kingine kimekwenda katika taasisi nyingine kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania.
Alisema kuwa kiasi kilichopatikana juzi hakijavunja rekodi iliyowekwa katika mechi ya kwanza ya ligi kuu msimu huu uwanjani hapo iliyowakutanisha Prisons na Yanga ambapo Sh. milioni 50 zilipatikana.
Alisema pia hali ya hewa ya mvua jijini Mbeya nayo ilichangia kupunguza idadi ya mashabiki katika mechi ya juzi.
Hata hivyo, habari za mtaani zinadai kuwa wimbi kubwa la mashabiki lilioibuka kuishabikia timu iliyopanda daraja hadi Ligi Kuu ya Bara msimu ujao ya Mbeya City Council linaweza kuwa moja ya sababu za kupungua kwa mapato katika mechi hiyo.
Simba inayoshika nafasi ya tatu katika msimamo, ilishinda mechi hiyo kwa bao 1-0 na kuifanya ifikishe pointi 31, tano nyuma ya vinara Yanga ambao wana mechi moja mkononi. Azam ni ya pili ikiwa na pointi 36 sawa na vinara, lakini wanabaki katika nafasi ya pili kutokana na tofauti nzuri ya magoli. Azam kama Simba wamecheza mechi 17.   

CHANZO:NIPASHE

MAKOCHA WA MASUMBWI WAHITIMU KOZI YA AWALI


Meja Charles Mbuge wa pili kushoto akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya awari ya ukocha wa mchezo wa masumbwi, Charles Mhilu wakati wa kumalizika kwa kozi hiyo Dar es salaam leo kushoto ni mjumbe wa BFT, Koba Kimanga na Rais wa shirikisho hili, Michael Changalawe.
Baadhi ya makocha wa mchezo wa masumbwi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuhitimu mafunzo ya awali yaliyomalizika jana Dar es salaam 
Meja Charles Mbuge akihojiwa na wana habari wakati wa kufunga mafunzo hayo
Mmoja ya wakufunzi Kulwa Kindondi akihojiwa na wandishi wa habari
kocha Charles Mhilu kushoto akihojiwa kuhusu kozi hiyo
Mmoja ya wakufunzi Kulwa Kindondi kushoto akiwa na Patric Nyembela wa EATV