STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, March 25, 2013

Madhira amlilia Rais Kikwete




MUIGIZAJI mahiri wa filamu, Mbwana Salim 'Bessa' au Madhira, amemlilia Rais Jakaya Kikwete na kuomba kuonana naye ili aweze kumfikishia kilio chake na cha wasanii wenye ulemavu kama yeye.
Bessa ambaye pia ni mtunzi wa riwayana mchoraji, alisema kutokana na wasanii wenye ulemavu kutothaminika wala kutiwa moyo, angependa kuonana na Rais Kikwete akiamini anaweza kusikia kilio chao na kuwasaidia ili nao wawe na hadhi sawa na wasanii wengine nchini.
"Ningependa nipate nafasi ya kuonana na Rais Kikwete ili nimfikishie kilio tulichonacho sisi wasanii wenye vipaji vya sanaa, lakini tunadhalilika kwa sababu ya ulemavu wetu, tafadhali naomba unifikishie ujumbe wangu kwa mheshimiwa," alisema Bessa.
Msanii huyo ambaye ni mtunzi mkuu wa vichekesho na filamu za kampuni ya Al Riyamy alisema hali wanayotendwa wasanii wenye ulemavu nchini ikiwemo kunyonywa kimasilahi na kutothaminika hata kwa viongozi wanaosimamia sanaa inawakatisha tamaa, ilihali waliamua kujitegemea.
"Wapo watu wenye ulemavu kama sisi walikata tamaa na kuwa tegemezi, sisi tumeamua kutumia vipaji vyetu kujiajiri na kuwatia moyo wengine, lakini bado tunaangaliwa kama watu duni na kukatishwa tamaa, naimba serikali iliangalie hili," alisema msanii huyo.
Aliongeza kuwa, pamoja na juhudi anazozionyesha akiwa pia ni mwalimu wa chekechea, mchoraji na mtengenezaji wa chaki na batiki, alisema kuna haja wasanii waenye vipaji kama yeye watupiwe macho kuwafanya wapige hatua kimaendeleo na kuwahamasisha wengine kujitegemea.

Golden Bush yazidi kutoa dozi ikiisubiri Wahenga FC

Kikosi cha Golden Bush Veterani
SIKU chache kabla ya kuvaana na wapinzani wao, timu ya Golden Bush Veterani imeendelea kutoa dozi baada ya mwishoni mwa wiki kuinyuka Kibangu Veterani kwa mabao 4-1 kabla ya kuwakung'uta tena watoto zao Golden Bush Fc kwa magoli 2-0.
Mechi hizo za kujipima nguvu zilichezwa Jumamosi na Jumapili ikiwa ni maandalizi ya kuvaana na wapinzani wao, Wahenga Fc pambano litakalochezwa kwenye uwanja wa Tp Afrika, Sinza siku ya Pasaka.
Katika mechi yao dhidi ya Kibangu, Golden Bush walipata ushindi wao kupitia mabao ya Sadik Muhimbo aliyefunga mara mbili, Said Swedi 'Panucci' na Di Natale, huku bao la kufutia machozi la Kibangu liliwekwa kimiani na Daudi.
Katika mechi iliyochezwa jana, dhidi ya vijana wao wanaoshiriki Ligi ya TFF- Kinondoni, Wazee wa Golden walipata ushindi wa 2-0 na kuendeleza ubabe kwa watoto hao kwani wiki iliyopita waliwanyuka mabao 2-1.
Katika hatua nyingine, Mlezi wa Golden Bush Veterani, Onesmo Waziri 'Ticotico' ameamua kutangaza dau kwa wapinzani wao iwapo wataibuka na ushindi au kuambulia sare atakuwa tayari kuwapa papo hapo kitita cha Sh 200,000.
Mechi hiyo ya Golden Bush na Wahenga, inatarajiwa kuhudhuriwa na mgeni rasmi, Kamanda Thobias Andengenye na itachezwa majira ya saa 10 jioni ambnapo lineup ya Golden Bush, kwa mujibu wa msemaji wao itakuwa kama ifuatavyo;

Philemon, Said Swedi, Faraji, Majuto Komu, Wisdom Ndlovu, Godfrey Bonny, Onesmo Wazir 'Ticotico' (captain), Waziri Mahadhi  'Mandieta', Athumani Machupa 'Magoli', Herry Morris na Sadik Muhimbo.

Rais TFF kufungua semina Copa Coca Cola








Na Boniface Wambura
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina elekezi ya michuano ya Copa Coca Cola itakayofanyika kesho (Machi 26 mwaka huu).

Semina hiyo inayoshirikisha makatibu wakuu wa vyama vya mpira wa miguu mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na itafunguliwa na Rais Tenga kuanzia saa 3 kamili asubuhi.

Washiriki wengine katika semina hiyo itakayokuwa na watoa mada kutoka TFF na wadhamini kampuni ya Coca Cola ni waratibu wa michuano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).

MAPINDUZI SIMBA YALIKUWA BATILI-TFF

Wanachama wa Simba walipokutana Machi 17

Na Boniface Wambura
MKUTANO Mkuu wa Dharura ulioitishwa na wanachama wa Simba, Machi 17 mwaka huu na kuuondoa uongozi wa klabu hiyo si halali kwa vile haukufuata taratibu, na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) halitambui Kamati za Muda.
Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Machi 24 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa.
Kamati imebaini kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 22(2) ya Katiba ya Simba, Mkutano Mkuu wa Dharura unaitishwa na Kamati ya Utendaji baada yawanachama wasiopungua 500 kuwasilisha ombi hilo kwa maandishi na kujiorodhesha. Mkutano huo haukuitishwa na Kamati ya Utendaji ya Simba.
Utaratibu huo haukufuatwa ambapo barua ya Mkutano huo iliandikwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo badala ya Kamati ya Utendaji ya Simba ambayo ndiyo matakwa ya Katiba ya Simba.
Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Kamati ya Utendaji ndiyo inayoitisha Mkutano Mkuu wa Dharura baada ya kuhakiki uhai na uhalali wa wanachama waliojiorodhesha kuomba mkutano huo.
Kamati imesisitiza kuwa Katiba za wanachama wote wa TFF hazina
kipengele cha kura ya kutokuwa na imani na uongozi (vote of no
confidence), ndiyo maana uko nyuma wanachama wa Yanga, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) walipiga kura hiyo, na TFF kutotambua uamuzi wao.
Hata Katiba ya Simba haitoi mamlaka kwa Mkutano Mkuu wa Dharura kufukuza uongozi uliochaguliwa.
Katiba za wanachama wote wa TFF zimezingatia katiba mfano za
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambazo zinasema
kiongozi ataingia madarakani kwa uchaguzi, na si kuteuliwa (Kamati ya
Muda).
Pia Kamati imesema endapo wanachama wa Simba wangefuata taratibu na uongozi ukakataa kuitisha mkutano, wanachama wangetuma ombi hilo TFF kupitia Kamati ya Sheria ili kutoa mwongozo kwa uongozi wa Simba .
TFF ina mamlaka ya kutoa adhabu kwa viongozi wa wanachama wake wanaokwenda kinyume cha Katiba zao. Pia Kamati imesisitiza kwa wanachama wa TFF kuitisha mikutano yao kwa mujibu wa taratibu na Katiba zao, na wale ambao muda umefika wafanye hivyo haraka.

TENGA APONGEZA WACHEZAJI, SERIKALI USHINDI WA STARS

Na Boniface Wambura
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
ameipongeza wachezaji wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi, washabiki, mdhamini na Serikali kwa kufanikisha ushindi wa jana.

Tenga amesema ushindi huo umetokana na ushirikiano kutoka kwa wadau wote, na hasa wachezaji walioonesha kiwango kikubwa kulinganisha na mechi zilizopita ikiwemo kiwango cha kujituma uwanjani.

Amesema Serikali ni mdau mkubwa wa mpira wa miguu katika miundombinu, usalama na idara zake mbalimbali ikiwemo Uhamiaji ambayo imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mechi hiyo ambapo Taifa Stars iliifunga Morocco mabao 3-1.

MECHI YA TAIFA STARS YAINGIZA MIL 226/


Na Boniface Wambura
PAMBANO la mchujo la Kombe la Dunia  kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) lililochezwa jana (Machi 24 mwaka huu) na Stars kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 imeingiza sh. 226,546,000.

Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 32,614 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh.10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 34,557,864.41, maandalizi ya mchezo sh. 28,450,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh.
8,625,641.88.

Nyingine ni bonasi kwa timu ya Taifa Stars sh. 28,798,220.34, asilimia 15 ya uwanja sh. 18,917,141.01, asilimia 20 ya gharama za mechi sh.25,222,854.67 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) sh. 6,305,713.67.

Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh.71,885,135.82 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,783,428.20 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.