STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, April 13, 2014

Liverpool, Manchester City hapatoshi leo England

Liverpool v Manchester  City kivumbi kitakuwaje leo?
Chelsea wenyewe wataanza mapema kibarua chao ugenini na Swansea City
LONDON, England
LIGI Kuu ya England (EPL) inatarajiwa kuendelea leo kwa timu zilizopo Tatu Bora zinazowania ubingwa ambao kwa sasa unashikiliwa na Mashetani Wekundu zitashuka dimbani kusaka pointi tatu za kuelekea kwenye ndoto zao kabla ligi haijafikia ukingoni mwezi ujao.
Vinara Liverpool chini ya Brendan Rodgers watakuwa dimba la nyumbani la Anfield kuialika Manchester City wanaokamata nafasi ya tatu, huku Chelsea iliyofanya maajabu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufuzu Nusu Fainali, itakuwa wageni kwa Swansea City.
Liverpool wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 74, pointi mbili zaidi ya Chelsea na nne zaidi ya wapinzani wao watakaovaana nao Anfield na ushindi wowote kwao moja ya timu hizo ina maana msimamo mzima kwa nafasi tatu za juu utabadilika.
Pambano hilo la Anfield litawakutanisha ndugu Yaya Toure anayekipiga Manchester City dhidi ya kaka yake Koro Toure wa Liverpool, huku Luis Suarez akiangaliwa kwa jicho la ziada kuona kama atafunga bao na kuweka rekodi ya kufumania mabao mengi katika msimu mmoja.
Nyota huyo wa Uruguay amefunga mpaka sasa mabao 29, akifuatiwa kwa mbali na mchezaji mwenzake wa Liverpool, Danile Sturridge mwenye mabao 20 kisha Yaya Toure akifuatia akiwa mabao 18 matatu zaidi ya Muargentina, Sergio 'kun' Aguero.
Upande wa pili pambano la Swansea wanaokamata nafasi ya 15 katika msimamo wakiwa na pointi 33 itakuwa na kazi ngumu kuwazuia Chalsea ambao wana furaha ya kuwanyoa PSG ya Ufaransa kwa mabao 2-0 na kufuzu Nusu Fainali akiungana na timu za Bayern Munich ya Ujerumani, Real Madrid na Atletico Madrid za Hispania kuwania kucheza Fainali.
Licha ya kocha Jose Mourinho kuiponda mara kwa mara safu ya timu yake, lakini timu hiyo wiki iliyopita kwenye ligi hiyo ilipata ushindi wa kishindo wa mabao 3-0 dhidi ya Stoke City mabao yakifungwa na viungo wake, Mohammed Sallah, Willian na Frank Lampard.
Hiyo ni kuonyesha kuwa hata kama mabeki wa Swansea watawakaba vilivyo, akina Samuel Et'oo, Fernando Torres na hata Demba Ba anayetokea benchi, bado Chelsea ni nouma kwa viungo wake kufuimania nyavu, hali inayofanya mechi hiyo kusubiriwa kwa hamu.

Azam kuweka historia kwa kutangazwa mabingwa wapya?

Azam Fc
KLABU ya soka ya Azam leo kuwa Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014? Hilo ndilo swali linalotawala vichwa vya mashabiki wa soka nchini wakati kitimtim cha ligi hiyo kitakapoendelea tena leo kwenye viwanja vinne tofauti.
Azam ambayo haijapoteza mechi yoyote mpaka sasa katika ligi hiyo, itakuwa ugenini kwenye uwanja wa Sokoine kuvaana na wenyeji wao Mbeya City, huku mabingwa watetezi Yanga pia watakuwa kwenye uwanja wa ugenini dhidi ya Oljoro JKT jijini Arusha.
Hata kama Yanga itashinda pambano lake la Sheikh Amri Abeid kwa idadi kubwa ya mabao haitawasaidia kama Azam itashinda jijini Mbeya kwa sababu haitaweza kuzifikia pointi ilizonazo Azam ambayo Alhamisi ilikata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataiga mwakani.
Azam iliyo kwenye kiwango bora kwa sasa ilikata tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa mwakani baada ya kuilaza Ruvu Shooting mabao 3-0 katika mechi ya kiporo siku ya Alhamisi na kufikisha jumla ya pointi 56, akisaliwa na pointi tatu tu za kutangazwa mabingwa.
Klabu hiyo kama itaishinda Mbeya itafikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikia hata na Yanga wanaowapumulia kwa mbali na pia itaweka rekodi ya kutwaa taji hilo bila kupoteza mechi yoyote kama  ilivyowahi kufanya Simba mwaka 2011.
Yanga inayopo nafasi ya pili na pointi 52 kufuatia kuilaza Kagera Sugar kwa mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa siku ya Jumatano, itakuwa jijini Arusha kuomba wapete ushindi na pia kuiombea mabaya Azam mjini Mbeya ili wasubiri mechi za kufungia msimu kujua hatma yao.
Mbali na mechi hizo mbili ambazo ndizo zinazoangaliwa sana kwa sababu ya nafasi yake ya kutoa bingwa mpya wa msimu wa 2013-2014, pia leo kutakuwa na mechji nyingine mbili Simba iktakuwa uwanja wa Taifa kuikaribisha Ashanti Utd na Mgambo kuialika Kagera.
Simba itakuwa ikitaka kulinda heshima yake tu mbele ya Ashanti inayopigana kuepuka kushuka daraja kwa sababu hata ikishinda haiwezi hata kuingia kwenye Tatu Bora.
Vijana wa Msimbazi wanaonolewa na Zdrakov Logarusic yenyewe ina pointi 37 na kama itashinda mechi hiyo na ile ya watani zao Yanga itafikisha pointi 43 ambazo zimeshapitwa na wapinzani wao wa juu.
Hata hivyo Ashanti imeapa kuitoa nishai 'Mnyama' ili kufikisha pointi ambazo zitawanusuru kushuka daraja ikiwa ni msimu wao wa kwanza tangu warejee kwenye ligi hiyo, huku Mkwakwani Tanga Mgambo nayo itakuwa na kibarua cha kusaka ushindi mbele ya Kagera.
Timu hiyo nayo ipo kwenye janga la kushuka daraja, japo nafasi yake ya kusalia kwa msimu ujao ni kubwa kutokana na rekodi yao ya kushinda mfululizo kwenye duru la pili ikiwa imezitungua Simba, Yanga na Coastal Union.
Msimamo Top 4
                                  P    W     D     L     F    A    GD  PTS
01.Azam                    24   16    08   00   48   14   34   56
02.Yanga                   24   15    07   02   58   17   41   52
03.Mbeya City          24   12    10   02   30   17   13   46
04.Simba                  24   09    10   05   40   25   15   37

Real Madrid yaua, Barca ikipigwa na vibonde La Liga

Gareth Bale aliifungia Real Madrid bao la pili dhidi ya Almeria

REAL Madrid usiku wa jana ilikwea hadi nafasi ya pili wakiwashusha wapinzani wa Barcelona baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Almeria, huku Barca wenyewe wakifa kwa bao 1-0 dhidi ya timu chovu ya Granada katika Ligi ya Hispania.
Angel di María alianza kuandika karamu ya mabao ya wenyeji ambao wametoka kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakitarajiwa kuvaana na watetezi Bayern Munich kwa kufunga bao la kwanza katika dakika ya 28 na kudumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Gareth Bale aliiandikia Real Madrid bao la pili dakika ya 53 akimalizia kazi nzuri ya Mfaransa Karim Benzema kabla ya Benzema kumpa pande Isco dakika tatu baadaye na kuandika bao la tatu na dakika tano kabla ya pambano hilo kuisha Alvaro Morata alihitimisha karamu kwa kufunga bao la nne kwa kazi ya Illarramendi na kuwafanya Madrid kufikisha pointi 79 na kulingana na vinara Atletico Madrid ambao watashuka dimbani leo kuumana na Getafe kwa kutofautiana uwiano wa mabao na kufunga na kufungwa.'
Barcelona waliokuwa wakishikilia nafasi ya pili wameshuka hadi ya tatu wakiwa na pointi 78 kutokana na kulazwa bao 1-0 na Granada uwanja wa ugenini kwa bao la mapema la Yacine Brahim.
Nazo timu za Osasuna na Real Vallodolid zilishindwa kutambia juzi kwa kutofungana, huku Celta Vigo ikiwa nyumbani kwao walilazimishwa sare ya mabao 2-2 na Real Sociedad na Levante ikafa ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Villarreal.

Arsenal yaivua ubingwa Wigan, yatinga Fainali za FA









KLABU ya Arsenal imetinga Fainali ya Kombe la FA baada ya kuwavua taji waliokuwa mabingwa watetezi Wigan Athletic kwa kuitupa kwenye hatua ya Nusu Fainali kwa mikwaju ya penati 4-2 kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120 katika pambano kali lililochezwa uwaja wa Wembley.
Arsenal sasa itasubiri kujua inacheza na nani kati ya timu ya Hull City na Sheffield United katika mechi ya Fainali itakayochezwa Mei 17 kwenye uwanja huo huo maarufu uliopo London.
Kutinga huko kwa Arsenal kumewapa faraja wa kukata kiu ya muda mrefu bila klabu hiyo kunyakua taji lolote tangu walipotwaa taji la FA mwaka 2005.
Timu ya Wigan iliyotwaa taji hilo mwaka jana kwa kuilaza Manchester City, ilikuwa wa kwanza kuandika bao katika dakika ya 63 kupitia Jordi Gomez aliyefunga kwa penati kufuatia Per Mertesacker kumuangusha Callum McManaman.
Mjerumani huyo hata hivyo alisahihisha makosa yake kwa kuisawazishia Arsenal bao zikiwa zimesalia dakika nane kabla ya mchezo huo kumalizika na timu hizo kuongezewa dakika 30 zilizoisha patupu na kufuatiwa na hatua ya kupigiana mikwaju ya penati.
Kipa Lukasz Fabianski alikuwa shujaa kwa kuokoa penati mbili za awali za Wigan zilizopigwa na Caldwell na Collison huku  Mikel Arteta, Källström, Olivier Giroud na Santi Cazorla kuzamisha zao wavuni dhidi ya mbili za Wigan zilizofungwa na Beausejour na McArthur.