STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, August 21, 2013

Kim Poulsen aita 24 kuivaa Gambia

 
Kocha Kim Poulsen

Na Boniface Wambura
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameita kambini wachezaji 24 kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu nchini humo.
Wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini Agosti 29 mwaka huu kabla ya saa 1 kamili usiku. Kambi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kwenye hoteli ya Accommondia jijini Dar es Salaam.
Makipa walioitwa katika timu hiyo Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na David Luhende (Yanga).
Viungo Khamis Mcha (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Dilunga (Ruvu Shooting), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Amir Kiemba (Simba), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga), John Boko (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na Juma Liuzio (Mtibwa Sugar).

Veterani kuchuana Tamssha la Gym, Victoria Sound kumwaga burudani

Bwendi ya Victoria Sound itakayopamba Tamasha la Home Gym
TIMU za soka za maveterani na klabu za jogging za mkoa wa Dar es Salaam zinatarajiwa kuchuana na kupamba tamasha maalum la kuadhimisha miaka 15 ya kituo cha mazoezi cha Home Gym litakalofanyika wiki ijayo jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo litakalohusisha michezo mingine kama ya kutunisha misuli, kunyanyua vitu vizito, kukimbiza wanyama kama kuku, kanga na sungura litafanyika Agosti 31 kwenye kiwanja cha Mwenge, Dar es Salaam na litapambwa na burudani toka bendi ya Victoria Sound inayotamba na nyimbo kama 'Shamba la Bibi'.
Mkurugenzi wa Home Gym, Andrew Mwangomango aliiambia MICHARAZO kuwa kituo chao kimeandaa tamasha hilo kuadhimisha mafanikio yao tangu kilipoanzishwa rasmi mwaka 1998.
Mwangomango alisema tamasha hilo litaenda sambamba na burudani na michezo mbalimbali ikishirikisha klabu za maveterani na jogging na kutaja baadhi yake kuwa ni Mwenge Shooting, Mabenzi, Survey, Meeda, Mapambano, 501 Veterani, Home Gym wenyewe, Coca Cola Veterani, NMB Veterani, Magenge 20 Jogging Team, Kingungi Jogging na nyingine.
Mwangomango alisema kwa upande wa soka mshindi atazawadiwa mbuzi beberu huku upande wa watunisha misuli na kunyanyua vitu vizito na michezo mingine pia watazawdiwa.
"Kwa sasa tunafanya mipango kwa ajili ya mgeni rasmi atakayejumuika nasi katika tamasha hilo ambalo mbali na kusherehekea miaka 15 ya kituo chetu, lakini lina lengo la kujenga umoja, urafiki na kufahamiana miongoni mwa wanamichezo wa jijini Dar es Salaam," alisema.
Aliongeza kuwa kwa upande wa burudani wanatarajiwa tamasha lao kupambwa na bendi ya Victoria Sound baada ya bendi waliyoikusudia awali ya Extra Bongo siku hiyo ya Agosti 31 kuwa na majukumu mengine.
"Tulipanga Extra Bongo ya Ally Choki ndiyo itumbuize siku hiyo, lakini ratiba hiyo inaingilia na kazi watakayoifanya siku kama hiyo kwenye viwanja vya Posta katika tamasha la mashule," alisema Mwangomango.

Tuesday, August 20, 2013

Msondo Ngoma yabakiza kidogo kupakua albamu

Waimbaji Shaaban Dede na Juma Kitundu
Wapuliza tarumbeta


Kizazi kipya! Hassani Moshi Tx Junior', Eddo Sanga na Katundu wakifanya mambo
BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' imebakiza hatua chache kabla ya kabla ya kukamilisha albamu yao mpya itakayofahamika kwa jina la 'Suluhu'.
Msondo, ambayo ipo studio tangu katikati ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani, imesharekodi nyimbo zote isipokuwa kwa sasa zinasubiri nyimbo hizo kufanyiwa 'mixing' na kuahiriwa ili kuikamilisha albamu hiyo itakayokuwa na nyimbo sita.
Msemaji wa Msondo Ngoma, Rajabu Mhamila 'Super D' alisema mashabiki wao waanze kujiandaa kusuuza roho zao baada ya kipindi kirefu cha ukimya wa kutolewa albamu mpya kwa sababu wamesalia hatua chache kukamilisha albamu yao ya 'Suluhu'.
Super D, alisema nyimbo zote tano za kukamilisha albamu hizo zimesharekodiwa katika studio zilizopo Mbagala nje kidogo ya jijini Dar es Salaam na wanasubiri kuchanganywa vionjo vyake kabla ya kukabidhiwa rasmi ili mashabiki wao waanze kupata burudani.
"Albamu yetu kwa 'Suluhu' bado kidogo kutoka hadharani, kwani tumesharekodi nyimbo zote isipokuwa zinasubiriwa kufanyiwa 'mixing' kabla ya kuhaririwa na kukabidhiwa rasmi," alisema.
Baadhi ya nyimbo zilizorekodiwa na zitakazokuwa katika albamu hiyo mpya ni 'Nadhiri ya Mapenzi' wa Juma Katundu, 'Lipi Jema' na 'Baba Kibebe' za Eddo Sanga, 'Kwa Mjomba Hakuna Mirathi' wa Huruka Uvuruge, 'Machimbo' na 'Suluhu' wa nyota Shaaban Dede 'Super Motisha'.
Bendi hiyo yenye umri wa zaidi ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwake kwa zaidi ya miaka miwili sasa haijatoa albamu mpya tangu ilipotoa albamu ya mwisho mwaka 2010 iliyofahamika kwa jina la 'Huna Shukrani'.

Bibi Cheka sasa alia videoni

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgb4ddGFF-_jlkI6BjyvEoPbRlZI_PsxKeFVhZEecs4BlpZTswOKt4y3CxqQb7mIcLdbNwj82vP9W7Yp5dJBtOeuEQ_P5nE9EgHXH8UdsNyIxj_qvdPU-STM0-5V9K7qnSWAC3KOMdlGB4u/s640/bi+chekaaaa.jpg
Bibi Cheka
BAADA ya nyimbo zake za 'Ni Wewe' na 'Good Baba Fella' kufanya vyema, msanii mwenye umri mkubwa lakini chipukizi katika muziki wa kizazi kipya nchini, Cheka Hija 'Bibi Cheka' amekamilisha video ya wimbo mpya uitwao 'Nalia' inatarajiwa kuanza kusambazwa wiki hii.
Meneja wa msanii huyo, Said Fella aliiambia MICHARAZO asubuhi hii kuwa, video hiyo iliyorekodiwa na kampuni ya Fast Door na itaanza kutolewa kabla ya 'audio' yake tofauti na nyimbo za nyuma.
Fella alisema wameamua kutanguliza video kabla ya 'audio' katika kuleta tofauti na kazi za awali za mkongwe huyo aliyewahi kuwa mnenguaji wa bendi ya Msondo Ngoma enzi iitwa JUWATA.
"Baada ya kimya tangu alipotoa 'Good Baba Fella', Bibi Cheka amefyatua kazi mpya akiakamilisha video ya wimbo wake wa tatu uitwao 'Nalia' itakayoachiwa wiki hii, wakati 'audio' ikifuata baadaye," alisema.
Fella alisema tofauti na nyimbo za awali zilizomtambulishwa msanii huyo mwenye ambapo aliimba kwa kushirikiana na wasanii wengine, safari hii Bibi Cheka kauimba 'Nalia' peke yake.
Katika wimbo wake wa kwanza wa 'Ni Wewe', mkongwe huyo alimshirikisha Mheshimiwa Temba na aliimba na Godzillah katia kibao cha 'Good Baba Fella'.
Mbali na nyimbo hizo zake binafsi, Bibi Cheka mwenye umri zaidi ya miaka 50 alishirikishwa pia katika nyimbo kadhaa za wasanii wa TMK Wanaume Family, ukiwamo 'Mario' wa Mhe Temba.

Nyilawila atimka Russia, kuzipiga Jumamosi nchini humo

BONDIA mchachari wa ngumi za kulipwa nchini, Karama Nyilawila 'Captain' ameondoka nchini kwenda Russia kwa ajili ya pambano lake la kimataifa dhidi ya mwenyeji wake, Fedor Chudinov atakayepigana naye siku ya Jumamosi (Agosti 24, 2013).
Nyilawila aliyepitia nchini Kenya kwa ajili ya kuungana na wakala wake, Franklyn Imbenzi kwa ajili ya kuelekea Russia, atapanda ulingoni kupigana na Chudinov katika pambano l;a uzito wa kati la raundi nane litakalochezwa kwenye mji wa Vulgo Grad.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited), ambayo ndiyo iliyotoa kibali kwa Nyilawila kwenda Russia, bondia huyo aliondoka juzi Jumapili kupitia Nairobi Kenya kabla ya kuelekea Urusi kwenye pambano hilo.
Hilo litakuwa pambano la kwanza la kimataifa kwa Nyilawila, tangu 2010 alipomtwanga Kreshnik Qato wa Albania  na kutwaa taji la kimataifa la WBF ambalo alikuja kuvuliwa baada ya kugoma kwenda kulitetea ili apigane kirafiki na Francis Cheka  mwaka 2012.
TPBO-Limited, limemtakia kila la heri bondia Nyilawila ili apeperushe vyema bendera ya taifa kwa kufanya vizuri katika pambano hilo la kimataifa litakalomrejesha tena kwenye ramani ya mchezo huo.