STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 16, 2014

Inter Milan yaichabanga Fiorentina kwao

Kitu! mpira ukielekea wavuni mkwa wenyeji Fiorentina
Palacio akishangilia bao lake

MABINGWA wa zamani wa Ulaya, International Milan usiku wa kuamkia leo wameikwanyua Fiorentina ikiwa nyumbani kwao kwa kuilaza mabao 2-1 na kuzidi kuipumulia nyuma yake katika msimamo wa Ligi Kuu ya Italia (Seria A).
Inter walianza kuwashtukiza wenyeji wao kwa kufunga bao la kuongoza dakika ya 34 kupitia Palacio na kudumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili iliwachukua dakika mbili tu kwa Fiorentina kurejesha bao hilo kupitia kwa Cuadrado aliyemalizia kazi nzuri ya Fernandez.
Hata hivyo walikuwa ni wageni waliojihakikishia ushindi baada ya Icardi kuifungia Inter bao la pili na la ushindi dakika ya 65 kwa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Nagatomo.
Kwa ushindi huo, Inter imefikisha pointi39 tano nyuma ya wapinzani wao hao waliopo nafasi ya nne wakiwa na pointi 44.
Kivumbi cha ligi hiyo kinatarajiwa kuendelea tena leo kwa michezo kadhaa likiwamo lile la vinara wa ligi hiyo Juventus itakayoumana na Chievo mjini Turin.

Messi aendelea kufanya maajabu Barcelona ikiua 6-0 nyumbani

Yebaaa! Watatukoma mwaka huu, Messi na Neymar wakipongezana jana
LIONEL Messi ameendelea kudhihirisha hana mpinzani katika medani ya ufumaniaji nyavu wakati usiku wa kuamkia leo alipotupia mabao mawili na kuisaidia Barcelona kuishindilia Rayo Vallecano kwa mabao mabao 6-0 katika mechi ya La Liga, Hispania.
Adriano Correia  alianza kuiandikia Barca bao dakika ya pili tu ya mchezo huo akimalizia kazi ya Pedro kabla ya Messi kuanza vitu vyake kwa kufunga bao la pili dakika ya 36  kwa pasi ya Fàbregas, mabao yalidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa wenyeji kuandika bao la tatu kupitia Alexis Sanchez aliyemalizia pasi ya Messi katika dakika ya 53.
Pedro aliiongezea Barca bao dakika tatu baadaye kwa kasi nzuri ya Fabregas ndipo Messi aliporejea tena kambani kwa kufunga bao lake la pili lililokuwa la tano kwa Barca akisaidiwa na Sánchez na msumari wa mwisho ukapigiliwa na Neymar dakika moja kabla ya kumalizika kwa mchezo huo na kuirejesha Barcelona kileleni ikiitoa Atletico Madrid waliokuwa wamekaa baada ya jana kushinda mabao 3-0 dhidi ya Real Valladorid.
Timu zote zimelingana pointi zikiwa na 60 kila mmoja ila zinatofautisha uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, huku wakifutiwa kwa karibu na Real Madrid ambayo itashuka dimbani leo ugenini dhidi ya Getafe.
Katika mechi nyingine iliyochezwa jana Levante ilishinda nyumbani bao 1-0 dhidi ya Almeria na Celta Vigo imepata ushindi wa mabao 2-0 ugenini leo Jumapili dhidi ya wenyeji wao Villarreal.