STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 19, 2010

Boban awagawa wadau wa soka nchini



UAMUZI wa kiungo nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Harun Moshi 'Boban' kuamua kurejea nchini kwa kuvunja mkataba na klabu yake ya GIF ya Sweden umewagawa wapenzi na wadau wa soka nchini baadhi wakimuunga mkono wengine wakimshangaa.
Baadhi ya wadau wamedai kitendo cha Boban kurejea ghafla nchini na kuiacha timu yake ya GIF ni kuonyesha jinsi wachezaji wa Kitanzania wavumilivu au kuwa tayari kucheza soka la kulipwa kama wenzao wa mataifa mengine.
Mmoja wa wajumbe wa kamati ya fedha ya klabu ya Simba Onesmo Wazir 'Ticotico'alisema hata kama kulikuwa na matatizo yaliyomkera Boban alipaswa kuzungumza na wakala wake kuona namna ya kutatua ikiwemo kuhamishwa klabu nyingine ya nje kuliko kurejea nchini.
"Unajua nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje huja kwa nadra sana na ilipaswa Boban kutumia nafasi hiyo kuangalia mbele katika kipaji chake badala ya kukimbilia kurejea nchini ili kuendelea kuchedza soka la sifa kwa klabu za Simba na Yanga," Ticotico alisema.
Hata hivyo Kocha Mkuu wa timu ya TMK United, Kennedy Mwaisabula, alisema binafsi haoni sababu ya Boban kulaumiwa, iwapo hakuona faida ya kuendelea kucheza soka la kulipwa katika klabu hiyo ya Sweden kutokana na kuonyesha hakuufahamu vema mkataba wake.
Mwaisabula alisema huenda wakala wake, Damas Ndumbaro hakuwa muwazi kwa kiungo huyo na yeye alipoona mambo yapo ovyo hakuona sababu ya kuendelea kuwepo huko, huku akisema uamuzi wa kurejea nchini kucheza soka sio wa ajabu kwani ni suala lake binafsi.
"Sioni sababu ya kumshutumu na kumdhalilisha Boban, kurudi kwake ni sahihi na hasa baada ya kukaa nae kwa saa zima na kuzungumza nae akieleza kila kitu na sio kweli kama kaikimbia baridi au kuwakumbuka washkaji zake," alisema Mwaisabula.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Yanga na Bandari Mtwara, alisema huenda Boban ameona soka la Bongo linalipa kuliko huko Sweden kwani kabla hajaenda huko tayari alishakuwa na uwezo wa kiuchumi akimiliki nyumba na gari la kisasa.
Mwaisabula alisema pia Boban hatakuwa mchezaji wa kwanza kucheza soka la nyumbani badala ya nje ya nchi akiwataja, Tresot Mputu wa DR Congo, Mohammed Abutrika wa Misri aliodai pamoja na uwezo wa kisoka hawajahi kuwaza au kwenda kucheza soka la kulipwa licha ya kuwindwa na klabu mbalimbali maarufu za Ulaya.

Mwisho

No comments:

Post a Comment