STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 19, 2010

Rage achukua na kurudisha fomu Tabora Mjini





MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Tabora, Ismail Aden Rage, mapema leo asubuhi amekuwa mtu wa kwanza kuchukua na kurudisha fomu ya kuwania Ubunge wa Jimbo la Tabora Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi.
Akizungumza kwa simu kutoka Tabora, Rage, alisema alichukua fomu hiyo ya kuwania kiti hicho kinachoshikiliwa na Juma Siraju Kaboyoga majira ya saa 2;55 asubuhi na kuijaza kabla ya kuirudisha saa 5:30.
Rage alisema kuwa alikuwa ni mtu wa kwanza kujitokeza kuchukua fomu hiyo na pia amekuwa wa kwanza kuirudisha na matumaini yake ni kuibuka mshindi katika uteuzi wa CCM ili aweze kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31.
"Nimekuwa mtu wa kwanza kuchukua na kurudisha fomu ya kuwania Ubunge Jimbo la Tabora Mjini, nikichukua muda wa saa tatu kuchukua na kurudisha fomu hiyo na tumaini langu kama ilivyokuwa uchaguzi wa mwaka 2000, naamini nitashinda," alisema Rage.
Katika uchaguzi huo wa mwaka 2000, Rage aliwania uteuzi wa CCM katika jimbo hilo na kuibuka na ushindi wa kishindo, lakini utaratibu wa chama chake uliliengua jina lake na kumpitisha aliyekuwa mshindi wa pili, Henry Mgombelo aliyekuja kuibuka mshindi wa kiti hicho.
Rage alisema ni yake ya kujitosa katika jimbo hilo ni kuipeperusha bendera ya CCM dhidi ya wapinzani na pia kutaka ridhaa ya wananchi ili awatumikie kama ambavyo amekuwa akijitolea kwa hali na mali kwao hata kabla ya kuwa mbunge.
Alisema kwa vile katiba ya nchi na demokrasia ndani ya chama chake inamruhusu yeyote kuwania uongozi naye haoni sababu ya kujiweka nyuma na haswa kusukumwa kwake na nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo.
Rage aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Wazazi-Tabora mwaka 2004 na kukitetea kjiti chake tena mwaka jana, alisema anaamini chama chake kitampa ridhaa ya kuongoza na wananchi wa Tabora Mjini hawatamuangusha Oktoba mwaka huu.
Mtetezi wa kiti hicho cha Ubunge wa Jimbo la Tabora, Juma Kaboyoga, ndiye aliyekuwa mtu wa pili kuchukua fomu majira ya saa 5:40, ingawa haikufahamika kama aliwahi kurejesha au la.

Mwisho

No comments:

Post a Comment