STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 19, 2010

Nukuu kali za kukumbukwa Kombe la Dunia 2010





JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MAKOCHA na wachezaji wamekuwa wakizungumzwa mara kwa mara, si kwa sababu ya viwango vyao uwanjani pekee, bali pia kwa sababu ya kauli zao za nje ya uwanja. Zifuatazo ni nukuu kali za kukumbukwa zilizowahi kutolewa nao wakati wa michuano ya mwezi mmoja ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.

Milovan Rajevac
* "Nyie watu, hebu tumieni akili. Yeye si shujaa, yeye ni muongo mkubwa. Ni mkono gani wa Mungu? Ule ni mkono wa shetani," kocha wa Ghana, Mserbia Milovan Rajevac, alisema kuhusy mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez, ambaye alizuia kwa mikono mpira uliokuwa ukivuka mstari wa goli katika dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza kwenye mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
‘Mkono wa shetani’ wa Suarez uliinyima Ghana nafasi ya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kufuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia.


Patrice Evra
* "Tunajihisi kama taifa dogo la mchezo wa soka na hili linaumiza. Hakuna cha kuelezea zaidi ya kusema kwamba hili ni balaa," nahodha wa Ufaransa, Patrice Evra, akielezea kwa uwazi hitimisho la kiwango chao kibovu katika fainali zilizomalizika za Kombe la Dunia 2010. Ufaransa, sio tu ilimaliza ikiwa mkiani katika kundi ambalo ilitarajiwa kuwa kinaea, lakini pia ilikumbwa na kashfa ya wachezaji wake kugomea mazoezi kufuatia kutimuliwa kikosini kwa mshambuliaji Nicolas Anelka.

Jean-Louis Valentin
* "Hawataki kufanya mazoezi, ni kashfa. Najiuzulu, naachoa ngazi kwenye shirikisho. Hapa sina zaidi cha kufanya. Narudi zangu Paris," Mkurugenzi wa timu ya Ufaransa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Soka la Ufaransa, Jean-Louis Valentin, alisema baada ya wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa kugomea mazoezi kufuatia kutimuliwa kikosini kwa Anelka.

Diego Maradona
* "Hii ilikuwa ni (kama) ngumi kutoka kwa Muhammad Ali. Sikuwa na nguvu yoyote ile. Siku niliyostaafu soka ingeweza kufanana na hii, lakini hii ya leo ni mbaya zaidi," Maradona alisema baada ya Argentina kupata kipigo kikali cha 4-0 kutoka kwa Ujerumani, kipigo kibaya zaidi kwao katika fainali za Kombe la Dunia tangu waliposhindiliwa kwa magoli 6-1 katika mechi ya michuano hiyo dhidi ya Czechoslovakia mwaka 1958.

Dunga
* "Siku zote tunatakiwa kushinda, lakini hata tunaposhinda, hawatufurahii kwa madai kwamba hatuchezi soka la kuvutia. Tukicheza soka la kuvutia, hawafurahi kwa sababu hatushindi kwa magoli mengi kama sita au saba hivi. Tukishinda kwa magoli sita au saba, wanaibuka tena na kusema wapinzani wetu ni dhaifu," alisema kocha wa Brazil, Dunga, akidai kwamba hata siku moja, vyombo vya habari huwa haviridhiki.

Gennaro Gattuso
* "Miaka minne iliyopita tuliheshimiwa kwa kuwa mabingwa, leo hii tunacheza hovyo kama mabeberu ya mbuzi vile," kiungo wa Italia, Gennaro Gattuso, alisema katika tathmini isiyo ya kawaida ya kujishutumu binafsi kwa kiwango cha hivyo kiichoonyeshwa na timu yao iliyokuwa ikitetea ubingwa wa fainali za Kombe la Dunia na kumaliza ikiwa mkiani katika Kundi lao.

Howard Webb
* "Anashindwa hata kuwaongoza watoto wake mwenyewe. Sijui anamudu vipi jukumu la kuongoza mchezo wa soka uwanjani," mke wa refa aliyechezesha mechi ya fainali ya Kombe la Dunia, Howard Webb, alisema kabla ya mechi hiyo ya fainali iliyozikutanisha timu za mataifa ya Hispania na Uholanzi.

Cristiano Ronaldo
* "Maholi, kama gwiji mmoja wa soka alivyowahi kuniambia, huwa yanafuatana ... wakati mwingine, kadri unavyojaribu kuhaha ili ufunge, hayaji, na wakati yanapokuja, yanakuja mengi kwa wakati mmoja," alisema mchezaji wa bei mbaya zaidi duniani, Cristiano Ronaldo wa Ureno, kuelekea mechi yao ufunguzi ya hatua ya makundi ya Kombe la Dunia. Kiwango cha Ronaldo katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia kilikuwa cha hovyo, huku mshambuliaji huyo akifunga goli moja pekee.

Roger Milla
* "Kwa hakika hakuna anayeweza kucheza kama mimi! Mauno yangu yalikuwa ya kwanza, tena ya ubunifu kabisa. Unahitaji kunengua kiasili, kuchezesha nyonga. Yote ni kuhusiana na uasili wa mguso binafsi, na inatakiwa uwe na mshawasha kutoka moyoni, iwe ni kitu chako mwenyewe. Na hakika, vilevile unapaswa kufunga goli kwanza, usisahau jambo hilo!" alisema Roger Milla kuhusiana na ushangiliaji wake wa goli kwa kukata viuno.
Mauno ya Milla kwenye kibendera cha kona kila mara alipofunga goli yalikuwa maarufu kama magoli yake aliyoifungia Cameroon wakati nchi hiyo ilipotinga robo fainali za Kombe la Dunia mwaka 1990.

England v Ujerumani
* "England walianzisha soka, lakini Ujerumani wanashinda soka", ulisema utani wa zamani uliotumika wakati wa fainali za Kombe la Dunia kuelezea ushindi wa kishindo wa Ujerumani wa 4-1 dhidi ya mahasimu wao wa jadi katika hatua ya 16-Bora ya Kombe la Dunia.

Sepp Blatter
"Itakuwa ni upuuzi kutolifungua tena jalada la mapendekezo ya kutaka kutumiwa kwa teknolojia ya goli," alisema Rais wa FIFA, Sepp Blatter, baada ya makosa ya marefa kuwagharimu England na Mexico.


Felipe Melo
* "Mimi ni mzoefu wa kupenda. Watu wanaweza kufikiri kuwa kuwa nina sura mbaya, lakini ninapenda kutuma kadi na maua kwa mke wangu na ninapenda pia kutumiwa," beki mpambanaji wa Brazil, Felipe Melo, akisema kuwa yeye si mtu mbaya ‘kiivyo’.

Oscar Tabarez
* "Soka ni kama blanketi fupi, ama litatosha kukufunika kichwani au miguuni," kocha wa Uruguay, Oscar Tabarez, alisema kuhusiana na udhaifu wa mabeki wa Korea Kusini kabla ya mechi yao ya hatua ya mtoano ambayo Uruguay walishinda dhidi ya Waasia hao.

Carlos Marchena
* "Sawa, ni pweza," alisema beki wa Hispania, Carlos Marchena, katika muonekano wa kukasirika wakati alipotakiwa kuelezea maoni yake kuhusiana na utabiri wa pweza uliodai kwamba Hispania watashinda katika mechi yao ya fainali dhidi ya Uholanzi. Pweza huyo maarufu alitabiri kwa usahihi matokeo ya mechi zote saba za Ujerumani wakati wa fainali za Kombe la Dunia.

Felipe Melo
* "Najua kwamba wakati mwingine huwa napitiliza. Ni jambo ambalo huwa nalifikiria muda wote na ninajua kwamba hili ni jambo linalohofiwa na Wabrazili wote. Baba yangu siku zote amekuwa akinisisitiza kuhusu jambo hili, haachi kunikumbusha," alisema kiungo wa Brazili, Felipe Melo, kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia, kuhusiana na umuhimu wa yeye kuepuka kadi nyekundu. Hata hivyo, alitolewa uwanjani katika mechi yao ya robo fainali dhidi ya Uholanzi kwa kumkanyaga mpinzani wake.

Dunga
* "Wakati wakionyesha vipande vya picha za video za fainali za mwaka 1970, unachoona ni sehemu nzuri tu. Kuanzia mwaka mwaka 1958, wanaonyesha vipande vya sehemu nzuri tu, na kuanzia mwaka 1962, pia wanaonyesha vipande vya sehemu nzuri tu. Kama tukichukua vilevile vipande vya sehemu nzuri tu za timu ya Brazil ya sasa, mashabiki wataamini kwamba ndio timu bora kabisa. Lakini leo hii, wanaonyesha vipande vingi vya picha za matukio mabaya kama ilivyo kwa matukio mazuri." Dunga akilalamikia kumbukumbu za timu ya Brazil ya mwaka 1970 na kudai kwamba haikuwa timu nmzuri sana kama inavyoonyeshwa kwenye televisheni.


Marcelo Bielsa
* "Wote tunajifunza kutokana na makosa tunayofanya na kutoka kwenye makosa tuliyoyashuhudia yakifanywa na watu wengine, na kujaribu kuepuka kuyarudia. Huu ni mchakato wa kufanya makosa na kuepuka kuyarudia tena, kuona namna wengine wanavyofanya makosa ili kuyaepuka makosa kama hayo, ni mchakato ambao hausimami, na hauwezi kupimika." kocha asiyetabirika wa Chile, Marcelo Bielsa, akizungumzia umuhimu wa kujifunza kutokana na makosa.
--------------

No comments:

Post a Comment