STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 19, 2010

Njoroge apigiwa ramli Jangwani



HATMA na uwepo wa beki wa kimataifa wa Yanga, Mkenya John Njoroge ndani ya klabu hiyo bado haieleweki, kutokana na uongozi wa klabu hiyo kudai unasubiri maamuzi ya kocha wao, Kostadin Papic
Njoroge aliyetua Yanga akitokea Tusker ya Kenya, kwenye usajili wa dirisha dogo msimu uliopita, amekuwa akitajwa ataachwa ili kutoa nafasi ya kusajiliwa kwa kipa Mserbia, Ivan Knezevic kutekeleza kanuni mpya ya usajili inayosisitizwa na Shirikisho la Soka nchini, TFF.
Kanuni hiyo ya usajili inaelekeza klabu zote za ligi kuu kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi watano, kitu ambacho ndicho kinachomchanganya kocha wa Yanga, kuamua nani abaki na nani aondoke klabuni hapo.
Msemaji wa Yanga, Louis Sendeu aliliambia Micharazo kuwa, pamoja na kwamba usajili wao unaelekea kukamilika vema, lakini hadi sasa haijafahamika nani na nani katika wachezaji wageni watakaokuwa kwenye kikosi hicho hadi kocha wao atakapoamua.
Sendeu alisema kutokana na hilo, ndio maana inakuwa vigumu kwao kuweka bayana kama itamuacha Njoroge au la ambaye ilielezwa awali angeungana na mastaa wengine wa kigeni waliotupiwa virago katika timu hiyo.
"Aisee ni vigumu kuweka bayana juu ya hatma ya Njoroge, tunasubiri suala hilo liamuliwe na kocha na nasisitiza kuwa lolote linaweza kutokea katika usajili huo mpya wa timu yetu ambao utatangazwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya kukamilika," alisema Sendeu.
Tayari uongozi wa Yanga umejinasibu kuwasainisha wachezaji wanne kutoka Ghana, kipa Yew Berko, mlinzi, Isaac Bokye, kiungo Ernest Boake na mshambuliaji Kenneth Asamoah, huku ikidaiwa kukaribia kumalizana na kipa Knezevic aliyetua wiki iliyopita kwa majaribio.
Iwapo kipa huyo atasajiliwa ili kuziba nafasi ya Obren Curcovic basi ni lazima kati ya Waghana wanne au Njoroge, mgeni pekee aliyebakishwa kikosi kilichopita mmojawao jina lake likatwe.
Yanga inayoendelea na mazoezi yao katika uwanja wa Uhuru, imedaiwa tayari imewanasa Nsa Job, Yahya Tumbo, George Minja, Chacha Marwa, Stephano Mwasika, Omega Sunday na Salum Telela kwa ajili ya kikosi kipya kuungana na nyota wengine walisalia msimu uliopita.

Mwisho

No comments:

Post a Comment