STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, July 11, 2013

Arsenal yaongeza dau la Suarez, mwenyewe apagawa

http://www.thenational.ae/deployedfiles/Assets/Richmedia/File/on30-Real-Suarez.jpg
Luis Suarez
LONDON, England
ARSENAL wanaandaa ofa ya paundi za England milioni 35 (Sh. bilioni 82.5) ili kumsajili mshambuliaji nyota wa Liverpool, Luis Suarez, imeelezwa.
Arsenal watatuma ombi la kumtwaa Suarez kwa mara ya pili kwenda kwa Liverpool baada ya ombi lao la awali kukataliwa wiki iliyopita.
Kulikuwa na taarifa Jumatatu isemayo kuwa Arsenal ilituma ofa ya paundi za England milioni 30 (Sh. bilioni 70) kwa Liverpool ili kumtwaa Suarez, na vyanzo vimekaririwa na Goal.com vikieleza kwamba sasa, klabu hiyo ya jiji la London iko tayari kulipa hadi paundi milioni 35 ili kunasa saini ya mshambuliaji huyo wa kutegemewa pia katika timu ya taifa ya Uruguay.
Inafahamika kuwa kocha Arsene Wenger ameamua kuelekeza nguvu zake katika kujaribu kumnasa Suarez baada ya Arsenal kushindwa kulipa dau la kumtwaa mshambuliaji Gonzalo Higuain wa klabu ya Real Madrid ya Hispania.
Suarez anachukuliwa na Wenger kuwa ni mbadala sahihi wa Higuain, ambaye alikaribia kujiunga na Arsenal mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya klabu hiyo kuboresha ofa yake hadi kufikia paundi milioni 23.1 (Sh. bilioni 54).
Hata hivyo, Real Madrid wanasisitiza kuwa hawawezi kumuachia Muargentina Higuain kwa dau la chini ya paundi za England milioni 25.5 (Sh. bilioni 60), na, ingawa Arsenal bado wanamfukuzia Higuain huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa kufaulu vita hiyo, Wenger ameamua kuangalia uwezekano wa kupata mshambuliaji mwingine.
Huku wakiwa na kiasi kikubwa cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya usajili ghali zaidi katika historia ya klabu ya Arsenal, Mfaransa Wenger amewashtua wengi kwa uamuzi wake wa kumfukuzia Suarez wiki iliyopita.
Ombi la Arsenal lilikutana na tahadhari kutoka kwa Liverpool, ambao wanapambana kumbakiza Suarez aliyekaririwa mara kadhaa akisisitiza kutaka kuondoka katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, zaidi akikusudia kuhamia Real Madrid.
Arsenal sasa wataongeza nguvu ya kutaka kumtwaa Suarez baada ya wawakilishi wa mchezaji huyo kueleza kwamba yuko tayari kuhamia kwao ili kutimiza dhamira yake ya kucheza katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.
Katika mahojiano yake na kituo cha redio cha Sport 890 juzi, Suarez alidai kwamba "klabu mbili au tatu hivi" zinataka kumsajili na kwamba amevutiwa sana na taarifa za kutakiwa na Arsenal.
Alicheka kuambiwa kuwa Chelsea wanamtaka, lakini akakiri kwamba amejiandaa kukatisha likizo yake nchini Uruguay ikiwa uhamisho wake utakuwa tayari.
"Je, kuna ombi lolote lililokamilika? Hapana, hadi sasa hakuna lolote. Kuna klabu mbili au tatu ambazo nadhani zinanitaka na klabu yangu inalijua hilo.
"Napaswa kuwapo Liverpool Julai 21 kwa ajili ya ziara yao ya Australia lakini hakuna anayejua kile kitakachotokea. Nimeshasema kile ninachopaswa kusema, na kwanza nitapaswa kuwa pale (Liverpool)  Julai 21 lakini labda mwito wa simu siku moja unaweza kubadili mipango yote hii."
Inafahamika vilevile kwamba kuna kipengele katika mkataba wa Suarez kinachomruhusu kuomba kuzungumza na klabu nyingine ikiwa kutatokea ofa ya kumnunua kwa paundi za England milioni 40 (Sh. bilioni 94) . Hata hivyo, inaaminika kwamba Liverpool wanataka kulipwa paundi milioni 50 (Sh. bilioni 118)ndipo wamruhusu kuondoka.

No comments:

Post a Comment