STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 4, 2013

Meshack Abel kwenda Ulaya akiizitabiria Ashanti, Coastal kufanya maajabu Ligi Kuu 2013-2014


Meshack Abel (kulia) akiwa na wachezaji wenzake wa Kitanzania wanaoichezea Bandari-Kenya, Mohammed Banka, Thomas Mourice na David Naftar
BEKI wa kimataifa zamani wa Simba anayecheza soka la kulipwa nchini Kenya katika timu ya Bandari, Meshack Abel, anajiandaa kuitema timu hiyo na kwenda Ulaya kusaka timu ya kuichezea.
Aidha Abel amezitabiria timu za Ashanti United na Coastal Union ya Tanga kufanya vyema kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza rasmi Agosti 24, akiamini itazipiku vigogo Simba na Yanga zinazopokezana taji kila msimu.
Akizungumza na MICHARAZO toka Kenya, beki huyo wa kati alisema anatarajiwa kuachana na timu hiyo na kutimka Ulaya mara baada ya mkataba wa kuitumikia klabu hiyo ya Ligi Kuu nchini humo utakapomalizika Desemba mwaka huu.
Abel, aliyewahi kuzichezea pia timu za Ashanti United na African Lyon, alisema tayari mipango ya safari ya kwenda Ulaya inafanywa na meneja wake.
Beki huyo aliyejaliwa mwili mkubwa, alisema ingawa bado hajadokezwa anatafutiwa timu katika nchi gani barani huko, lakini mipango ya awali ilikuwa kati ya nchi za Sweden, Norway au Uswisi.
"Mkataba wangu unakaribia kuisha na tayari sina mpango wa kuongeza kwa vile najiandaa kwenda kusaka timu ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya, wakati wowote natimkia huko," alisema.
Alipoulizwa kama alikuwa na mipango ya kurejea nchini kucheza soka baada ya kutamba na timu kadhaa ikiwamo Simba, Abel alisema kwa sasa hafikirii kabisa jambo hilo zaidi ya kusonga mbele kwa madai soka la Bongo limejaa mizengwe tofauti na hali aliyokutana nayo nchini Kenya ambapo klabu zinawathamini na kuwajali wachezaji huku mashabiki wakiwaunga mkono.
"Sifikirii kurudi nyumbani kwa sasa, mawazo yangu ni kusonga mbele zaidi ndiyo maana najiandaa kuondoka Kenya," alisema.
Kuhusu Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013-2014 inayoanza Agosti 24, Abel alisema kwa namna anavyozifuatilia timu shiriki anaweka turufu yake kwa klabu za Coastal Union na Ashanti United kuzifunika Simba na Yanga katika mbio za kuwania ubingwa.
"Simba na Yanga zilikuwa zamani, kama siyo mizengwe Azam ilishazifunika na msimu huu naamini Coastal Union na Ashanti United itaongeza ushindani kwa klabu hizo na kufanya vyema katika ligi ijayo," alisema.
Alisema hata hivyo klabu hizo hazipaswi kujiamini kupita kiasi na badala yake wachezaji wake wajitume na kuhakikisha kila mechi wanapata ushindi na kusaidia kutimiza utabiri wake kwa klabu hizo msimu huu.

No comments:

Post a Comment