STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 4, 2013

Zahoro Pazi hahofii chochote Simba

Zahoro Pazi
 MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Zahoro Pazi amesema hahofii ushindani wa namba katika kikosi cha timu hiyo.
Akizungumza na MICHARAZO, Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa 'Wekundu wa Msimbazi', Idd Pazi 'Father' alisema licha ya kutambua ametua Msimbazi wakati kikosi hicho kikiimarishwa kwa kusajiliwa wachezaji wapya wakiwemo wa ndani na wale wa kigeni bado anajiamini kupata nafasi kwa kipaji na uwezo mkubwa alionao katika soka.
Pazi, alisema kitu cha muhimu kwake atakachozingatia ni kujituma mazoezi, kucheza kwa bidii akipata nafasi kama ilivyotokea katika mechi za kirafiki ambazo Simba imeshacheza hivi sasa zikiwemo mbili zilizopita dhidi ya URA na Coastal Union ambapo timu hiyo ilipoteza mechi zote.
"Ni kweli kuna ushindani mkubwa katika kikosi cha Simba, tumekutana wachezaji wapya wenye uwezo mkubwa, lakini sihofii chochote kwa vile najiamini na nitajitahidi kumridhisha kocha Abdallah Kibadeni kisha kuliacha jukumu mikononi mwake kuamua nani wa kumpanga katika mechi za Ligi zinazotarajiwa kuanza karibuni," alisema.
Pazi alisema katika mechi zote za kujipima nguvu anashukuru alipewa nafasi ya kucheza na kuonyesha uwezo wake, ingawa bado hajafunga bao lolote, akiamini anaendelea kuzoea mazingira ya klabu hiyo iliyowahi kuchezwa na baba yake.
Mshambuliaji huyo alisema kwa namna kikosi chao kilivyo chini ya kocha anayemzimia aliyewahi kumnoa alipokuwa Mtibwa Sugar, anaamini Simba itatamba katika msimu ujao, ingawa alikiri huenda ikakamiwa na kupata wakati mgumu kutimiza ndoto za kurejesha ubingwa baada ya msimu uliopita kuupoteza kwa watani zao Yanga.
Simba inatarajiwa kufungua dimba la pazia la ligi kuu msimu huu kwa kuumana ugenini na timu 'ngeni' ya JWTZ, Rhino Rangers ya Tabora iliyopanda toka daraja la kwanza sambamba na timu za Ashanti United na Mbeya City.

No comments:

Post a Comment