STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 23, 2013

Huyu ndiye Abdi Kassim 'Babi' a.k.a Ballack wa Unguja

Abdi Kassim 'Babi'
MASHABIKI wa soka wa Zanzibar walimbatiza jina la 'Ballack wa Unguja' wakimfananisha na kiungo nyota wa zamani wa Ujerumani, 'Michael Ballack', ingawa majina yake halisi ni Abdi Kassim 'Babi'.
Kiungo-mshambuliaji huyo mmoja wa wachezaji nyota wa Tanzania anayesifika kwa uwezo wa kufumua mashuti makali ya mbali yanayolenga lango, akishikilia pia rekodi kadhaa zinazompaisha nchini.
Babi aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kucheza soka la kulipwa nchini Malaysia katika Klabu ya UiTM FC, ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la kwanza kwenye Uwanja wa Taifa wakati unafunguliwa rasmi mwaka 2007.
Babi alifunga bao hilo kwa 'shuti' kali la umbali wa mita 35 walipoizamisha Uganda 'The Cranes' kwa bao 1-0 katika mechi maalum ya ufunguzi wa uwanja huo wa kisasa, akishikilia rekodi ya kuifungia Azam bao la kwanza kwenye michuano ya kimataifa mapema mwaka huu.
Nyota huyo alifunga bao hilo kwenye Uwanja wa Taifa Azam ikiizamisha Al Nasir Juba ya Sudan Kusini kwa mabao 3-1 katika pambano la kwanza la Kombe la Shirikisho Afrika iliyoshiriki kwa mara ya kwanza.
Kadhalika anashikilia rekodi ya kuichezea kwa mafanikio timu ya Taifa, Taifa Stars kwa miaka 13 mfululizo na kuifungia mabao ya kukumbukwa kama lile lililoipa sare ya 1-1 Tanzania ugenini dhidi ya Algeria katika mbio za kuwania Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2012.
Kama kawaida yake Babi alifunga bao hilo la mapema kwa shuti la umbali wa mita 25 kutoka langoni mwa wenyeji na kuwapa wakati mgumu Algeria kabla ya kuja kulikomboa baadaye.
Ukimuuliza Babi siri ya mafanikio yake ya kuwa na nguvu za kupiga mashuti makali yenye shabaha anakuambia ni kutokana na kupenda kwake kufanya mazoezi ili kuwa na stamina ya kutosha.
Hata sasa akiwa ametua Malaysia, tayari ameshapata mwalimu maalum wa viungo, aliyemtaja kwa jina la Amir anayemnoa ili kumweka fiti ndani ya klabu hiyo inayomilikiwa na Universiti Teknologi MARA iliyopo mji wa Shah Alam- Selango.


Abdi Kassim akiwa na kocha wake wa viungo, Amir
FURAHA
Babi anasema amefurahi mno kupata nafasi nyingine ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi baada ya kukutana na misukosuko mingi tangu aliporejea Tanzania akitokea Vietnam.
Kiungo huyo aliyevutiwa kisoka na nyota wa zamani wa Tanzania, Ramadhani Hamza 'Kidilu' alikuwa Vietnam akiichezea Klabu ya DT Long kwa mkataba wa miaka miwili, lakini alikatisha mkataba wake miezi nane tu akikerwa na ubaguzi.

Abdi Kassim akiwajibika wakati akiichezea Azam. Hapoa ilikuwa ni dhidi ya Tusker katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo aliisaidia Azam kutawazwa kuwa mabingwa mwaka 2013
Baada ya kurejea alitua Azam na kuichezea kwa misimu miwili hadi mapema mwaka huu alipoamua kurejea nyumbani kwao Zanzibar kuichezea KMKM.
Anasema tangu alipotua KMKM alikumbana na wakati mgumu akiwekewa mizengwe mingi na baadhi ya watu wakiwamo rafiki zake wa karibu waliokuwa hawamtaki awepo katika klabu hiyo ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar.
"Kwa kweli namshukuru Mungu kwa kupata nafasi hii, nawashukuru wote walionipa sapoti na kunitakia kila la heri katika harakati zangu za soka na Mungu atawalipia," anasema Babi.
Babi anasema kwa jinsi anavyojiamini na kuamini uwezo wake kisoka upo juu na kumwezesha kucheza kokote, anadai ana miaka 10 zaidi mbele ya kuendelea kusakata kabumbu.
"Nina kama miaka 10 mbele ya kuendelea kucheza soka kwani naamini uwezo na nguvu hizo ninazo na Inshallah Mungu anijalie afya njema na kunipa umri mrefu," anasema.
Babi anasema mtihani aliyopewa na Mungu akiwa KMKM ulikuwa msaada mkubwa kwake wa kuwabaini watu wasiopenda maendeleo yake na hatimaye sasa anapumua baada ya kutua Malaysia.
Anasema kutua kwake Malaysia kumempa furaha na faraja kubwa kama afarijikavyo pale anapoona familia yake inavyompa sapoti muda wote katika kuhangaikia maisha kupitia soka.


Abdi Kassim alipokuwa akiichezea DT Long An ya Vietnam
USHAURI
Babi anasema soka ni mchezo unaohitaji ustahimilivu, kujituma na kujibidiisha kwa mazoezi na hata uwanjani ili mchezaji afike mbali, kitu ambacho kwake imekuwa ni kama kanuni na ndiyo maana yupo hapo alipo.
Anasema soka la Tanzania limejaa mizengwe na kukatishana tamaa, kitu anachotaka wachezaji wenzake kuwa makini nacho ili waweze kucheza kwa muda mrefu na kwa mafanikio.
"Baadhi ya watanzania wanapenda kukatisha tamaa wachezaji, ni vyema wachezaji wakalitambua hilo na kuviamini vipaji walivyonavyo ili wafike kule wanakokuota la sivyo wanaweza kuacha soka mapema wangali wana uwezo."
Babi analitaja pambano la Tanzania na Algeria aliyofunga bao 'tamu' lililoipa  Stars sare ugenini kuwa ndiyo mechi isiyofutika kichwani mwake kwa namna ilivyokuwa ngumu na ukali wa bao lake lililokuwa gumzo.


Abdi Kassim akiitumikia timu ya taifa, Taifa Stars
KIPAJI
Abdi Kassim, alizaliwa Oktoba 19, 1986 visiwani Zanzibar akiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto nane wa Mzee Kassim Abdul yenye watoto wawili wa kike na sita wa kiume.
Kisoka alianza kucheza tangu wakati akisoma Shule ya Msingi Haile Sellasie, visiwani Zanzibar akitamani kuwa nyota kama baba yake aliyetamba visiwani humo katika soka.
Klabu yake ya kwanza ilikuwa Medisan aliyoichezea akiwa darasa la nne ikishiriki Ligi Daraja la Tatu visiwani humo kabla ya kutua Vikokotoni ikicheza daraja la pili na kusajiliwa Mlandege akisoma Sekondari ya Kisiwandui.
Akiwa Mlandege aliitwa timu ya Taifa ya Zanzibar akiwa na miaka 15 tu kabla ya kutua ile ya wakubwa na baadaye Taifa Stars iliyokuwa chini ya kocha Syllersaid Mziray na kuichezea chini ya makocha tofauti hadi mapema mwaka huu.
Baada ya kung'ara Mlandege, Babi alienda Falme za Kiarabu kucheza soka la kulipwa Nadisul FC mwaka 2003, aliporejea 2004 alijiunga na Mtibwa Sugar aliokaa nao hadi 2007 alipohamia Yanga.
Aliichezea Yanga akiwa kama nahodha kwa kipindi tofauti na kutwaa nao mataji kadhaa kabla ya mwaka 2010 alipoenda Vietnam kucheza soka la kulipwa.
Aliporejea mwaka juzi na kujiunga na Azam aliyoichezea hadi msimu uliopita na msimu huu kutua KMKM na kuichezea kwa muda.
Babi ni mume wa Aisha Yusuph aliyebahatika kuzaa naye watoto watatu, Zaliha na mapacha Zulfati na Abdul, pia hupenda kuangalia filamu za kihindi na kusikiliza muziki wa taarabu akiwa pia ni mtu wa swala tano.


Abdi Kassim alipokuwa Yanhga kama nahodha akiteta jambo na aliyekuwa kocha wao, Kostadin Papic
WASIFU WAKE:
Jina: Abdi Kassim 'Babi'
Kuzaliwa: Oktoba 19, 1986
Mahali: Jang'ombe, Zanzibar
Klabu alizochezea:
Medisan- 1994/95
Vikokotoni- 1995/98
Mlandege-   1999/03
Nadisul- 2003-04
Mtibwa Sugar- 2004/07
Yanga-  2007/10
DT Long-   2010/11
Azam- 2011/2013
KMKM- 2013
UiTM- 2013
Taifa- Tanzania

No comments:

Post a Comment