STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 23, 2013

Yanga 'waukubali' muziki wa Simba

 
Picha zote kwa hisani wa Lenzi ya Michezo
KOCHA msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro, amesema wachezaji wa timu yake hawakuwajibika na hawakufuata maelekezo ndiyo maana wakachezea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Simba juzi walipokutana katika mechi ya kirafiki ya 'Nani Mtani Jembe' iliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Minziro, alisema Kikosi cha Yanga kilizidiwa na watani zao Simba kutokana na kila mchezaji kutumia kipaji chake na si kucheza kitimu.
Minziro alisema hali hiyo ndiyo iliwaangusha na kuwapa nafasi wapinzani wao kutawala mchezo.
Alisema wameshauona upungufu huo na sasa watajipanga ili kurekebisha makosa kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
"Wachezaji hawakuwajibika ipasavyo na hawakufuata maelekezo tuliyokuwa tunawapa kila mara, imetuuma sana, tuna timu bora na hatukupaswa kupoteza mechi," alisema Minziro.
Hata hivyo, kipa aliyesimama langoni juzi, Juma Kaseja, hakuwa tayari kuzungumza lolote kuhusiana na matokeo hayo.
Kaseja aliyerejea Yanga kwa mara ya pili, juzi ilikuwa ni mechi yake ya kwanza kuichezea timu yake hiyo mpya baada ya kusajiliwa katika dirisha dogo msimu huu huku akiwa amekaa bila timu tangu Julai Mosi mwaka huu.
Baada ya matokeo hayo, uongozi wa Yanga jana, ulisema utajipanga upya kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na kwamba wanajiandaa na safari ya kwenda nje ya nchi kuweka kambi ili kuweza kuutetea ubingwa wao na kujiandaa na mashindano ya kimataifa.
Klabu hiyo imesema pia bado inaheshimu na inathamini uwezo wa Kaseja licha ya kufungwa mabao matatu jana.
Katika hatu nyingine, Kamati ya Utendaji ya Yanga imesema haikumsajili kipa Juma Kaseja kwa ajili ya kuwafunga 'Wanamsimbazi' huku ikiwapongeza wapinzani zao kwa kucheza soka la kuvutia lililostahili kupata ushindi.
Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Frank Sanga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, alisema jijini Dar es Salaam jana, hawakumsajili kipa huyo kuwafunga na kuwakomoa Simba, bali wamemsajili awasaidie kwenye michuano ya kimataifa.
Kamati ya Utendaji ya Yanga ilikuwa inamjibu Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali aliyeushutumu uongozi kwa madai kwamba kumsajili  Kaseja ni makosa makubwa.
Akilimali alikakaririwa usiku wa kuamkia jana akiporomosha maneno makali dhidi ya kipa huyo na uongozi akisema: "mabao mawili kipa wetu (Kaseja) ametoa zawadi. Si mabao ya kufungwa kipa mwenye weledi kama yeye. Nafikiri uongozi ulipaswa kumsajili Ivo Mapunda badala ya Kaseja."
“Huyu mzee (Akilimali) nadhani umri umemzidi, lakini nataka nimkumbushe, huyo Ivo Mapunda aliondoka Yanga akiwa anatumikia adhabu ya kufungiwa miezi sita na uongozi wa wakati huo kwa tuhuma za kufungisha kwenye mechi zetu (Yanga) dhidi ya Simba," alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaii ya Yanga ambaye alikuwa amefuatana na Sanga.
“Lakini pia nataka nimuulize, wakati Simba inarudisha mabao yote matatu Kaseja alikuwapo langoni? Nadhani hivi vitu si vizuri, tuache kulaumiana tushikamane kwa mustakabali mzuri wa timu,” alisema mjumbe huyo.
Sanga, alisema wanaheshimu uwezo wa Kaseja kwa sababu ndiye kipa aliyedaka mechi nyingi za mashindano ya Afrika kati ya makipa wote nchini, hivyo thamani yake haitashuka kwa kufungwa mabao matatu juzi.
Aidha, Kamati ya Utendaji ilisema mechi ya juzi haikuwa na uzito wowote kwao na ilikuwa sawa na bonanza au fete (michezo ya kubahatisha), hivyo hata kufungwa hakujawaumiza.
“Tuliamua kucheza kumfurahisha  mdhamini, TBL. Tumefungwa lakini bado tunaongoza ligi, hatujapoteza pointi hata moja, ile ilikuwa fete tu,” alisema Sanga ambaye pia alikuwa amefuatana na Katibu Mkuu mpya wa klabu hiyo, Beno Njovu.
Kiongozi huyo aliendelea kueleza kuwa Simba walicheza vizuri zaidi ya Yanga juzi na walistahili ushindi, hivyo anawapongeza kwa hilo, pamoja na wadhamini, TBL kwa kuandaa mechi hiyo ya aina yake.
Sanga alisema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Vodacom Tanzania Bara na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika wataimarisha benchi la ufundi na kuboresha timu, huku kukiwa na taarifa zinazodai kwamba kocha Ernie Brandts yuko hatarini kutimuliwa.
Alisema timu itaenda tena kambini Ulaya ili kufufua makali yao kama walivyofanya mapema mwaka huu walipoweka kambi kwenye Hoteli ya Fame Residence iliyopo katika mji wa matanuzi wa Antalya nchini Uturuki.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment