STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 1, 2014

Nani kuwa bingwa wa CHAN 2014

http://www.cafonline.com/userfiles/image/amr%20el%20sadek/trophy1234.jpg
BINGWA mpya wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2014 anatarajiwa kufahamika leo wakati Libya itakapopepetana na Ghana katika mchezo wa fainali utakaochezwa usiku, ukitanguliwa na pambano la kusaka mshindi wa tatu kati ya Nigeria dhidi ya Zimbabwe.
Ghana na Libya zinakutana katika pambano hilo la fainali baada ya kufuzu kwa mikwaju ya penati dhidi ya wapinzani wao hao, Ghana ikiishinda Nigeria mikwaju 4-1 na Libya ikiiacha solemba Zimbabwe kwa penati 5-4.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu za nchi hizo kukutana katika mchezo wa fainali tangu mwaka 1982 na wengi wamekuwa wakitabiria Ghana kunyakua taji hilo ambalo lilikuwa likishikiliwa na Tunisia iliyotwaa mara ya mwisho mwaka juzi.
Hata hivyo timu hizo zilishakutana katika michuano hiyo ya CHAN zikiwa kundi moja na matokeo yalikuwa sare ya 1-1 na hivyo kuwa vigumu kutabiri timu gani itakayoibuka na ushindi.
Kocha wa Ghana, James Kwasi Appiah, amenukuliwa akisema amewaandaa vijana wake kupata ushindi na kutwaa taji hilo baada ya kushindwa kufanya hivyo mwaka wa kwanza wa michuano hiyo walipofungwa na DR Congo.
Hata hivyo alisema hofu yake ni hali ya hewa iliyokuwa Cape Town akiamini inaweza kuwaathiri kwa vile mechi zao zote walizicheza katika mji wa Bloemfontain.
Ghana ni kati ya timu tatu ambazo zimeshiriki fainali za michuano hiyo mfululizo tangu ilipoanzishwa mwaka 2008, ikiwa sambamba na DR Congo waliotwaa ubingwa wa kwanza mwaka 2009 na Zimbabwe.
Libya inayonolewa na kocha kutoa Hispania inataka kuweka rekodi ya kunyakua taji hilo baada ya kushinda mechi zake mbili za Robo fainali na Nusu Fainali kwa mikwaju ya penati ikiipania kuizima Ghana katika muda wa kawaida.
Licha ya mbio za kuwania ubingwa pia leo kutakuwa na hitimisho ya kujua nani ni mfungaji bora wa michuano hiyo ambapo Mnigeria, Ejike Uzoenyi mwenye mabao manne sawa na Bernard Parker wa Afrika Kusini ana nafasi ya kutwaa kiatu cha dhahabu kwa vile mwenzake timu yake imeshatolewa.
Hata hivyo Mnigeria huyo anakabiliwa na upinzani toka kwa Mlibya, Abdulsalam Faraj Omar mwenye mabao matatu ambapo kama akifunga katika fainali dhidi ya Ghana anaweza kuwapiku wenzake.
Abdulsalama hayupo pekee yake katika orodha ya wenye mabao matatu kwani wamo pia Mnigeria Rabiu Ali na Mganda Yunus Sentamu ambaye tayari timu yake ilishafungashwa virago hatua ya makundi.

No comments:

Post a Comment