STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 8, 2014

Huyu ndiye kocha mpya wa Taifa Stars


Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
KOCHA mpya wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ni Martinus Ignatius ‘Mart’ Nooij ambaye anatarajiwa kutambulishwa rasmi Machi 24 mwaka huu na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi.
Tangu TFF kusema inatafuta kocha mpya atakayerithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen, BIN ZUBEIRY imekuwa ikifuatilia kwa undani mwalimu mpya wa Stars atakuwa nani na sasa inaibuka na jibu ni Mart Nooij.
Tayari Nooij ambaye kwa sasa ni kocha wa St George ya Ethiopia amekwishasaini Mkataba wa miaka miwili na TFF na atakuja nchini mwishoni mwa mwezi huu.
Atatutoa?; Kocha mpya wa Taifa Stars Mart Nooij anatarajiwa kutua nchini mwishoni mwa mwezi huu

Ulikuwa mchakato makini, uliohusisha wataalamu na washauri wa kimataifa juu ya masuala ya ufundi ya soka ambao umefanikisha kupatikana mwalimu huyo wa Kiholanzi aliyezaliwa Julai 3, mwaka 1954 mjini Beverwijk, Uholanzi.
Nooij amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12.
Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya  AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kunyakuliwa na St George ya Ethiopia anakoendelea na kazi hadi sasa.
Baada ya kusaini Mkataba wa miaka miwili na TFF kuja kuifundisha Stars, Nooij anasubiri barua maalum ya kuruhusiwa kuondoka baada ya kukamilisha taratibu za kuvunja Mkataba uliokuwa unaelekea ukingoni na klabu hiyo ya Addis Ababa.
Yanga SC pia inafundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm.
Chanzo: Bin Zubeiry

No comments:

Post a Comment