Suleiman Msuya
WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Magufuli amewataka
wahandisi kujenga ushirikiano ili kuhakikisha kuwa wanafanikiwa katika kupata
miradi mbalimbali ya ujenzi ambayo inatolewa na Serikali.
Magufuli ametoa rai wakati akifunga Mkutano wa Mwaka
wa Bodi ya Wasajili ya Wahandisi (ERB) uliofanyika jana katika ukumbi wa Mlimani City
Jijini Dar es Salaam.
Alisema ni vema wahandisi wote ambao wamepata
usajili baada ya kula kiapo kuwa na umoja ili kuhakikisha kuwa miradi
inayotolewa na serikali wanaipata kwa kutokufanya hivyo kutachangia kuikosa.
Katika mkutano huo zaidi ya wahandisi 250, wataalamu
na washauri waliapa katika mkutano huo ikiwa ni baada ya kupata usajili kupitia
ERB.
Waziri Magufuli alisema Serikali inaangalia
uwezekano wa kuhakikisha kuwa fedha zote ambazo zinapatikana katika mfuko wa
barabara zinatumika kwa kuwapatia wahandisi wa ndani ambao watapata miradi.
“Napenda kutumia nafasi hii ya kufunga mkutano huu
kwa kuwaomba muungane katika baadhi ya miradi ambayo inatangazwa na serikali
kama wenzenu wanaofanya kule katika daraja la Mmbutu Igunga Tabora ambao
umeonyesha mafanikio makubwa”,alisema.
Dk. Magufuli alisema Wizara yake itaendelea kutoa
ushirikiano wa aina yoyote ili kuhakikisha kuwa wahandisi wa Kitanzania
wanafaidika na kodi zao kwa kupata zabuni ambazo watakuwa na sifa nazo.
Kwa upande wake Msajili wa (ERB) Mhandisi Stephen
Mlote alisema kwa sasa jumla ya wahandisi wataalamu na washauri 13826
wamesajiliwa na makapuni 261pamoja na kula kiapo cha kazi hiyo.
Mlote alisema pia hadi kufikia sasa jumla ya
wahadisi 330 wamefutiwa usajili pamoja na kampuni 32 ambazo zimeonekana kukiuka
kanuni za ERB na kiapo walichoapa.
Alisema pamoja na idadi hiyo bado nchi ina kabiliwa
na uchache wa wahandisi wataalamu na washauri ambapo kwa sasa ni sawa na 0.2 asilimia
ya watanzania wote hali ambayo ni kinyume na nchi zilizoendelea.
Alitolea mfano nchi ya Australia ambayo ni
asilimia0.4, Malaysia 0.13, Uingereza 0.8 na Japani ni asilimia 1 hivyo juhudi
zinahitajika zaidi ili kuakukisha kuwa vijana wengi wanahamasishwa kusoma
masomo ya sayansi.
Msajili huyo alisema ERB pia inajitahidi kuwatafutia
vijana waliosoma fani ya uhandisi ajira ambapo hivi karibuni vijana 448
wameajiriwa katika taasisi mbalimbali hapa nchini.
Aidha Mlote alisema changamoto nyingine ni wahandisi
kukimbia fani hiyo na kujihusisha na fani nyingine kwasababu ya kufuata maslahi
mazuri ambayo yanapatikana katika sekta zingine.
Changamoto nyingine ni kuwepo kwa utamaduni wa
watanzania walio wengi kutotaka kutumia wahandisi katika ujenzi jambo ambalo
linawakatisha tama wahandisi kwani wajenzi hutumia mafundi wamitaani.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ( ERB) Profesa Ninatubu
Lema aliwataka wahandisi kuzingatia misingi ya kazi yao ili wawe watu wenye
kuchangia uchumi wan chi kwa kazi ambazo wanazifanya.
Lema aliwataka kuzingatia mambo yafuatayo ambayo ni
kuchagua, kupanga, kipaumbele, kutekeleza, kufuatilia na kutathimini wakati
wanatekeleza miradi mbalimbali ya hapa nchini ili kufikia lengo la Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).
No comments:
Post a Comment