STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 1, 2013

Nadhipa na wenzake wa Isidingo kupanda Mlima Kilimanjaro





















WASICHANA wadogo 14 kutoka nchini Nepal, Afrika Kusini na Tanzania, akiwemo muigizaji maarufu kwenye filamu ya Isidingo wameanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro kupitia lango la Machame.
Kati ya wasichana hao saba wanatoka Nepal na wamewahi kupanda mlima Evarest ulioko nchini Nepal, watatu kutoka Tanzania na Balozi wa Mpango
wa Chakula Ulimwenguni (WFP) nchini Afrika Kusini, Hlubi Mboya maafuru kama Nandipa kwenye filamu ya Isidingo.
Mratibu wa WFP nchini Tanzania, Richard Regani, alisema katika nchi za Afrika na Asia, wasichana wadogo wanakutana na vikwazo vingi katika kupata elimu, ndoa za utotoni, mimba, fedha za kulipa shuleni na kazi
nyingi za nyumbani.
Alisema lengo la la safari hiyo ni  kuionyesha jamii kuwa wasichana wadogo wanaweza na wanastahili kupata huduma muhimu za kijamii bila kubaguliwa ili kuweza kujenga jamii yenye maendeleo endelevu.

Simba yaenda Angola na matumaini kibao

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika Simba


KIKOSI cha wawakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, Simba wameondoka alfajiri ya leo kuelekea Angola kucheza mechi yao ya marudiano ya  michuano hiyo dhidi ya Recreativo de Libolo huku wakiahidi ushindi.

Simba imetamba kwamba licha ya kuwa nyuma kwa bao 1-0 iliyofungwa nyumbani, bado wanaamini wanaweza kurejea historia waliyowahi kuifanya mwaka 1979 na 2003 katika michuano hiyo.
Katika michuano ya mwaka 1979 Simba ililala nyumbani bao 4-0 na Mufulira Wanderers kabla ya kwenda kuwafumua wapinzani wao hao kutoka Zambia kwa mabao 5-0 na kusonga mbele.
Pia mwaka 2003 ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi wa Afrika Zamalek na kwenda kuing'oa nyumbani kwao kwa mikwaju ya penati baada ya kulazwa 1-0 nchini Misri.
Nahodha wa Simba, Juma Kaseja alilsema jijini jana kuwa anaamini timu yao itapata ushindi ugenini kama ilivyotokea kwa wapinzani wao kupata matokeo mazuri nchini.Kaseja alisema kuwa baada ya matokeo mabaya katika mechi za ligi, wachezaji wamebadili mawazo na kuahidi kupigana katika mchezo huo wa kimataifa ili kurejesha amani ndani ya klabu yao.
"Ni mechi ngumu lakini tukumbuke Simba mara kadhaa imefanya maajabu ikiwa ugenini, tutajituma na tunaomba sala zenu ziwe pamoja nasi katika vita hii ya kusonga mbele," alisema Kaseja ambaye ndiye nyota pekee aliyebaki kwenye timu hiyo ambayo mwaka 2003 iliivua ubingwa wa Afrika, Zamalek jijini Cairo, Misri.
Kocha wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig, naye alisema kuwa hakuna mechi rahisi na yeye alichokifanya ni kuwaandaa wachezaji wake kwa dakika 90 zilizobakia.
Liewig alieleza kuwa kufanya vibaya katika mechi za ligi kumechangia kushusha morali ya wachezaji wake lakini Jumapili watashuka dimbani wakiwa na malengo ya kusonga mbele.
Wachezaji walioondoka ni Kaseja, Abel Dhaira, Nassor Masoud "Chollo", Amir Maftah, Komalbil Keita, Juma Nyoso, Shomari Kapombe, Salim Kinje, Ramadhani Chombo 'Redondo', Amri Kiemba, Haruna Moshi 'Boban', Kiggi Makasi, Abdallah Seseme, Haruna Chanongo, Mrisho Ngassa, Felix Sunzu na Abdallah Juma huku kiongozi wa msafara akiwa ni Zacharia Hans Poppe na Muhsin Balhabou (mjumbe kamati ya utendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania-TFF).
Mechi kati ya Simba na Libolo itachezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Calulo uliopo katika mji wa Calulo, Angola.

MICHUANO YA MPINGA CUP YAANZA RASMI 


 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Seleman Kova akidaka mpira ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa michuano ya Mpinga Cup inayowahusisha waendesha pikipiki maarufu kama Bodabado iliyoanza rasmi jana kwa muda wa wiki moja. Mpinga cup imedhaminiwa na  Airtel , Rotary Club, Mr price na Shoprite  ikiwa na lengo la kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki na kupunguza ajali barabarani . akishuhudia kushoto ni  Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani  SACP. Mohamed Mpinga
 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Seleman Kova akikagua timu wakati wa uzinduzi wa  michuano ya Mpinga Cup inayowahusisha waendesha pikipiki maarufu kama Bodabado iliyoanza rasmi jana kwa muda wa wiki moja. Michuano hii imeanza rasmi kwa mechi kati ya Kawe Tiptop na Manzese anayefata pichani ni Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani  SACP. Mohamed Mpinga
 kikosi cha timu ya Manzese  katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa mashindano ya mpinga Cup yaliyofanyika jana katika viwanja vya polisi oyesterbay , katikati pichani ni Kanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es Saalam Suleiman Kova akifatiwa na Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani  SACP. Mohamed Mpinga
 kikosi cha timu ya Kawe Tiptop katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa mashindano ya mpinga Cup yaliyofanyika jana katika viwanja vya polisi oyesterbay , katikati pichani ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Seleman Kova akifatiwa na Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani  SACP. Mohamed Mpinga
 Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani  SACP. Mohamed Mpinga akikagua timu kabla ya mechi kati ya  Kawe Tiptop na Manzese jana wakati wa uzinduzi wa michuano ya Mpinga Cup, anayefata pichani ni Meneja Uhusiano wa Airtel Jackson Mmbando
Kanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es Saalam Suleiman Kova akijiandaa kudaka mpira ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa michuano ya Mpinga Cup inayowahusisha waendesha pikipiki maarufu kama Bodabado iliyoanza rasmi jana kwa muda wa wiki moja. Mpinga cup imedhaminiwa na  Airtel , Rotary Club, Mr price na Shoprite  ikiwa na lengo la kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki na kupunguza ajali barabarani . akishuhudia kushoto ni  Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani  SACP. Mohamed Mpinga

Thursday, February 28, 2013

NI FAINALI YA WANA MADRID WATUPU KOMBE LA MFALME HISPANIA

Ramidel Falcao akiwajibika uwanjani kuipeleka Atletico Madrid fainali ya Kombe la Mfalme kuvaana na mahasimu wao Real Madrid
MAHASIMU wa jiji la Madrid, nchini Hispania, Real Madrid na Atletico Madrid zitatarajiwa kuumana kwenye pambano la fainali za michuano ya Kombe la Mfalme litakalochezwa Mei 18 mwaka huu.
Atletico Madrid iliifuata Real Madrid kwenye fainali baada ya usiku wa kuamkia leo kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Sevilla katika mechi ya marudiano ya hatua ya nusu fainali iliyochezwa ugenini.
Mabao ya haraka ya kipindi cha kwanza kutoka kwa nyota wake, Diego Costa na Falcao yalitosha kuivusha Atletico hadi fainali kuwakabili Real iliyoitoa nishai Barcelona juzi usiku kwa kuisasambua mabao 3-1.
WEnyeji walipata bao la kwanza dakika ya 39 lililofungwa na Jesus Navas na kufanya matokeo ya mchezo huo wa jana kusomeka 2-1 wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili wenyeji kilianza kwa kasi na wenyeji walijikuta wakipoteza wachezaji wake wawili kabla ya kusawazisha bao dakika za lala salama na kuepuka aibu ya kulala nyumbani.
Sevilla ilimpoteza Medel dakika ya 76 kabla ya kufuatiwa na Kondogbia aliyeonyeshwa kadi ya pili ya njano dakika moja baada ya kusaidia kupatikana kwa bao la kusawazishwa lililofungwa na Rakitic dakika za nyongeza za pambano hilo.
Mashabiki wa soka wanasubiri kwa hamu pambano hilo la fainali, licha ya Real Madrid inayonolewa na kocha Jose Madrid ikipewa nafasi kubwa ya kujifariji kwa kutwaa taji hilo baada ya kuonekana wazi ni vigumu kutetea taji la Ligi Kuu ya nchi hiyo.