








---
Baadhi
ya wasanii, wabunge na wanamasumbwi watakaoshiriki katika Tamasha la
Usiku wa Matumaini 2013, leo walikusanyika katika mkutano wao na
wanahabari uliofanyika katika Hoteli ya The Atriums iliyopo Sinza jijini
Dar na kuelezea jinsi walivyojipanga kuelekea katika tamasha hilo kubwa
ambalo litafanyika Julai 7, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam. Katika tamasha hilo, wabunge wa Simba na wale wa Yanga
watashuka dimbani kucheza soka huku baadhi yao wakishiriki katika
mapambano ya ndondi dhidi ya waigizaji. Kwenye eneo la ndondi, Mhe.
Halima Mdee atapigana na Jacqueline Wolper, Mhe. Zitto Kabwe na Vincent
Kigosi ‘Ray’, Mhe. Ester Bulaya atavaana na Aunt Ezekiel huku balaa
zaidi likitarajia kuandikwa na mabondia Patrick Amote (Mkenya)
atakayevaana na Thomas Mashali (Mtanzania) huku Mkenya Shadrack Muchanje
akipigana na Francis Miyeyusho (Mtanzania). Burudani nyingine
zitakazokuwepo siku hiyo ni wakali wa muziki, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na
Prezzo, ambao watashindana katika jukwaa moja ili kutafuta nani mkali
zaidi. Bendi za Msondo Ngoma, Mlimani Park ‘Sikinde’ na Jahazi
zitawaburudisha mashabiki wao. Vilevile, burudani nyingine itatoka kwa
wakali wa Temeke, Wanaume Family na Halisi, wataokata mapanga Taifa kwa
staili zao za kuvutia. Soka la kukata na shoka kati ya Bongo Movie na
Bongo Fleva litahakikisha linawapa raha mashabiki wa wasanii
watakaoingia uwanjani siku hiyo.GPL