 |
Javu wa tatu toka kushoto akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar |
 |
Jamaa nouma, Ona alivyuowaacha akina Himid katika pambano baina ya timu zao |
 |
Hapa akijifua katika timu ya taifa, Taifa Stars |
 |
Akiwajibika uwanjani na kikosi cha Stars |
 |
Akitokelezea kibrazamen akiwa home |
INGAWA anadai amefunga magoli mengi kiasi hakumbuki
idadi yake kamili, lakini Husseni Javu anasema mabao aliyowafunga Yanga
katika pambano la duru la kwanza la Ligi Kuu msimu uliopita ndiyo matamu
asiyoyasahau kwa urahisi.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Sept. 19,
mwaka jana, mshambuliaji huyo nyota wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars,
alifunga magoli mawili yaliyotosha kuipa Mtibwa ushindi wa mabao 3-0
dhidi ya Yanga na kusababisha aliyekuwa kocha wa timu hiyo ya Jangwani,
Tom Saintfied kutimuliwa klabuni hapo akiwa na siku 77 tu.
Javu
anasema kwa jinsi alivyoyafunga kiufundi na kuzima ngebe za wapinzani
wao waliotamba kushinda kabla ya pambano hilo ndiyo inayomfanya
asiyasahau.
"Kwa yeyote aliyeyaona atakubaliana
nami yalikuwa ya ufundi na kubwa zaidi ni kukata kilimilimi cha Yanga
kwa kuwalaza mabao 3-0 licha ya tambo zao kwamba wangetuchapa Jamhuri,"
anasema.
Javu shabiki mkubwa wa Manchester United na anayemhofia beki
wa zamani wa Simba aliyetua Coastal Union, Juma Nyosso anasema hata
hivyo pambano gumu kwake lisilofutika kichwani ni lile la Mtibwa na
Mgambo JKT.
Anasema anaikumbuka mechi hiyo ya duru la pili
lililochezwa Mkwakwani Tanga kwa sababu ya kuchezewa vibaya na beki
aliyekabana naye asiyemkumbuka jina kiasi cha kumtia hasira na kulimwa
kadi ya njano kabla ya kocha wake Mecky Mexime kumpumzisha ili
kumwepusha na kadi nyekundu.
"Sijawahi kukutana na mechi ngumu kama
ile ya Mgambo JKT hasa beki yake iliyokuwa inacheza kwa vurugu hadi
nikapewa kadi ya njano na kumfanya kocha anitoe nje,"anasema.
Anasema licha ya vurugu hizo anashukuru Mtibwa walishinda bao 1-0 kupitia Salvatory Mtebe.
YANGA
Javu
aliyeanza soka tangu akisoma Shule
ya Msingi Turiani-Kilimanjaro, Morogoro na chandimu akikipiga Mwembeni
Stars, amekuwa akitajwa kutua Yanga kwa msimu ujao, japo mwenyewe
ameziruka taarifa hizo.
Mkali huyo ambaye hajaoa japo ana mchumba na
watoto wawili kati ya watatu aliyokuwa nao baada ya mmoja kufariki,
anakiri Yanga na Simba zilishamfuata kumtaka ajiunge nazo, ila hajasaini
kokote.
"Sijasaini kokote kwani Simba na Yanga ziliponifuata
nilizieleza nina mkataba na Mtibwa hivyo wazungumze na viongozi ili
waafikiane," anasema.
Anadai tangu baada ya hapo hajajulishwa
chochote na kushangaa kudaiwa ameshamwaga wino Jangwani, huku
akizushiwa pia ni majeruhi wa kudumu.
"Taarifa hizi zinashangaza
wakati ni juzi tu tumemaliza ligi na kuichezea Mtibwa karibu mechi zote
sasa majeraha hayo yametoka wapi," anahoji.
Anadai taarifa hizo zimempa usumbufu kwa kocha na daktari wake wakidhani aliumia kwenye 'ndondo' wakati hazina ukweli.
Javu anayependa kula chakula kizuri kwa
afya na kunywa juisi , anasema kama Yanga na Mtibwa wamekubaliana juu yake, yeye hajajulishwa.
Hata
hivyo anasema kama Yanga imemtaka kweli wamalizane na uongozi wake
anaodai anauheshimu kwa kumtoa mbali kisoka tangu alipotua timu ya
vijana enzi za kocha anayemsifia 'King' Abdallah Kibadeni.
"Hakuna
asiyependa kuzichezea timu kubwa hivyo Yanga wakimalizana na Mtibwa nami
nikaridhishwa na masilahi sitakuwa na tatizo lolote, soka ni ajira
yangu na kokote nacheza,"anasema.
 |
Javu (kulia) akiwa na jamaa yake Bakar Seblungo 'Beka' |
TUZO
Hussein Omar Javu,
alizaliwa Februari 16, 1988 Turiani Morogoro akiwa mtoto wa pili kati ya
sita wa familia yao na alisoma Shule ya Msingi Turiani Kilimanjaro
kabla ya kubobea jumla katika soka.
Anasema wakati akiibuka katika
soka alikuwa akiitwa Hussein Masha, bila kujua sababu, ingawa
anamkumbuka nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi
kutamba na Pamba, Simba na Taifa Stars.
"Mtaani walikuwa wakiniita Masha, cha ajabu Masha alikuwa kiungo mimi
tangu utoto nacheza ushambuliaji ila nililizoea jina hilo,"anasema.
Anasema
wakati akiichezea chandimu aliumia tumboni na kumfanya baba yake amzuie
kucheza kwa miaka mitatu kabla ya kubembelezwa wadau wa soka kijijini
kwao wakiongozwa na Mzee Hamis Cheza na kurejea tena uwanjani.
"Kama
siyo Mzee Hamis sidhani kama ningecheza tena kwani baba hakutaka kusikia
habari za soka akihofia ningeumia tena, niliporuhusiwa nilijiunga
Kingstone." anasema.
Mkali huyo anayeitaka serikali kuwekeza katika
soka la vijana kwa kuboresha shule za michezo hasa kuzisaidia 'academia'
zilizopo ili kuibua na kukuza vipaji, anasema baada ya kuichezea
Kingstone katika Ligi Daraja la Tatu alihamia kwa mahasimu wao Docks na
kuongeza uhamasa mkubwa mpaka sasa.
Alipokuwa Docks alifuatwa na
Alphonce Modest kumshawishi ajiunge Mtibwa iliyokuwa ikisaka vijana wa
kuunda timu ya vijana ambapo hata hivyo alikataliwa kabla ya Kibadeni
kumkingia kifua na kumbakisha
akishajiliwa mwaka 2007.
Akiwa na timu ya vijana walishiriki
michuano ya Uhai na kufanikiwa kuibuka Mfungaji Bora akiifungia timu
yake iliyomaliza nafasi ya tatu jumla ya mabao 7.
Javu anasema kabla
ya tuzo hiyo alishanyakua tuzo nyingine kama hiyo katika michuano kadhaa
ya mchangani mjini Morogoro na ameendeleza moto wa mabao hata
alipopandishwa timu ya wakubwa ya Mtibwa aliyonayo mpaka sasa.
Anasema
japo hajapata mafanikio makubwa katika soka, anashukuru amenunua
kiwanja, kutwaa tuzo na mataji kadhaa kama ya Tusker na Mapinduzi akiwa
na Mtibwa mbali na kumudu maisha na familia yake.
Ndoto za Javu ni
kucheza soka la kulipwa na anasema analizwa na kifo cha mwanae huku
akiwataja King Kibadeni, wazazi wake, rafikie Bakari Seblungo na kaka
yake Mrisho Javu kama waliomsaidia kufika alipo.
Javu anayewataka
wachezaji wenzake kupendana na kuzingatia nidhamu anadai anaimani kubwa
Stars kufuzu fainali za CHAN kwa mara ya pili baada ya zile
za mwaka 2009.