STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, January 6, 2014

Boti ya Kilimanjaro yaua 6,. miili yatambuliwa


WATU kumi wamefariki dunia katika ajali mbili tofauti  katika Bahari ya Hindi.
Katika ajali ya kwanza, watu sita walifariki baada ya boti ya Kilimanjaro II ilipokumbwa na dhuruba kali katika mkondo wa Nungwi, Zanzibar wakati ikitokea Pemba kwenda kisiwani Unguja jana asubuhi.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Riziki Juma, alisema jana jioni kuwa maiti sita zilipatikana na kwamba abiria watatu waliokolewa wakiwa hai huku uokoaji ukiendelea.
Awali, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yusuph Ilembo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa kazi ya kuwatafuta watu wanaohofiwa kupotea imeanza kufanywa na mabaharia kwa kushirikiana na wananchi.
Alisema boti hiyo ilipofika katika mkondo wa Nungwi ilipigwa na wimbi moja kubwa na injini kuzimika na watu waliokuwa wamekaa juu wakiwamo watoto waliteleza na kuhofiwa kutumbukia ndani ya bahari.
Alisema kuwa boti hiyo baada ya injini zake kuzimika ilibakia ikielea baharini na kwamba Nahodha wake alifanikiwa kuziwasha tena na kuendelea na safari na abiria waliobakia walifika salama.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar Maalim, alisema wazamiaji waliondoka jana mchana kuungana na baadhi ya wananchi huko Nungwi kufanya kazi ya kutafuta watu wanaohofia kupotea baada ya ajali hiyo.
Hata hivyo, alisema ZMA itatoa taarifa baada ya kukamilika uhakiki wa majina ya abiria kwa meli zote zilizosafiri jana kutoka kisiwani Pemba pamoja na wazamiaji kufika katika eneo la tukio na kufanya kazi ya kutafuta watu hao.
Hata hivyo, wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Khalfan Mohamed Mshangi, alisema baadaye kuwa zimepatikana maiti tano na tatu zimetambuliwa.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Akram Khamis issa (11), mkazi wa Mwanakwerekwe; Masoud Hamad Abdallah (30), mkazi wa Wete na Nashra Khamis (9), mkazi wa Mombasa, Zanzibar.
Aliongeza kuwa boti hiyo ilikuwa na abiria 396 wakiwamo watoto 60 na kwamba abiria ambao hawajapatikana ni 18.
Baadhi ya mashuhuda waliohojiwa  walisema mkasa huo ulitokea sasa 2:30 asubuhi wakati boti hiyo ilipofika eneo la Nungwi na kupigwa wimbi kali na kuelemea upande mmoja.
Suleiman Muhammed Said, abiria katika boti hiyo, alisema baada ya boti hiyo kuelemea upande mmoja, baadhi ya watu walidondoka baharini pamoja na mizigo na kwamba boti iliendelea na safari baada ya kukaa sawa.
Alisema boti hiyo iliondoka Pemba majira ya saa 2:00 asubuhi na kwa mujibu wa  ratiba, boti ilitarajiwa kufika Unguja saa 4:00 asubuhi, lakini kutokana na hitilafu hiyo, ilifika saa 6:00 mchana.
Alisema boti ilipoondoka Pemba, hali ya bahari haikuwa nzuri na ilipofika Nungwi hali ya bahari ilizidi kuchafuka na boti kuyumba.
Alisema hadi boti inafika bandarini, ndugu zake wawili hawakuonekana pamoja na mizigo waliyokuwa  nayo katika boti hiyo.
“Nilikuwa na ndugu zangu wawili na mizigo, baada ya meli kutaka kuzama mizigo na baadhi ya watu walidondokea baharini, lakini meli ilipoibuka iliendelea na safari bila ya kuwatafuta,” alisema Suleiman huku akitokwa machozi.
Baadhi ya watu walifika bandarini Malindi waliangua vilio na sura zao kujaa na huzuni kutokana na kutowaona ndugu na jamaa zao.
Abdallah Mohammed Abdallah, aliyefika bandarini kumtafuta mtoto wake ambaye bado hakuwa na taarifa zake, alisema alipokea simu ya mtoto wake aliyekuwamo katika boti saa 2:30 asubuhi kuwa boti inazama.
“Nilipokea simu ya mtoto wangu, alikuwa akilia na kuniambia baba baba tunakufa, meli huku inazama, baada ya hapo simu yake ikawa haipatikani” alisema Abdallah.
Aidha alisema alifika bandarini kupata taarifa sahihi, lakini hakupewa jibu linaloridhisha kutokana na boti kufika bila kumuona mtoto wake.

Friday, January 3, 2014

Semera, Aisha Bui warejea Bongo Movie

Semera
Aisha Bui
WAKATI msanii Leah John 'Semera' akitangaza kurejea tena kwenye fani ya uigizaji baada ya kujiweka kando mwaka 2013, muigizaji mwingine nyota Aisha Fat'hi ak.a Aisha Bui amesema mashabiki wajiandae kumpokea upya.
Semera aliiambia MICHARAZO kuwa alikuwa kimya akifanya shughuli nyingine za kiuchumi na sasa amerejea upya akiwa mbioni 'kuuza sura' kupitia kazi ambayo hata hivyo hakuitaja jina.
"Nilikuwa kimya kwa sababu ya kutingwa na majukumu mengi, sasa nimerejea upya na mashabiki wangu wasubiri kuniona katika kazi mpya itakayotoka mapema mwezi huu," alisema.
Kabla ya kutoweka mwanadada huyo alifanya vyema kwenye filamu za 'Mateka wa Kiroho', 'Mateso Kama Haya', 'Uyoga', 'Chozi'  na nyingine.
Katika hatua nyingine muigizaji nyota, Aisha Bui aliyerejea nchini hivi karibuni baada ya kuwa Afrika Kusini kwa muda mrefu, amewataka mashabiki wa filamu kukaa tayari kumpokea akiwa amezaliwa upya.
Mwanadada huyo alisema anataka kuutumia mwaka 2014 kuwapa burudani mashabiki wake waliomkosa kwa muda mrefu akiwa nje ya Tanzania.
 Wakati huo huo nyota  wa muziki wa Hiphop, Emmanuel  Elibariki 'Ney wa Mitego' ameacha video ya wimbo wake mpya uitwao 'Nakula Ujana'.
Video hiyo tayari imekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii kutokana na kutazamwa na wengi tangu ilipoachiwa hewani na staa huyo wa vibao kama 'Muziki Gani', Salamu Zao' na nyingine ilirekodiwa hivi karibuni jijini Nairobi.

Mata aonyeshwa mlango wa kutoka darajani

Mourinho akiwa na Mata
 KOCHA Jose Mourinho amemwambia Juan Mata anaweza 'kuchapa mwendo' (kuondoka) Chelsea baada ya kukasirika alipofanyiwa 'sabu' dakika ya 53 katika mechi ya kwanza ya mwaka mpya dhidi Southampton kwenye Uwanja wa St Mary's.
Mata alimpuuza Mourinho wakati alipokuwa akitoka uwanjani na kisha kukataa kugonga siti za wachezaji wa akiba.
Katika mchezo huo alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Oscar, ambaye alionyeshwa kadi ya njano kutokana na 'kupiga mbizi' (kujirusha), na baada ya hapo kufunga bao wakati Chelsea ikishinda 3-0.
Mata amewahi kutwa tuzo ya mchezaji bora wa klabu katika misimu miwili iliyopita na alitajwa katika kikosi cha wachezaji wakulipwa cha msimu wa 2012/13.
Lakini sasa Mourinho amesema hawezi kumzuia Mhispania huyo kuondoka kama atataka kuchapa mwendo Stamford Bridge.
Mourinho, aliweka wazi kuhusu mchezaji huyo, kwa kusema: "Sitaki aondoke, hayo ndiyo maoni yangu na hilo ndilo ninalolitaka - lakini mlango wangu upo wazi.
"Mlango wa klabu upo wazi pia, hivyo kama mchezaji anataka kuzungumza na sisi tupo pale tunawasubiri. Lakini kama utaniluliza endapo ninata kumuuza, sihitaji pia.
"Sikuona alivyofanya, kutibuka kwake ni kwa sababu ya matokeo- tunahitaji kushinda.
"Kama hatukushinda mchezo huu, tofauti ya pointi kutoka timu inayoongoza ingekuwa kubwa. Mwishoni mwa mchezo kila mmoja akiwamo yeye walisherehekea ushindi."

Arsena majanga, Bendtner aongezeka wodi ya majeruhi Emirates

NICKLAS Bendtner anajiandaa kukaa nje ya uwanja kwa "wiki kadhaa" kutokana na majeraha ya 'enka' yanayowafanya vinara hao wa Ligi Ku ya England wakiwa na upungufu wa washambuliaji.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Denmark aliingia kutokea benchi na kufunga goli la kuongoza la Gunners katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Cardiff lakini akaumia 'enka' wakati akifunga goli hilo.
Mfungaji anayeongoza Olivier Giroud alikosa mechi hiyo kutokana na majeraha ya 'enka' pia.
"Inaonyesha tumepungukiwa," alisema kocha Arsene Wenger, huku dirisha la usajili likifunguliwa.
Hata hivyo, kocha huyo hakutaka kubainisha kama anawania kusajili mshambuliaji mwezi huu, licha ya Bendtner kutarajiwa kuwa nje katika mechi ya kesho ya Kombe la FA nyumbani dhidi ya Tottenham, na Giroud akiwa shakani zaidi.
Wenger alisema: "Yeye (Bendtner) aliumia enka, kwa muda gani atakuwa nje hatujui lakini inaonekana ni wiki kadhaa.
"Tunaye Lukas Podolski na Theo Walcott ambao wanaweza kucheza kama washambuliaji wa kati lakini kwa mipango ya muda mrefu tunahitaji mtaalamu wa nafasi hiyo ya kati.
"Kwa kuwapoteza wachezaji wawili ni ngumu. Msiwe na haraka sana kwa sasa, tunachosema ni kwamba tuna washambuliaji wawili ambao ni majeruhi."
Kuhusu Bendtner, Wenger alisema anaonekana kurejea kucheza vile anavyotaka hivyo anapenda kuendelea kuwa naye, lakini hatamzuia akitaka kuondoka.
Arsenal pia iliwakosa Aaron Ramsey (paja), Mesut Ozil (bega), Kieran Gibbs (kiazi cha mguu) na Tomas Rosicky (kiazi cha mguu).

Yanga wajipange kwa Ashanti Utd, yapigwa na Tusker lakini....!

IKIWA na uchovu wa safari, Ashanti United iliyochukua nafasi ya Yanga kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi usiku wa jana ilianza vibaya kwa kulazwa bao 1-0 na Tusker ya Kenya, lakini ikionyesha kuimarika zaidi.
Ashanti inayonolewa kwa sasa na kocha Abdallah Kibadeni 'King' ilitua jana asubuhi visiwani humo na kushuka dimba la Amaan usiku na kuionyesha kazi Tusker kabla ya kukubali bao 1-0 lililofungwa dakika ya 24 na Joshua Oyoo.
Kwa muziki iliyouonyesha Ashanti, ni wazi Yanga itakuwa na kazi kubwa katika mechi ya fungua dimba ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara inayoanza Januari 25.
Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo, Yanga iliisasambua Ashanti kwa mabao 5-1.
Michuano hiyo itaendelea tena jioni ya leo kwa michezo kadhaa ikiwemo la 'mnyama' Simba iliyoitafuna Leopards wa Kenya itashuka dimbani usiku kuwakabili watoza ushuru wa Uganda, URA.