STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 9, 2014

Steve Nyerere aomba kukutana na serikali, wasambazaji


MWENYEKITI mpya wa Bongo Movie Unity, Steven Mengele 'Steve Nyerere' ameiangukia serikali akiomba kukutana nao pamoja na wasambazaji wa kazi za wasanii ili kujadili mambo mbalimbali yanayowakabili.
Steve Nyerere alisema kwa muda mrefu wasanii wamekuwa wakinyonywa jasho lao na yeye kama kiongozi mwenye dhamana wa kuwasaidia wasanii wenzake ameona ni vyema kukutana na serikali na wasambazaji kuweka mambo sawa.
Alisema wasanii wamekuwa wakinyonywa katika jasho lao, na kumekuwa na juhudi kubwa za kuwasaidian wasanii, lakini bila mafanikio hivyo anaamini mkutano wake na serikali na wasambazaji utaleta jibu zuri.
"Baada ya kuchaguliwa na wasanii wenzangu, nimepanga kuanza kuomba kukutana na serikali na wasambazaji ili kuweza kumaliza kilio cha muda mrefu cha unyonyaji wanaofanyiwa wasanii," alisema.
Steve aliyechaguliwa mwishoni mwa wiki katika uchaguzi mkuu wa umoja huo, alisema ni Tanzania pekee ambayo msanii na mtayarishaji ndani ya mwaka anaweza kutengenezea filamu kuanzia 6 mpaka zaidi ya 10.
"Duniani kote mtayarishaji anaweza kutengeneza filamu kati ya moja mpaka mbili, lakini hapa msanii mmoja anazalisha filamu zaidi ya 10 kwa mwezi na kuuza kazi hiyo kati ya Sh. milioni 10-20, huu ni wizi," alisema.
Alisema ni vyema msanii akaweza kutengeneza filamu angalau moja kwa mwaka na kuiuza pengine hata kwa Sh. milioni 200 kuliko mtindo wa sasa ambao unawanufaisha wasambazaji wanaouziwa 'master' na kuzalisha filamu maradufu tofauti na fedha walizonunulia kazi hizo.
Alisema Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40, lakini alisema kwa mauzo ya hata nakala 10,000 tu kwa bei ya Sh.5,000 kwa nakala, muuzaji anapata Sh. milioni 50 hivyo si sawa kuwapa wasanii waliotoka jasho Sh. milioni 10 wakagawane.
Mwenyekiti huyo aliyechukua nafasi ya Vincent Kigosi 'Ray' aliyekuwa akiiongoza Bongo Movie kabla ya uchaguzi huo, alisema anaamini serikali ikiweka mikakati mizuri kuwabana wasambazaji wasanii watanufaika na kulipa kodi itakayosaidia kuleta maendeleo ya nchi kuliko ilivyo sasa.

Negredo apiga hat trick, Man City ikiigonga West Ham x6

MSHAMBULIAJI Alvaro Negredo usiku wa jana alifunga mabao matatu (hat trick) wakati Manchester City ikiisambaratisha West Ham United kwa mabao 6-0 katika pambano la Nusu Fainali ya Kombe la Ligi.
Negredo alifunga mabao hayo mawili kipindi cha kwanza katika dakika ya 12, 26 na la tatu kipindi cha pili kwenye dakika ya 49.
City waliokuwa uwanja wao wa nyumbani wa Etihad, walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3-0 bao la tatu lilifungwa na Yaya Toure dakika ya 40.
Kipindi cha pili mbali na bao la Negredo, Edin Dzeko aliongeza mengine mawili kwenye dakika za 60 na 89 na kuifanya City kunusa fainali za michuano hiyo.
Japo soka linadunda, lakini itakuwa kibarua kigumu kwa West Ham kuilaza City ikiwa nyumbani kwake Upton Park mabao 7-0 katika mechi ya mkondo wa pili wiki mbii zijazo.
Nusu fainali ya kwanza iliyochezwa juzi ilishuhudia Manchester United ikizabuliwa mabao 2-1 ugenini na Sunderland.
 

Wednesday, January 8, 2014

Azam haoo nusu fainali kuwavaa KCC

Azam
 MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Azam, ameendelea kuonyesha dhamira yao ya kutaka kutetea taji hilo baada ya leo kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Spice Cloves na kutinga Nusu Fainali ya michuano hiyo.
Ushindi huo uliotokana na mabao ya kipindi cha pili toka kwa  mabeki wao Agrey Morris na Waziri Salum yalitosha kuivusha Azam kwenye mechi ya roba fainali na sasa kusubiri kuvaana na KCC ya Uganda iliyoitoa Tusker ya Kenya kwa mikwaju ya penati.
Wakati Azam ikiwa tayari imeshajua itaumana na nani, wawakilishi wengine wa Tanzania, Simba usiku huu wapo dimbani kuvaana na wawakilishi ya Zanzibar kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Chuoni ili kutafuta nafasi ya kuvaana na URA ya Uganda iliyoiondosha Mabingwa wa Zanzibar, KMKM kwa bao 1-0.
Simba iliyotinga robo fainali kutoka kundi B kwa kujikusanyia pointi saba itahitaji ushindi ili kuweza kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo wowote chini ya kocha mpya, Dzavkov Logarusic.

Yanga yaomba radhi, yamwaga noti Mapinduzi Cup

Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
KLABU ya Yanga SC imeomba radhi kwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd kwa kitendo chao cha kujitoa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, sambamba na kutoa Sh. Milioni 10 kwa Kamati ya Mashindano hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga alikutana na Balozi Seif Ali Idd ofisini kwake eneo la Vuga, karibu na Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mazungumzo ya kuomba radhi.
Clement Sanga kushoto akiwa na Mwenyekiti wake, Yussuf Manji. Leo ametua Zanzibar kuomba radhi na kutoa Sh. Milioni 10 kwa Kamati ya Kombe la Mapinduzi 

Balozi Seif ameupokea msamaha huo na pamoja na hayo, Sanga aliahidi Yanga itakuja Zanzibar mwezi ujao kucheza mechi tatu za kirafiki na hawatachukua fedha za mapato ya milangoni, ili ziende kwenye mfuko wa Kombe la Mapinduzi.
Yanga SC ilijitoa kwenye Kombe la Mapinduzi kwa sababu haikuwa na benchi la Ufundi, baada ya kuwafukuza makocha wake wote, Mholanzi Ernie Brandts na wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Mkenya Razack Ssiwa, kufuatia kufungwa na mahasimu wao wa jadi, Simba SC mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe Desemba 21, mwaka jana.
Kwa sasa tayari Yanga SC imeajiri makocha wawii, Msaidizi Charles Boniface Mkwasa na kocha wa makipa Juma Nassor Pondamali, wakati mchakato wa kumsaka kocha mkuu wa kigeni unaendelea.
Msafara wa zaidi ya watu 32 wa Yanga SC unatarajiwa kuondoka kesho alfajiri kwenda Uturuki kwa kambi ya wiki mbili, kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga walitarajiwa kupata viza zao jioni ya leo na kesho watapanda ndege ya Uturuki (Turkish Airline) kwenda kwenye kambi ya mafunzo katika nchi hiyo ya Ulaya kwa mara ya pili mfululizo.  
Wachezaji wanaotarajiwa kuondoka na timu hiyo kesho ni makipa; Juma Kaseja, Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki David Luhende, Oscar Joshua, Juma Abdul, Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Job Ibrahim na Rajab Zahir.
Viungo ni Hassan Dilunga, Bakari Masoud, Hamisi Thabit, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Hamisi Kiiza, Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa, Said Bahanuzi, Shaaban Kondo, Didier Kavumbangu, Simon Msuva, Reliant Lusajo na Hussein Javu.
Viongozi ni makocha Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali, Daktari Juma Sufiani, Meneja Hafidh Saleh na Ofisa Habari, Baraka Kizuguto. 
Kunaweza kukawa na watu wengine katika msafara huo kutoka kwenye uongozi, lakini bado haijajulikana ni akina nani.
Wachezaji ambao wameachwa ni Athumani Iddi ‘Chuji’ aliyesimamishwa kwa utovu wa nidhamu, Salum Abdul Telela ambaye ni majeruhi na wachezaji waliopandishwa kutoka timu ya vijana, Issa Ngao, Yussuf Abdul na Abdallah Mguhi ‘Messi’.

Mashetani Wekundu wadundwa tena

Namanja Vidic akishangilia bao lake la kusawazisha la Man Utd ambalo hata hivyo halikusaidia kitu
MANCHESTER United imeendelea kuwa 'mdebwedo' chini ya kocha David Moyes baada ya usiku wa jana kulambishwa tena kipigo cha 2-1 na Sunderland katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Ligi.
Mashetani hao Wekundu walikumbana na kipigo hicho ugenini na kuzidi kumweka pabaya Moyes aliyeichukua timu hiyo toka mikononi mwa kocha aliyekuwa na mafanikio makubwa Old Trafford, Alex Ferguson.
Sunderland ikiwa kwenye uwanja wake wa Uwanja wa Light ilijikuta ikizawadiwa bao dakika za nyongeza baa da mkongwe Ryan Giggs kujifunga.
Kipindi cha pili kilianza kwa Manchester kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 52 kupitia kwa nahodha wake, Nimanja Vidic hata hivyo wenyeji waliwakata maini wageni wao baada ya Borini kufunga bao la ushindi kwenye dakika ya 65 kwa mkwaju wa penati.