STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 4, 2012

Bwana Misosi avunja ukimya na mpya

Bwana Misosi katika pozi

STAA wa kitambo wa muziki wa Bongofleva, ambaye kwa sasa amejitosa kwenye fani ya filamu, Joseph Rushahu 'Bwana Misosi', amevunja ukimya kwa kuachia wimbo mpya uitwao 'Iweje'.
Wimbo huo umefyatuliwa na Bwana Misosi, baada ya kipindi kirefu cha ukimya tangu mwaka jana alipoachia nyimbo mbili za 'Pilato na Game' alioimba na Sir Juma Nature na Fid Q na ule wa 'Mungu Yupo Bize'alioimba na Said Chigunda 'Chegge'.
Akizungumza na MICHARAZO, Bwana Misosi, alisema wimbo huo mpya ameurekodia studio za HM Records zilizopo Kawe na anatarajiwa kuachia hivi karibuni sambamba na video yake aliyoanza kuishuti.
"Kaka nimekamilisha 'ngoma' mpya iitwayo 'Iweje' ambayo nimekamua mwenyewe bila kupigwa tafu na mtu na kwa sasa nakamilisha mipango ya video kabla ya kuachia kwa pamoja itakapokamilika video hiyo," alisema Bwana Misosi.
Msanii huyo alisema wimbo huo kama zilizotanguliwa zitakuwa za kufanyia show tu na wala hana mpango wa kutoa albamu kama alivyofanya mwaka 2004 na 2007.
"Sina mpango wa kutoa albamu, natoa singo tu kuwapa burudani mashabiki wangu sawia na kupata nafasi ya kugonga shoo," alisema.
Aliongeza wakati akiendelea na mchakato wa kupakua video ya wimbo huo wa 'Iweje', pia anaendelea na zoezi la upigaji picha wa filamu mpya ya pili anayotarajiwa kuibuka nayo.
Bwana Misosi , aliyeingia kwenye fani hiyo akiwa na filamu ya 'Mkoba' ambayo ipo njiani kuachiwa mtaani ikiwa imeshirikisha wakali kama Amanda na Mzee Majuto, alisema filamu hiyo mpya ya pili ipo hatua ya mwisho kabla ya kukamilika.

Zuku Tv yazindua huduma mpya ya malipo kwa wateja wao

Meneja wa kampuni ya Wananchi Satellite Ltd, Fadhil Mwasyeba (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa huduma za malipo kwa wateja wao uliofanyika leos asubuhi jiji Dar es Salaam baada ya kampuni hiyo kuingia mkataba na kampuni ya Selcom Wireless Ltd. Anayeonekana kati ni Meneja Uhusiano wa Selcom, Juma Tumaini Mgori.



KAMPUNI ya Wananchi Satellite Ltd inayomiliki televisheni ya kulipia ya Zuku kikishirikiana na kampuni ya Selcom Wireless Ltd zimeingia mkataba wa kuanza kutoa huduma rahisi ya malipo kwa wateja wa televisheni hiyo kwa nchi nzima.
Uzinduzi wa huduma hizo ulifanyika leo jijini Dar es Salaam baada ya viongozi wa pande hizo mbili kusaini mkataba huo mbele ya waandishi wa habari katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond, uliopo  Ubungo.
Meneja wa Wananchi Satellite kwa hapa nchini, Fadhili Mwasyeba alisema wameamua kurahisisha huduma ili kuwapa fursa wateja wao kufanya malipo kwa njia nyepesi na ya haraka tofauti na siku za nyuma.
"Tuna furaha juu ya ushirikiano huo mpya na utakaowajali wateja wetu wa Zuku. Ahadi yetu ni kutoa ufumbuzi rahisi kwa wateja wetu wafanyabiashara na wauzaji na ufumbuzi huui utatuwezesha kufika mbali zaidi ya matarajio ya vwateja wetu." alisema.
Aidha Mwasyeba aliongeza kuwa wakati wakiwarahisishia unafuu wa kulipa malipo ya kila mwezi kwa wateja wao, pia kampuni yao inaendelea na promosheni yao ya kuwazawadia wateja wao iitwayo Zuku Tunakuthamini-Pata Tv Bure'.
Alisema kinachotakiwa kwa wateja kuwaunganisha wateja watano kujiunga na Zuku na kulipia malipo na kisha kujishindia runinga kati ya inchi 22 na wale watakaofikisha idadi ya wateja 10 watanyakua rungina ya inchi 42 na walioungwanishwa nao wakiambulia 'offer' nyingine zinazotolewa na kampuni yao kupitia promosheni hiyo.
Naye Meneja Uhusiano wa Selcom, Juma Tumaini Mgori, alisema kuanza kutoa huduma hiyo kwa wateja wa zuku ni fursa ya kuwapa unafuu wateja wa televisheni hiyo popote walipo nchini kutokana na kampuni yao kuwa na vituo vya malipo zaidi ya 1500.
"Tunajitahidi kufanya kazi kwa ufanisi kwa malipo ya ushirikiano wa kipekee na zuku ili kuwafikia wateja kwa ukaribu zaidi," alisema na kuongeza;
Tuna furaha kufanya kazi na Zuku na tunaamini huu ni mwanzo tu wa ushirikiano wa kibiashara," alisema.
Televisheni ya Zuku inatoa uchaguziu mpana wa stesheni za burudani ikiwa ni pamoja na habari, michezo na sinema, majarida na muziki ikiwa imejumuisha chaneli za kimataifa kama BBC, MTV Base. Sentanta Sports, MGM Movies na nyinginezo ka gharama nafuu kwa ubora na kiwango cha hali ya juu.
Mameneja wa kampuni za Wananchi Satellite Ltd, Fadhil Mwasyeba (kushoto) na Juma Tumaini Mgori wa Selcom Wireless wakibadilishana mkataba waliosaini leo ili kutoa huduma rahisi na ya haraka ya malipo kwa wateja wa Zuku Tv. Uzinduzi huo uliofanyika leo asubuhi jijini Dar es Salaam.

PICHA ZA TIMU ZA TAIFA ZA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR ZILIZOPOWEZA KUTINGA NUSU FAINALI ZA KLOMBE LA CHALENJI NCHINI UGANDA. (zote kwa hisani wa Bongostaz

Wachezaji wa Bara wakimpongeza Bocco baada ya kufunga bao la pili katika Robo Fainali ya kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge dhidi ya Rwanda. Bocco alishangilia huku akichechemea baada ya kufunfa bao hilo kutokana na kuumia, baada ya kugongwa na kipa wa Rwanda, Jean Claude Ndoli wakati anaenda kufunga. Bara ilishinda 2-0 na kutinga Nusu Fainali. 


Kaseja amedaka, huku Yondan akiwa tayari kumsaidia


Manahidha wakisalimiana kabla ya mechi, Juma Kaseja wa Bara kulia na Haruna Niyonzima wa Rwanda kushoto


Kikosi cha Rwanda leo


Kikosi cha Bara leo


Watanzania waliokuja kuisapoti timu hapa


Shomary Kapombe akimdhibiti Dadi Birori 


Athumani Iddi 'Chuji' akiruka juu kulia kuokoa


Amri Kiemba anamkokota mchezaji wa Rwanda


Kocha Milutin Sredojevic 'Micho'


John Bocco akiwashughulisha mabeki wa Rwanda


Refa anaonyesha kati, baada ya Kiemba anayekimbia nyuma yake kufunga bao la kwanza


Bao la Kiemba


Mwinyi Kazimoto kulia akimburuza mchezaji wa Rwanda


Ulinzi mkali langoni mwa Rwanda, lakini bado mbili zilipenya


Bocco anasababisha


Jean Claude Ndoli wa Rwanda aliyeruka hewani kudaka moja ya michomo ya hatari iliyoelekezwa langoni mwake


Saturday, December 1, 2012

Shamsa Ford, Mayasa warejea 'After Death'

Shamsa Ford


Mayasa Mrisho 'Maya' katika pozi kabambe

BAADA ya kitambo kirefu cha mapumziko ya uzazi, msanii Shamsa Ford amerejea upya kwa kasi katika fani ya uigizaji akitarajiwa kuonekana kwenye filamu ya 'After Death' akishirikiana na wazoefu Mayasa Mrisho, Ruth Suka 'Mainda' na Jacklyne Wolper.
Shamsa aliyekuwa mmoja wa waigizaji waliofanya kazi kwa karibu na marehemu Steven Kanumba ameshiriki filamu hiyo iliyotayarishwa na Jacklyne Wolper kama njia ya kumuenzi Kanumba aliyefariki Aprili 6 mwaka huu.
Muongozaji wa filamu hiyo inayotarajiwa kuzinduliwa mapema mwakani. Leah Richard 'Lamata' alisema filamu hiyo mpya imemrejesha upya Shamsa na kukumbushia 'umoja' wa wasanii hao waliokuwa wakishiriki kazi na marehemu Kanumba.
"Ndani ya filamu yetu ya 'After Death' ambaye ni maalum kwa ajili ya kumuenzi Kanumba imemrejesha upya Shamsa Ford, aliyeigiza na akina Mayasa Mrisho 'Maya', Mainda, Irene Paul, Wolper, Patcho Mwamba na Uncle D aliyeigiza kama Kanumba."
Lamata, mmoja wa waongozaji wachache wa filamu wa kike nchini, mbali na wakongwe hao pia filamu hiyo imewashirikisha 'watoto wa Kanumba' Jenifer na Patrick na wanajipanga kwa ajili ya uzinduzi wake mapema mwakani.
"Tunapanga kuzindua mwakani katika ukumbi utakaotangazwa ambao siku hiyo itatumika pia kumkumbuka marehemu Steve Kanumba," alisema Lamata.
Lamata alisema mipango kwa ujumla juu ya uzinduzi huo utawekwa bayana kadri siku zitakavyokuwa zikisogea, ila alisisitiza utafanyikia jijini Dar es Salaam.

BASATA yawalilia akina Sharo Milionea

Sharo Milionea enzi za uhai wake





BARAZA la Sanaa la Taifa, BASATA, limetuma salamu za rambirambi na kueleza kusikitishwa na vifo vya wasanii wa watatu wa filamu na muziki nchini vilivyotokea mfululizo wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego baraza hilo limesema limepokea kwa masikitiko makubwa misiba ya wasanii hao ambao ni Khaleed Mohammed 'Mlopelo', John Maganga na Hussein Mkiety 'Sharo Milionea'.
BASATA limedai kuwa vifo vya wasanii hao ni pigo kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na wadau wote wa tasnia nzima ya sanaa nchini kwa kusema inaungana na wote walioguswa na msiba huo.
“Baraza limestushwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa ya vifo hivi vya wasanii hawa John Mganga, Mlopelo na Hussein Mkeity a.k.a Sharo Milionea ambao mchango wao unahitajika sana katika tasnia ya sanaa, pengo waliloliacha ni kubwa kwani ubunifu wao bado unahitajika katika tasnia hii.” Sehemu ya taarifa hiyo inasomeka hivyo.
Taarifa hiyo ikaongeza kuwa; " Baraza linatoa pole kwa familia za marehemu na wasanii wote nchini, aidha linawatakia moyo wa subira katika wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na wapendwa wetu. Tunaomba mwenyezi Mungu azipumzishe mahala pema peponi roho za marehemu.
BASATA likaongeza kuwa wapo pamoja na familia za marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, tutambue kuwa haya ni mapenzi ya Mungu.
Salamu hizo zimekuja wakati watanzania wakiendelea kuomboleza vifo vya wasanii hao pamoja na kile cha muimbaji wa taarab wa kundi la TOT -Plus, Mariam Khamis 'Paka Mapepe' kilichotokea wiki tatu zilizopita wakati akijifungua mwanae wa pili.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego


Man Bizo: 'Mvunja mbavu' anayetaka jamii iwathamini walemavu

Man Bizo akiwa kwenye kiti chake cha magurudu

Man Bizo akiwa na 'swahiba' zake, Mama Shotii na Kazi




KWA mashabiki wa filamu hasa za vichekesho ama wafuatiliaji wa kipindi cha 'vituko show', jina la Man Bizo huenda sio geni masikioni mwao kwa jinsi wanavyosuuzwa roho na umahiri wa msanii huyo mwenye ulemavu.
Man Bizo ambaye majina yake kamili ni Ally Boffu, amejizolea umaarufu mkubwa kwa namna ya uigizaji wake na umbile lake analolitumia vema katika kazi mbalimbali alizoshiriki pamoja na wasanii wenzake.
Msanii huyo amekuwa akikitendea haki kipaji chake cha sanaa sambamba na kile alichodai kutaka kuwaonyesha mfano walemavu wengine kwamba hali walizonazo sio mwisho wa kila kitu katika maisha yao.
Anasema walemavu wakiamua, kuthubutu na kujituma kama anavyofanya yeye ni wazi wanaweza kufika mbali kimaisha na kuepuka utegemezi.
Man Bizo anasema kama asingezingatia mambo hayo huenda kipaji chake kingepotea hivi hivi.
"Kujiamini, kuthubutu na kutaka kuonyesha mfano kwa wengine, ndiko kulikonifikisha hapa," anasema.
Anasema licha ya kukutana na changamoto nyingi, hajakata tamaa kwa vile  anatamani kufika mbele zaidi katika fani hiyo na kubwa kuja kuanzisha asasi ya kuwasaidia walemavu wenzake.
Man Bizo anayefahamika pia kama Kapeto, Jini Mahaba na Kipwinto, anasema tangu utotoni na hata alipokuwa shuleni alipenda kuchekesha watu, lakini hakuota kuja kuwa muigizaji nyota.
"Sikuota kuja kuwa muigizaji mkali kwa mazingira niliyokulia, ila kuvutiwa na msanii aitwae Zimwi na kujiamini kulinifanya nijitose rasmi mwaka 2007 na ninashukuru yapo mafanikio ya kujivunia" anasema.
Anasema licha ya umaarufu, sanaa pia imemwezesha apate ajira katika kampuni ya Al Riyamy na kumiliki maktaba ya kuuzia na kukodia kanda za filamu (video library) inayomuingizia pato la ziada.
"Nashukuru Mungu tangu nijitose kwenye sanaa, nimepata umaarufu, kupata ajira na kumiliki 'video library' na nina kila kitu katika nyumba yangu," anasema.

MUZIKI
Man Bizo anayependa kula ugali kwa mboga za majani na kunywa kinywa juisi,  ni mshabiki wa klabu ya Simba akiwazimia manahodha, Juma Kaseja na Haruna Moshi 'Boban'.
"Huniambii kitu kwa Simba, naipenda mno klabu hii na navutiwa na Kaseja na Boban, ila kimataifa mie ni mnazi wa Manchester United," anasema.
Msanii huyo anasema mbali na uigizaji, pia ni mahiri katika muziki akiwa mbioni kwa sasa kupakua albamu akitanguliza kwanza nyimbo tatu mpya.
Anasema nyimbo hizo tatu ameziimba akishirikiana na wasanii wakali kama Karapina, Dully Sykes na Prince Amigo na kudai kuwa kujitosa kwake kwenye fani hiyosio kwa kubahatisha bali ni kipaji alichonacho.
"Nilipokuwa nasoma Shule ya Jeshi la Wokovu, nilikuwa naimba hivyo kuibukia kwangu kwenye muziki sio kwa kubahatisha ila najua ninachokifanya," anasema.
Muigizaji huyo mwenye matumaini ya kuja kutamba zaidi ndani na nje ya nchi katika fani zote za muziki na uigizaji, anasema hakuna tukio la furaha kwake kama siku alipokabidhiwa nyumba ya urithi wa baba yake.

MTOTO
Man Bizo anasema hakuna tukio la huzuni linalomuuma mpaka leo kama lile la kukataliwa na kunyang'anywa mtoto  kwa kile alichodai hali yake ya ulemavu.
Anasimuliwa kuwa, alikuwa na mahusiano na msichana mmoja aliyekataa kumtaja jina la kumpa ujauzito aliokuja kujifungua mwaka 2009 mtoto wa kike ambaye alimtaja kwa jina la Lilian, ambaye ana umri wa miaka mitatu kwa sasa.
Anasema hata hivyo familia ya msichana huyo ilionyeshwa kuchukizwa na kitendo cha msichana huyo kuzaa naye na hivyo kumkana na kumnyima mtoto huyo anayedai anampenda kupita maelezo.
Hata hivyo Man Bizo anasema kwa sasa familia hiyo imemkubali kwa shingo upande na mama watoto wake wamekuwa wakimpeleka mwanae kwake kumuona, kitu kinachomfariji ingawa bado hajasahau tukio alilofanyiwa siku za nyuma.
"Lilian ni mwanangu na ninampenda mno, kwa sasa mie najipanga kufunga ndoa ili niweze kumtunza vema," anasema.
Akaongeza kuwa, suala la unyanyapaa dhidi ya walemavu ndani ya jamii ni kitu  kinachokatisha tamaa na kuonyesha namna gani baadhi ya watu wanashindwa  kuitambua uwepo wa Mungu na fani yake ya uumbaji.
"Nadhani jamii inapaswa kubadilika na kuwaona walemavu kama watu wengine licha ya kasoro za maumbile," anasema.

MAN BIZO
Ally Boffu 'Man Bizo' alizaliwa Julai 7, 1984 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto wa nne wa familia yao na Elimu ya Msingi aliisoma katika Shule ya Jeshi la Wokovu alipohitimu darasa la saba.
Alijitosa kwenye sanaa mwaka 2007 katika kundi la MCAP, na filamu yake ya kwanza ikiwa ni 'Olopong', kabla ya kushiriki 'Kiroba' na 'Vyumba Vimejaa' anayodai ndiyo iliyomtangaza zaidi na kumpa nafasi ya kucheza filamu nyingine zinazokaribia 50.
Baadhi ya kazi aliocheza msanii huyo anayeiomba serikali kuisaidia fani ya sanaa nchini kutoa tija kwa wasanii na kuondoka na unyonyaji wanaofanyiwa na baadhi ya watu wachache ni pamoja na 'Kitimtim', 'Hekaheka', 'Mishemishe', 'Kichefuchefu', 'Jazba' na 'Koziman'.
Man Bizo, anayewashukuru bosi wake, Khalfan Abdallah, Madhila Piana na wasanii wenzake wote anasema kubahatika kuigiza na wasanii wakubwa na wenye majina kama King Majuto, Kitale, Mzee Jangala, Sharo Milionea na wengine kwake ni fahari kubwa.
Juu ya ugonjwa wa Ukimwi, Man Bizo anasema kila mtu ndani ya jamii anapaswa kupambana nao kwa sababu umekuwa na madhara na kukatisha ndoto za watu wengi.
Msanii huyo anasema kitu cha muhimu watu ni kuwa waaminifu katika ndoa zao, kumcha Mungu na kuepuka anasa zinazoweza kuywapelekea kuangukia katika mapenzi yasiyo salama.
Man Bizo (aliyekaa kulia) akiwa na wasanii wenzake wa 'Vituko Show'



Man Bizo (kulia) akiwa na 'swahiba' yake Seleman Kazi

Sare tu kuivusha Kilimanjaro Stars ribi fainali

Kikosi cha Kilimanjaro Stars


Na Somoe Ng'itu, Kampala

Kilimanjaro Stars leo inahitaji angalau sare dhidi ya Somalia katika mchezo wa mwisho wa Kundi B la Kombe la Chalenji mjini hapa ili kukata tiketi ya kucheza robo-fainali.
Endapo itapata sare, Stars yenye pointi tatu sawa na Sudan katika kundi hilo inaweza kufuzu kama moja ya 'best liza' wawili katika mchezo utakaoanzia saa 8:00 kwenye Uwanja wa Lugogo jijini hapa, baada ya ushindi wa Kenya dhidi ya Somalia jana kumaanisha mshindi wa tatu wa Kundi A ana pointi tatu tu.
Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, alisema jana kuwa ameiona Somalia katika mechi zake mbili zilizopita hivyo hatawadharau kwa sababu ni timu inayoimarika kadri inavyocheza mechi.
Poulsen alisema amejipanga kupata ushindi, hata hivyo, ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika kundi hilo baada ya kupoteza mechi yake ya pili dhidi ya Burundi iliyofanyika Jumatano kwenye uwanja wa Namboole ambao ulijaa maji na matope kufuatia mvua zinazonyesha mfululizo jijini  hapa.
"Wapinzani wetu wanaimarika kila siku zinavyokwenda, tutaingia uwanjani ili kusaka ushindi na si kuwadharau," alisema kwa sababu "timu zote zimekuja kupambana na ndio maana hakuna anayekata tamaa hata  kama amefungwa mechi zote."
Poulsen alisema hali ya beki wake, Shomary Kapombe na kiungo, Mwinyi Kazimoto zinaendelea vyema na watakuwepo kwenye kikosi kitakachoshuka dimbani kuivaa Somalia.
Naye Kocha Mkuu wa Somalia, Sam Ssimbwa, aliliambia gazeti hili juzi kwamba wamekuja Kampala kupambana ingawa wachezaji wake hawana uzoefu wa mechi za kimataifa ukilinganisha na wapinzani wao.
Ssimbwa ambaye alikuwa akiifundisha Sofapaka ya Kenya alisema hana majeruhi kwenye timu yake na amejiandaa kucheza kwenye hali yoyote kwa sababu mazingira ya viwanja vya Afrika yanajulikana.
Mbali na mechi hiyo, leo pia saa nane mchana Burundi na Sudan zilizoko kundi B zitashuka kwenye uwanja wa Wankulukuku na baadaye Malawi itakutana na Zanzibar wakati Rwanda itaikaribisha Eritrea kuanzia saa 10:00 jioni kwenye uwanja huo.
Mabingwa watetezi na wenyeji Uganda Cranes, Zanzibar na Burundi tayari wameshakata tiketi ya kucheza robo fainali ya mashindano hayo ya kila mwaka.

Nguo alizovuliwa Sharo Milionea zakamatwa



Na Steven William, Muheza
Polisi ya Tanga imekamata mali kadhaa za marehemu msanii wa filamu na muziki wa bongofleva Sharo Milionea, ikiwemo suruali ya jeans na fulana alizokuwa amevaa, vilivyoibwa baada ya kupata ajali ya gari na kufariki papo hapo katikati ya wiki wilayani hapa.
Msako wa nyumba hadi nyumba uliofanywa na polisi kwa ushirikano na wananchi ulifanikisha kupatikana kwa tairi la akiba la gari alilokuwa akiendesha, radio ya gari na betri ya gari.
Vitu vingine vilivyopatikana ni simu yake ya mkononi, saa ya mkononi, suruali aina ya jeans na fulana ambavyo marehemu alivuliwa na kuachwa na chupi tu.
Akizungumza na Nipashe juzi usiku, mkuu wa wilaya ya Muheza Subira Mgalu alisema watu kadhaa waliokutwa na mali hizo za marehemu kwenye kijiji cha Maguzoni wanashikiliwa na polisi.
Sharo Milionea alifariki baada ya gari alililokuwa akiendesha aina ya 'Toyota Harrier' kupasuka tairi la mbele akiwa katika mwendo kasi na kupinduka mara kadhaa wakati akitoka Dar es Salaam.
Mgalu alisema msako huo wa nguvu uliohusisha jeshi la polisi na raia wema wa kijiji cha Maguzoni ulifanyika usiku kwa kupita nyumba hadi nyumba.
Mgalu alisema msako huo bado unaendelea, na jeshi la polisi linaongozwa na Kamanda wa Wilaya ya Muheza Endrew Satta.
Juzi mkuu huyo wa wilaya alitoa siku mbili vitu hivyo viwe vimerudishwa vinginevyo msako mkali wa nyumba hadi nyumba ungefanyika kijijini hapo.
Milionea alipata umaarufu mkubwa kwa kuigiza kama mchekeshaji msafi tofauti na wengi ambao huamini mchekeshaji ni lazima avae vinyago, kikatuni ama ajipake masizi.
Misemo yake ya "kamata mwizi meen", "umebugi meen!" na "ohh mamma!" ilimpa mashabiki wengi; hasa watoto.

Chanzo:NIPASHE JUMAMOSI

GUNDU LAKUMBA UZINDUZI WA MASHUJAA, KISA UMEME

Kiiipe Yayooo...! Mwanamuziki JB Mpiana na bendi yake wakifanya vitu vyao baada ya kupanda stejini kwenye viwanja vya Leaders Club, Kionondoni jijini Dar es Salaam  usiku wa kuamkia leo. Hapa ilikuwa ni mida ya saa 9:00 baada ya gwiji huyu kusubiri sana kutokana na mizinguo ya umeme wa TANESCO na pia wa jenereta kubwa lililotegemewa mahala hapo kuzalishia nishati hiyo usiku wa kuamkia leo (Desemba 1, 2012).
Litapona kweli...? Watu wakiwa wamelizunguka jenereta lililokuwa linawazingua wakati wa uzinduzi uliofeli wa albamu ya pili ya mashujaa kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Jumamosi (Desemba 1, 2012). (Picha: Zote kwa Hisani ya issamichuzi.com)
Gundu la aina yake limeikumba bendi ya Mashujaa inayoundwa na wanamuziki kadhaanyota akiwamo Chaz Baba baada ya uzinduzi wake kukwama usiku wa kuamkia leo kutokana na kukatika hovyo kwa umeme wa TANESCO na pia 'mizinguo' ya kuwaka na kuzima kila mara kwa jenereta kubwa liliotarajiwa kutoa huduma ya nishati hiyo kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa mizinguo hiyo ya umeme ilimchanganya kuliko kawaida mmiliki wa bendi ya Mashujaa, Mamaa Sakina, ambaye inasemekana alianguka na kupoteza fahamu kiasi cha kukimbiziwa hospitali akiwa hoi.

Tatizo hilo lilidumu kwa masaa kibao na kuwafanya mafundi kuihangaikia jenereta huku na huko huku mwanamuziki wa kimataifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyealikwa kusindikiza uzinduzi wa albamu hiyo, JB Mpiana akilazimika kusubiri sana --  hadi mishale ya saa 9:00 usiku -- ndipo alipopata nafasi ya kupanda jukwaani na kundi lake kufanya kazi iliyowapa fursa ya kutua nchini kwa mbwembwe.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki walishakereka mida hiyo na kutimkia zao, hivyo kukosa uhondo uliotarajiwa katika onyesho hilo ambalo awali lilikuwa na ratiba 'tamu' sana kwa wapenzi wa burudani.

Hakukuwa na taarifa za kina kuhusiana na hali ya kiafya ya Mamaa Sakina hadi kufikia leo asubuhi ya leo (Jumamosi Desemba 1, 2012); kwa mujibu wa chanzo chetu.

Thursday, November 29, 2012

KUMUONA JB MPIANA NI KWA 100,000



 JB Mpiana akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu shoo yake itakayofanyika Leaders Club Novemba 30.
Mtangaji wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Said Kilumbanga (kulia) akiwa amepozi na wanenguaji wa  mwanamuziki kutoka Congo, JB Mpiana
DAR ES SALAAM, Tanzania
MSANII nguli wa muziki wa dansi Afrika, JB Mpiana amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi na kushuhudia shoo yake itakayopigwa kwenye viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam Ijumaa hii, ambapo kiingilio kwa VIP A itakuwa sh 100,000 na kawaida sh 25,000.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, JB Mpiana alisema, anajikubali na kuithamini kazi yake ambayo anaifanya na kuahidi kuwapa raha wapenzi na wadau mbalimbali wa muziki hapa nchini ambao watajitokeza siku hiyo.

“Kwanza nimefurahia sana mapokezi ya jana, hivyo basi nitawapa raha siku hiyo na pia nawapongeza waandaaji kwa kuona umuhimu na kuniteua mimi kufanya nao kazi siku hiyo, nimekuja na kikosi changu kamili cha watu 25, hivyo basi nina imani siku hiyo itakuwa raha sana,” alisema Mpiana.

Mpiana aliwataka wanamuziki wa hapa nchini, kujituma na kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na kuziheshimu pia, ili waweze kufikia mafanikio ambayo wamejipangia kuyafikia, kwa kuwa hata yeye alianzia huko na ndio sababu amefikia hapa alipo.

Naye Mkurugenzi wa QS J Mhonda Entertainment, Joseph Mhonda, alisema kila kitu kimekamilika na kudai kuwa, kwa sasa wanasubiri siku ifike ili watanzania wapate raha na kile ambacho wamekitarajia.
Mhonda alisema, viingilio siku hiyo itakuwa sh 25,000 kwa atakayenunua tiketi mapema, huku 30,000 kwa watakaonunulia mlangoni na sh 100,000 VIP A kwa watakaonunua mapema huku kwa mlangoni ni sh 150,000.

Aliongeza kuwa, Mpiana ataanza kufanya shoo ukumbi wa Triple A, jijini Arusha na baadaye jijini Mwanza katika ukumbi wa Villa Park huku wasanii mbalimbali wakitarajiwa kutumbuiza siku hiyo ambao ni Ney Wamitego, H Baba, Mashujaa pamoja na Mb Dog.

BONDIA TYSON FURY KUMVAA WLADIMIR KLITSCHKO MWAKANI



LONDON, England
“Nimezungumza mara kadhaa na kocha wa Wladimir, Bernd Boente kuhusu pambano hilo na Tyson yu tayari sasa kwa hilo. Ni mpambano ambao unaweza kuwa katika uwanja wa soka katika kipindi cha kuanzia Mei, Juni au Julai
BONDIA mahiri Tyson Fury amepania kupanda ulingoni kupimana ubavu na Wladimir Klitschko kuwanuia ubingwa wa dunia kiangazi kijacho.
Fury, 24, bondia asiyepigika katika uzani wa ‘heavyweight,’ Jumamosi hii anapanda ulingoni kumvaa Mmarekani Kevin Johnson jijini Belfast, Ireland ya Kaskazini.
Na promota wa pambano la Jumamosi Mick Hennessy amedai kuwa, ushindi kwa Fury mwenye urefu wa futi 6.9, utampa fursa ya kuandaliwa pambano dhidi ya Klitschko - bingwa wa mikanda ya WBA, IBF, na WBO.
Hennessy alisema: “Nimezungumza mara kadhaa na kocha wa Wladimir, Bernd Boente kuhusu pambano hilo na Tyson yu tayari sasa kwa hilo.
“Ni mpambano ambao unaweza kuwa katika uwanja wa soka katika kipindi cha kuanzia Mei, Juni au Julai.
“Ujerumani ni nchi inayoweza kuwa kipaumbele chetu kupigwa pambano hilo, lakini nimeshazungumza na wamiliki wa Uwanja wa Old Trafford au Croke Park,” alisema Hennessy.
You might also like:

Waziri Mathayo, Nape kuwashuhudia Miyeyusho, Nassib PTA

Mabondia Francis Miyeyusho (kushoto) na Nassib Ramadhani watakaopigana Desemba 9


WAKATI mabondia Francis Miyeyusho na Nassib Ramadhani wakitarajiwa kupima uzito Desemba 8 kabla ya kuvaana kuwania ubingwa wa Mabara wa WBF, viongozi waalikwa watakaoshuhudia pambano hilo wamefahamika.
Promota wa pambano hilo litakalofanyika jijini Dar siku ya Desemba 9, Mohammed Bawazir aliiambia MICHARAZO, miongoni mwa viongozi hao waalikwa ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo.
Bawazir alisema mbali na Dk Mathayo, wengine waliothibitisha kushuhudia pambano hilo la uzani wa Bantam ni pamoja na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Katibu wa Itikidi na Uenezi-CCM, Nape Nnauye.
"Hao  ni baadhi ya viongozi wakuu tuliowatumia mwaliko na kutuhakikishia watahudhuria na tutamtangaza mgeni rasmi siku ya Desemba 6," alisema.
Promota huyo alisema wangependa mgeni rasmi katika pambano hilo awe mmoja wa viongozi wa juu wa Taifa na ndiyo maana wanaendelea kusubiri majibu ya mwaliko wao kabla ya kumtangaza jina katika mkutano wao ujao.
Juu ya maandalizi ya pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kutokana na ubora na rekodi za mabondia hao wawili, Bawazir alisema yanaendelea vema japo wamekwama kupata wadhamini wa kuwapiga tafu.
Bawazir alisema pamoja na hayo bado wanaendelea kuitoa wito kwa watu wenye mapenzi mema na mchezo wa ngumi kujitokeza kuwapa nguvu, huku akisema upimwaji wa uzito na afya kwa mabondia utafanyika Desemba 8.
"Maandalizi yaendelea vema japo wadhamini wanasuasua kujitokeza na mabondia wote watapimwa kupimwa uzito na afya zao Desemba 8, siku moja kabla ya kupanda ulingoni," alisema.
Pambano hilo litafanyika chini ya usimamizi wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, PST na litatanguliwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Michezo hiyo ya utangulizi ni kati ya Fadhili Majia vs Juma Fundi, Mohammed Matumla dhidi ya Doi Miyeyusho, Ibrahimu Class vs Said Mundi, Fred Sayuni dhidi ya Deo Samwel na Hassan Kidebe dhidi ya Baina Mazola.

Mwisho