STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 8, 2013

Uganda Cranes kutua nchini Alhamisi

Mabingwa wa Kombe la Kagame, The Cranes wanaokuja kuivaa Stars
TIMU ya soka ya taifa ya Uganda (The Cranes) inatarajia kutua nchini Alhamisi Julai 11 kwa ajili ya mechi yao ya kwanza dhidi ya wenyeji timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Stars na Cranes zinakutana katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Afisa Habari wa Chama cha Soka cha Uganda (FUFA), Rogers Mulindwa, alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kitawasili kikiwa chini ya kocha wake mpya, Mserbia Sredojovic Milutin 'Micho'.
Mulindwa alisema kuwa wana imani na kikosi hicho ambacho kimefanya maandalizi ya muda mrefu licha ya kukosa mchezo wa kirafiki kama walivyotarajia awali.
"Mipango ya kucheza dhidi ya Iraq ilipotea baada ya kukosa kibali kutoka FIFA, ila tuko tayari kuivaa Tanzania na wakati huu tutakuja tofauti," alisema Mulindwa.
Aliongeza kuwa kila mchezaji na shabiki wa soka wa Uganda anafahamu kwamba mashindano ya CHAN ndiyo yaliyobakia kwao baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali zilizopita za AFCON na Kombe la Dunia 2014 ikiwa ni kazi kubwa.
"Tumechoka kuwa wasindikizaji, tumejiandaa ili kushiriki mwakani, tunakuja kupambana na tutamalizia kazi katika mchezo wa pili nyumbani (Kampala)," Mulindwa aliongeza.
FUFA ilifanya mazungumzo na Iraq na kama wangepata ruhusa mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Cranes na wenyeji wao Iraq ulipangwa kufanyika kesho.
Cranes haijawahi kushiriki fainali hizo zinazofanyika kwa mara ya tatu ambapo mwaka 2007 katika mashindano hayo ilitolewa na Taifa Stars iliyokuwa chini ya kocha Mbrazil Marcio Maximo kwa jumla ya magoli 3-2.
Stars iliyocheza fainali hizo zilizofanyika Ivory Coast, ilishinda magoli 2-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza na katika mechi ya marudiano iliyochezwa Kampala walimaliza kwa sare ya 1-1.
Wakati huo huo, kikosi cha Stars kilichoko chini ya kocha Kim Poulsen, kinaendelea na mazoezi yake kama kawaida kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment