STRIKA
USILIKOSE
Sunday, August 11, 2013
Benchi la Ufundi linachekaaaaaa!
BENCHI la ufundi la klabu ya Yanga limeusifia usajili wao iliyofanya safari hii na kutamba kuwa hawaoni cha kuwazuia kutetea tena taji lao la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro, aliiambia MICHARAZO kuwa, kwa namna usajili wao ulivyofanywa kwa umakini mkubwa na hasa safu yao ya mbele kunawapa nafasi ya kuwa ya kutetea taji lao na kufanya vyema kwenye mechi za kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Minziro alisema, msimu wa 2013-2014 unaoatarajiwa kuanza wiki mbili zijazo utakuwa wao kwa kuringia wachezaji iliyonayo na namna wanavyojiandaa, huku wakiionya mapema Azam kwamba wajiandae na kipigo Jumamosi katika mechi ya Ngao ya Hisani.
Yanga na Azam zitaumana katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuashiria kuanza kwa msimu mpya, ambapo wana lamabalamba wenyewe walijichimbia Afrika Kusini na wanatarajiwa kuwasili kesho baada ya kambi ya wiki moja ugenini.
"Kikosi kipo imara na vijana wanatuma matumaini makubwa ya kufanya vyema msimu huu kuliko ilivyokuwa msimu uliopita. Kifupi tunaamini tutatetea taji letu kwa sababu hatuoni kitu cha kutuzuia kuanzia kikosi tulichonacho hadi maandalizi tuliyofanya," alisema.
Minziro aliongeza kushika kwa wepesi kwa maelekezo ya makocha kwa wachezaji wageni kikosini kunawafariji na kuwapa fursa ya benchi lao kumtumia mchezaji yeyote wakati wowote katika mechi yoyote bila tatizo.
"Wachezaji wageni wameshika haraka maelekezo kitu ambacho kimeturahisishia kazi na ndiyo maana tunaamini kwa silaha hizi tulizonazo sijui kama kuna timu itakayofua dafu mbele yetu," alisema Minziro beki wa zamani wa kimataifa wa Yanga na Taifa Stars.
Yanga inatarajiwa kukata utepe wa Ligi Kuu kwa kuumana na Ashanti United ambayo imejichimbia Kigoma na mwishoni mwa wiki wanatarajiwa kucheza mechi mbili na timu za nchini Burundi walikozifuata ili kujiweka fiti kabla ya kuwavaa watetezi hao wa ligi.
Jioni ya leo iliendeleza ubabe katika mechi zake za kirafiki za kujipima nguvu kwa kuilaza SC Villa ya Uganda kwa mabao 4-1 ikiwa ni ushindi wa tatu mfululizo baada ya awali kuilaza Mtibwa Sugar 3-1 kisha kuikamua kiduchu 3 Pillars ya Nigeria kwa bao 1-0.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment